Tafseer Ya Surah Ikhlaas

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ ‎﴿١﴾‏ اللَّهُ الصَّمَدُ ‎﴿٢﴾‏ لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ ‎﴿٣﴾‏ وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ ‎﴿٤﴾‏

Sema (Ewe Muhammad (Sallallahu ‘alaihi wasallam)), Yeye – Allah Ta’ala – ni Mmoja na wa Pekee (katika nafsi yake na sifa Zake). Allah Ta’ala anahitajika kwa wote (viumbe), hali yeye amhitaji yoyote. Hakuzaa, wala hakuzaliwa. Na wala hana anaye fanana naye.

Sura hii inazungumzia imani ya Tawhid (umoja wa Allah Ta’ala katika Utu na Sifa Zake), ambayo ni miongoni mwa imani za kimsingi za Uislamu.

Imani ya Tawhid ilikuwa ni jambo geni kwa wapagani, Mayahudi na Wakristo walioishi zama za Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam).

Kuhusu wapagani (washirikina), basi mbali ya wao kumuamini Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala), walikuwa pia na mungu wengi wengine waliyokuwa wakiiabudu. Pia waliwaita Malaika kuwa ni mabinti wa Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala)

Kwa upande wa Wakristo, waliamini Utatu (yaani Mungu amegawanyika mara tatu) na wakigawanya umungu katika nafsi tatu, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

Waliamini kuwa Yesu (Nabii Isa [alayhis salaam]) ni mwana wa Mungu.

Kuhusu Mayahudi wa Uarabuni waliamini kuwa Uzair (alayhis salaam) ni mwana wa Mungu.

Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alipowaeleza watu imani ya Tawhid na kuwalingania kumuabudu Allah Ta’ala peke yake bila ya kumshirikisha katika Utu Wake na Sifa Zake, watu wengi walianza kutaka maelezo ya ndani ya Allah Ta’ala. .

Ilikuwa ni kujibu maswali yao kwamba surah hii iliteremshwa.

Sura hii inaondoa dhana zote za upotofu kuhusu Allah Ta’ala kwa ufupi, ufasaha na kwa njia ya kuvutia ambao hauwezi kutafsiriwa katika lugha nyingine yoyote.

Kimsingi, surah hii inakanusha aina zote za shirki na inaweka kanuni za kimsingi za Tawhid.

Kuna fadhila nyingi zilizoandikwa katika Hadith kuhusu surah hii.

Katika Hadiyth moja, imetajwa kwamba kusoma surah hii mara moja utapata ujira unaolingana na ujira wa kusoma thuluthi moja wa Qur’an Takatifu.

Vile vile, imepokewa kwamba mtu anayesoma Qul huwallahu tatu (yaani Surah Ikhlaas, Surah Falaq na Surah Naas) asubuhi na jioni, atatosheleka na ulinzi wa matatizo, misiba na msukosuko yote ya siku hiyo.

قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ ‎﴿١﴾‏

Sema (Ewe Muhammad (Sallallahu ‘alaihi wasallam)), Yeye – Allah Ta’ala – ni Mmoja na wa Pekee (katika nafsi yake na sifa Zake).

Makafiri waliposikia kuhusu Allah Ta’ala, basi kwa mzaha wakamwambia Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam), “Tufafanulie nasaba ya Allah Ta’ala.” Baadhi yao walifikia hatua ya kuuliza, “Je, unaweza kutufafanulia ni nyenzo na kitu gani ambacho Allah Ta’ala ameundwa nacho?” Ilikuwa ni katika tukio hilo ambapo surah hii iliteremshwa.

Katika aya ya kwanza ya surah hii, Allah Ta‘ala anajielezea Mwenyewe kwa neno ‘Ahad’. Neno ‘Ahad’ limetafsiriwa kuwa ‘mmoja peke yake’. Neno hili linaashiria kwa Allah Ta’ala kuwa wa kipekee katika dhaat (utu wake) na wa kipekee katika sifa zake zote.

