Tafseer ya Surah Zilzaal

بِسْمِ اللّٰهِ الرَّحْمٰنِ الرَّحِيمِ

إِذَا زُلْزِلَتِ الْأَرْضُ زِلْزَالَهَا ‎﴿١﴾‏ وَأَخْرَجَتِ الْأَرْضُ أَثْقَالَهَا ‎﴿٢﴾‏ وَقَالَ الْإِنسٰنُ مَا لَهَا ‎﴿٣﴾‏ يَوْمَئِذٍ تُحَدِّثُ أَخْبَارَهَا ‎﴿٤﴾ بأن ربك أوحى لها ﴿٥﴾ يَوْمَئِذٍ يَصْدُرُ ٱلنَّاسُ أَشْتَاتًا لِّيُرَوْا أَعْمٰلَهُمْ ‎﴿٦﴾ ‏فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُۥ ‎﴿٧﴾‏ وَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَهُۥ ‎﴿٨﴾‏

Itakapotetemeshwa ardhi kwa mtetemesho wake. Na ardhi itakapotoa mizigo yake yote. Na watu watasema: Kumetokea nini? Siku hiyo itasimulia habari zake zote, kwa sababu Mola wako atakuwa ameiamrisha. Siku hiyo watu watarejea (kutoka mahali pa kuhesabiwa) makundi mbali mbali, ili waonyeshwe (matunda ya) matendo yao meema. Basi anayefanya jambo jema (hata) kwa uzito wa chembe, ataliona. Na anayefanya uovu (hata) kwa uzito wa chembe, atauona.

إِذَا زُلْزِلَتِ الْأَرْضُ زِلْزَالَهَا ‎﴿١﴾‏ وَأَخْرَجَتِ الْأَرْضُ أَثْقَالَهَا ‎﴿٢﴾‏ وَقَالَ الْإِنسٰنُ مَا لَهَا ‎﴿٣﴾‏

Itakapotetemeshwa ardhi kwa mtetemesho wake. Na ardhi itakapotoa mizigo yake yote. Na watu watasema: Kumetokea nini?

Siku ya Qiyaamah, ardhi itaanza kutetemeka na kutikisika. Itatupa mizigo yake yote na itadhihirisha chochote kilichomo ndani ya tumbo lake.

Mizigo inayotupwa nje na ardhi inahusu watu waliozikwa makaburini na hazina, iwe dhahabu, fedha, rubi, almasi, na vitu vingine vilivyofichwa katika ardhi. Hazina hizi zitakuwa zimetawanyika chini bila kutunzwa, ili kudhihirisha kutokuwa na thamani kwao mbele ya viumbe siku hiyo.

Kwa mujibu wa Hadithi sahihi iliyopokelewa na Imaam Muslim (rahimahullah): “Muuaji atakuja na kusema, ‘Ni kwa hili nilimuuwa mtu?’ Yule aliyevunja undugu kwa ajili ya mali atakuja na kusema, ‘Ni kwa hili nilivunja undugu?””

Kwa hiyo, dunia itafunua habari zake zote kuhusu matukio yaliyopita humo. Itadhihirisha matendo mema na mabaya ambayo watu walikuwa wameyafanya juu yake. Siku hiyo, mwanadamu atashuhudia ardhi ikitupa mizigo yake na kutoa habari, na kwa mshangao atauliza, “Kumetokea nini na ardhi?

يَوْمَئِذٍ تُحَدِّثُ أَخْبَارَهَا ‎﴿٤﴾

Siku hiyo itasimulia habari zake zote.

Imepokewa kutoka kwa Abu Hurairah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasulullah (Sallallaahu ‘alaihi wasallam) aliielezea aya hii kwa kusema: “Ardhi itashuhudia matendo yote yanayofanywa na watu juu yake, wakiwa wanaume au wanawake.

يَوْمَئِذٍ يَصْدُرُ النَّاسُ أَشْتَاتًا لِّيُرَوْا أَعْمَالَهُمْ ‎﴿٦﴾

Siku hiyo watu watarejea (kutoka mahali pa kuhesabiwa) makundi mbali mbali, ili waonyeshwe (matunda ya) matendo yao meema.

Katika dunia hii, watu huonekana pamoja bila utengano wowote. Lakini, siku hiyo, Allah Ta’ala Atawagawanya watu makundi tofauti kwa mujibu wa matendo yao. Watu wema watakuwa kundi tofauti na watu waovu watakuwa kundi tofauti. Kwa namna hii, matokeo ya matendo ya watu yatafichuliwa mbele ya watu.

فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ ‎﴿٧﴾‏ وَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَهُ ‎﴿٨﴾

Basi anayefanya jambo jema (hata) kwa uzito wa chembe, ataliona. Na anayefanya uovu (hata) kwa uzito wa chembe, atauona.

Tendo la mtu, hata sawa na uzito wa chembe, litaonekana. Kwa hivyo, mwanadamu hatakiwi kamwe kuzingatia hatua yoyote kuwa ndogo au isiyo na maana. Mtu anapaswa kuthamini kila kitendo kidogo na kuogopa kila tendo ovu, licha ya jinsi linaweza kuonekana kuwa ndogo. Inawezekana kwamba kitendo kidogo ambacho kinachukuliwa kuwa akina maana, kinaweza kuwa njia ya wokovu wake na kufaulu huko akhera. Vile vile, inawezekana kwamba tendo dogo la uovu linaweza kuwa njia ya kuangamia kwake.

About admin

Check Also

Tafseer Ya Surah Lahab

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ تَبَّتْ يَدَا أَبِي لَهَبٍ وَتَبَّ ‎﴿١﴾‏ مَا أَغْنَىٰ عَنْهُ مَالُهُ وَمَا كَسَبَ ‎﴿٢﴾‏ سَيَصْلَىٰ نَارًا …