Tafseer Ya Surah Faatihah

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ ‎﴿١﴾‏ الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ‎﴿٢﴾‏ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ ‎﴿٣﴾‏ مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ ‎﴿٤﴾‏ إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ ‎﴿٥﴾‏ اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ ‎﴿٦﴾‏ صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا الضَّالِّينَ ‎﴿٧﴾‏

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa ulimwengu wote. Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu. Mfalme wa Siku ya kuhukumu. Wewe peke yako tunakuabudu, na Wewe tu tunakuomba msaada. Tuonyeshe njia iliyonyooka – njia ya wale uliowafadhilisha (kwa fadhila Yako), sio njia ya waliokasirikiwa na njia ya waliopotea.

Surah Ya Kwanza

Surah Faatihah ni surah ya kwanza ndani ya Qur’an Tukufu. Sio tu surah ya kwanza katika pangilio za surah ya Qur’an, lakini pia ni surah ya kwanza kuteremshwa na Allah Ta‘ala. Kabla ya kuteremshwa kwa Surah Faatihah, ingawa aya za mwanzo za Surah Alaq na Surah Muddathir ziliteremshwa, lakini hakuna Sura kamili iliyoteremshwa kabla yake.

Sababu ya Surah Faatihah kuwekwa mbele ya kila Sura nyingine ya Qur’an Majeed ni kwamba Sura Faatihah ndio asili ya Qur’an Majeed, na katika mada yake, inajumuisha dhamira kuu tatu za Qur’an Majeed. Kwa hiyo, sehemu zote zingine katika Qur’an Majeed zinazofuata baada ya Surah Faatihah ni kama maelezo yake katika kufafanua mada zake kuu tatu.

Mada Tatu Kuu Za Qur’an Takatifu

Kimsingi, elimu iliyomo ndani ya Qur’an Takatifu yote inahusiana na mojawapo ya mada kuu tatu; (1) kuleta Imaan katika umoja wa Allah Ta‘ala na katika sifa Zake takatifu, (2) kutekeleza A’amaal-ul-Swaalihah (amali njema), (3) maisha ya Akhera.

Kanuni za msingi za mada zote hizi tatu kuu zimerejelewa na kuonyeshwa katika Surah Faatihah. Ni kwa sababu hii kwamba miongoni mwa majina ambayo Surah Faatihah imetolewa, kama ilivyotajwa katika Ahaadith, ni majina “Ummul Qur-aan” (Mama wa Qur’an), “Ummul Kitaab” (Mama wa Kitabu), na “Al-Qur’an-ul-Adhim (Qur’an Tukufu)”.

Ujumbe Wa Surah Faatihah

Mtu anapochunguza mada ya surah hii, anatambua kwamba ni ujumbe kutoka kwa Allah Ta’ala kwa mwanadamu kuhusiana na jinsi anavyopaswa kumuomba Allah Ta’ala na kutafuta mwongozo kutoka Kwake. Kwa hiyo, katika surah hii mtu anamuomba Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) amwonyeshe njia ya wale waliofadhiliwa na Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) na amuepushe na njia ya wale walioighadhibikiwa na njia ya waliotumia kupotea.

Allah Ta’ala anajibu dua hii ya mwanaadamu kwa kumpa muongozo ambao uliteremshwa katika Qur-aan nzima baada ya Surah hii. Kwa hivyo, ni kwamba sehemu nzima ya Qur-aan Takatifu uliosalia ni jibu kwa dua hii ya mwanadamu katika Surah Faatihah.

Mtazamo Wa Ujumbe Wa Surah Faatihah

Mtazamo wa ujumbe wa surah hii ni kwamba ili mtu afaidike na Quran Takatifu, anatakiwa kuleta imaan katika vipengele vya msingi vya imani k.m. (1) Kuamini umoja wa Allah Taala (2) Kuamini sifa zake zote nzuri (3) Kuamini kama kuna maisha ya akhera (4) Kuamini hisabu ya siku ya qiyama (5) Kuamini risaalah (utume) wa Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) (6) Kufuata njia ya wachamungu (Ambiyaa[‘alaihimus salaam]) (7) Kujiepusha na njia ya maadui wake yanayomfanya mtu kum’aasi Allah Ta’ala.