Allah Ta’ala kuwa wa pekee katika dhaat yake (utu waka) ina maana kwamba uwepo wa Allah Ta’ala si kama uwepo wa mwanadamu unakotokea kwa njia yoyote (kama kuzaliwa na wazazi), na pia sio uwepo wa muda ambao utaisha baada ya muda. Bali, kuwepo kwa Allah Ta‘ala ni milele kwa sababu Allah Ta’ala hana mwanzo wala mwisho.

Allah Ta‘ala kuwa wa kipekee katika sifa zake ina maana kwamba kila sifa ya Allah Ta’ala ni ya kipekee na kamilifu. Sifa za Allah Ta’ala hazina mapungufu yoyote kama sifa za mwanadamu. Sifa za mwanadamu zina mipaka. Ikiwa mtu anaweza kuona, basi anaweza kuona tu hadi hatua fulani, na hawezi kuona zaidi ya hatua hiyo. Vile vile ikiwa mtu anaweza kubeba mzigo, basi ana uwezo wa kubeba mzigo hadi uzito fulani tu, na hawezi kubeba mzigo unaozidi uzito huo. Kila sifa wa mwanadamu una mipaka fulani, lakini Allah Ta‘ala hazuiliwi na mipaka yoyote. Kwa hivyo, Allah Ta’ala ni Mkamilifu katika Nafsi Yake na Mkamilifu katika Sifa Zake zote.

اللَّهُ الصَّمَدُ ‎﴿٢﴾

Allah Ta’ala anahitajika kwa wote (viumbe), hali yeye amhitaji yoyote.

Katika aya hii, Allah Ta’ala anajisifu mwenyewe kwa neno ‘As-Samad’. Neno ‘As-Samad’ maana yake ni ‘Mwenye kuhitajika kwa viumbe vyote, hali Yeye amhitaji yoyote’. Kwa maneno mengine, Mwenyezi Mungu ni kiumbe ambaye anajitegemea. Viumbe vwote vinamtegemea yeye kabisa kwa uwepo wao kwa kila wakati, hali yeye hahitaji mtu yoyote au kitu chochote wakati wowote. Hivyo basi, sifa hii ya Allah Ta‘ala, ‘As-Samad’, ni sifa ambayo ni ya kipekee kwa Allah Ta’ala.

Wapagani waliamini kwamba Allah Ta’ala ana mungu wengine wa kumsaidia katika kusimamia mambo ya ulimwengu. Aya hii inatangaza kwamba Allah Ta’ala si mhitaji wa mtu yoyote kumsaidia kwa njia yoyote, bali ni msaada Wake ambao unahitajika na wote kila wakati. Kiumbe anayehitaji msaada kutoka kwa wengine hastahili kuitwa Mungu.

لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ ‎﴿٣﴾‏

Hakuzaa, wala hakuzaliwa.

Katika aya hii, Allah Ta’ala anaeleza kuwa hakumzaa yoyote (yaani hakumzaa mtoto), wala yeye mwenyewe hakuzaliwa na yoyote.

Aayah hii ni jibu kwa maswali ambayo watu wa Makka walimuuliza Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) kuhusu nasaba ya Allah Ta’ala. Wakamwambia Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam), “Tufafanulie nasaba ya Mwenyezi Mungu.”

Allah Ta’ala anawajibu akisema kuwa Yeye ni Mmoja na Peke Yake, na Hakuzaa, wala hakuzaliwa.

Kwa maneno mengine, Allah Ta’ala ni wa milele na hana mwanzo wala mwisho. Vile vile, kuwepo Kwake hakutegemei sababu yoyote au chombo chochote, tofauti na mwanadamu ambaye amezaliwa kupitia njia ya wazazi baada ya Nikaah baina yao.