Vile vile surah hii inamuelekeza mwanadamu katika kufikia lengo lake kwa kurejea kikamilifu kwa Allah Ta’ala kwa kumuabudu yeye pekee, kuomba mwongozo na msaada kutoka Kwake.

Iwapo mtu atasoma surah hii na akaisoma kwa akili iliyo wazi na moyo mnyofu, kama mtafutaji ukweli wa haki, bila shaka atabarikiwa na mwongozo wa kweli kutoka kwa Allah Ta’ala.

Fadhila za Surah Fatiha

Kuhusiana na fadhila za Surah Faatihah Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) amesema kuwa surah hii ni tiba ya kila aina ya maradhi. Kwa mujibu wa Hadith nyingine, surah hii pia inaitwa “As-Shifaa” (Tiba ya Maradhi Yote).

Imepokewa pia kutoka kwa Anas (radhiya allaahu ‘anhu) kwamba Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) ameiita surah hii kuwa ni surah kuu kati ya surah zote za Qur’an Takatifu.

Katika Hadith nyingine, Abu Hurairah (radhiya allaahu ‘anhu) anasimulia kwamba Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) amesema: “Naapa kwa Allah Ta’ala, ambaye ni Mola wa maisha yangu, kwamba si Tawrah, wala Injili wala Zabuur wala sehemu nyingine yoyote ya Qur’an inaweza kulinganishwa na Sura Faatiha.”

Maulamaa wanaeleza kwamba vitabu vya Allah Ta’ala yanafikia takriban 104, na ujumbe za vitabu hizi zote zimo katika vitabu vinne mashuhuri; Zabuur, Tawrah, Injili na Qur’an. Ujumbe mtukufu wa vitabu hivi vyote umefupishwa ndani ya Qur-aan, na ujumbe wa kimsingi wa Qur-aan umeingizwa ndani ya Surah Faatihah. Zaidi ya hayo, ujumbe wa Surah Faatihah unaweza kupatikana kwa ufupi katika maneno “Bismillahir Rahmaanir Raheem”.

Asili Ya Bismillah

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ ‎﴿١﴾

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rahma, Mwenye kurehemu

Ilikuwa ni tabia na njia ya watu katika zama ya kabla ya Uislamu kwamba wanapoanza kazi yoyote au kuanza mradi wowote, walichukua majina ya masanamu yao ili kupata baraka. Allah Ta’ala alivifuta vitendo hivi viovu vya wapagani na akawaagiza kwamba badala ya kuchukua majina ya mungu zao wa uwongo, wanapaswa kutaja jina la Allah Ta’ala wanapoanza kazi yoyote au kuanza mradi wowote.

Kwa hakika, maisha ya Muumini yanatawaliwa na imani na yakini kwamba ni kwa neema ya Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) tu na usaidizi wa Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) ndipo matendo yote yanatimizwa. Kwa hivyo, Muumini anafundishwa kusoma Bismillah wakati wa kufungua au kufunga mlango, wakati wa kufunika chombo chochote, wakati wa kula au kunywa, wakati wa kuanza safari, wakati wa kupanda au kushuka kwenye usafiri, nk.

Tunaposema “Bismillah” – kwa jina la Allah, kwa hakika tunasema kwamba tunaianza kazi yetu kwa jina la Allah Ta’ala na kwa usaidizi na baraka Zake tukufu. Kwa maneno mengine, tunakubali kwamba bila Allah Ta‘ala, hatuwezi kufanya kazi yoyote wala kukamilisha kazi yoyote, hata iwe kazi ndogo kiasi gani.

Kimsingi, kila kipengele cha maisha ya Muumini kinapaswa kuanza kwa kuchukua jina la Allah Ta’ala. Hivyo basi, kabla ya kuanza kusoma Qur’an Takatifu, tumeamrishwa kusoma Bismillah. Sababu ya kusoma Bismillah ni kutaka msaada na baraka za Allah Ta‘ala ili uweze kuisoma Qur’an Takatifu kwa usahihi na pia kuweza kuufahamu ujumbe wa Qur’an Takatifu na kupata mwongozo maalum kupitia kitabu cha Allah Ta’ala.

About admin

Check Also

Tafseer Ya Surah Nasr

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ إِذَا جَاءَ نَصْرُ اللَّهِ والْفَتْحُ ‎﴿١﴾‏ وَرَأَيْتَ النَّاسَ يَدْخُلُونَ فِي دِينِ اللَّهِ …