Baadhi ya dini zingine kama wale wasiomuamini Mungu hawaamini kuwa kuna Mungu. Kwa hivyo, Sura hii inakanusha imani yao na inathibitisha kwamba kuna Mungu ambaye ni Allah Ta‘ala, Mungu Mmoja na wa Pekee ambaye ni wa milele na wa pekee katika utu wake na sifa zake.

Dini zingine kama Wakristo wanamuamini mungu, lakini pia wanasema kwamba Mungu ana mapungufu fulani. Wakristo wanasema kuwa Yesu (Nabii Isa [alayhis salaam]) ni Mungu na pia ni mwana wa Mungu. Vile vile Mayahudi wa Uarabuni waliamini kuwa Nabii Uzair (alayhis salaam) ni mwana wa Mungu.

Kwa hivyo, makundi haya wanamfananisha Mungu na kiumbe ambae uwepo wake umekuja kupitia sababu na mungu ana mapungufu fulani.

Kwa hiyo, katika Aya hii, Allah Ta’ala anawajibu kwa kusema kwamba Allah Ta’ala hana mtoto na wala Hakuzaliwa na wazazi na hafanani na viumbe ambao wana mipaka.

Mbali na hayo hapo juu, kundi lingine kama Wapagani waliamini kwamba Allah Ta’ala ni Mungu, lakini ana washariki wa kumsaidia katika kusimamia mambo ya ulimwengu.

Allah Ta’ala anawajibu kwa kusema kwamba Yeye awahitaji viumbe vyote, lakini viumbe vyote vinamuhitaji yeye kabisa.

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ ‎﴿٤﴾‏

Na wala hana anaye fanana naye.

Aayah hii inaeleza kwa msisitizo kwamba Allah Ta‘ala yuko nje ya ufahamu wa mwanadamu. Kwa hiyo, mwanadamu anapaswa kumwamini Allah Ta‘ala bila ya kujaribu kufikiria jinsi Allah Ta’ala anavyoonekana na bila kumlinganisha Allah Ta‘ala na chochote katika viumbe vilivyoumbwa. Wakati mwanadamu hawezi kumuona Allah Ta‘ala katika dunia hii, basi haiwezekani kwake kujua jinsi Allah Ta’ala anavyoonekana.

Hivyo basi, huko Akhera, Allah Ta’ala atawabariki waumini na sifa njema ya kumuona Yeye. Hadith inaeleza kwamba baada ya Waumini kuingia Jannah, Allah Ta’ala atawauliza kama wamefurahishwa na fadhila alizowaruzuku. Watamwambia Allah Ta’ala kwamba wameridhika na kufurahi sana.

Kisha Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) atawauliza: Je! nikupeni fadhila kubwa kuliko neema zote za Jannah? Waumini watajibu: “Ewe Mwenyezi Mungu! Ni fadhila gani iliyo kubwa zaidi kuliko fadhila ulizotufadhilisha nazo?” Kisha Allah Ta’ala atasema: “Nitawabariki na uwezo wa kuniona.” Waumini watakapomuona Allah Ta’ala, watatambua kwamba bila shaka hiyo ni fadhila kubwa na kwamba hakuna fadhila inayoweza kuwa sawa nayo.

Allah Ta’ala anahitimisha surah hii kwa kusema, “Na hakuna anayelingana Naye”. Kutokana na Aayah hii, tunaelewa kwamba Allah Ta’ala ni wa kipekee katika Utu Wake na Sifa Zake zote, kwa namna ambayo hakuna kitu kinachofanana na Allah Ta’ala katika Utu Wake na Sifa Zake, na kwamba hakuna chochote kinachoweza kulinganishwa naye kwa njia yoyote.

Kimsingi, surah hii inakanusha aina zote za shirki (ushirikina) na inaweka kanuni za kimsingi za Tawhid.

About admin

Check Also

Tafseer Ya Surah Nasr

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ إِذَا جَاءَ نَصْرُ اللَّهِ والْفَتْحُ ‎﴿١﴾‏ وَرَأَيْتَ النَّاسَ يَدْخُلُونَ فِي دِينِ اللَّهِ …