Tafseer Ya Surah Lahab

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

تَبَّتْ يَدَا أَبِي لَهَبٍ وَتَبَّ ‎﴿١﴾‏ مَا أَغْنَىٰ عَنْهُ مَالُهُ وَمَا كَسَبَ ‎﴿٢﴾‏ سَيَصْلَىٰ نَارًا ذَاتَ لَهَبٍ ‎﴿٣﴾‏ وَامْرَأَتُهُ حَمَّالَةَ الْحَطَبِ ‎﴿٤﴾‏ فِي جِيدِهَا حَبْلٌ مِّن مَّسَدٍ ‎﴿٥﴾‏

Iangamie mikono yake miwili ya Abu Lahab, na aangamie! Mali yake hayakumnufaisha wala aliyo yachuma. Hivi karibuni ataingia kwenye moto uliojaa miali ya moto, pamoja na mke wake, mchukuzi mbaya wa kuni. Shingoni mwake kuna (kola ya chuma kama) kamba ya nyuzi iliyosokotwa ya majani ya mitende.

Ilipoteremshwa Aya – وأنذر عشيرتك الأقربين  – (na uwaonye ndugu zako wa karibu – adhabu ya Akhera ikiwa hawakuamini) kwa Mtume (Sallallahu’alaihi wasallam), Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) akapanda mlima wa Swafaa na akaita kwa makabila mbalimbali za maquraish, “Enyi Bani Abd Manaaf! Enyi Bani Abdul Muttalib!” na kadhalika.

Makabila mbalimbali ya Maquraishi yaliposikia mwito wake, wote walikusanyika kumzunguka ili kumsikiliza atakachosema.

Kisha akawaambia, “Ikiwa nitawaambia kwamba kuna jeshi limepiga kambi chini ya mlima huu na wanapanga kuwashambulia ninyi asubuhi, je, mtaniamini?”

Wote walijibu kwa sauti moja, “Hakika tutakuamini kwani hatujawahi kukuta kuwa wewe ni mwongo au sio mwaminifu.”

Kisha Nabi (sallallahu ‘alaihi wasallam) akawaonya: “Ikiwa mtashindwa kuukubali ujumbe wangu, basi mimi ninawatahadharisheni na moto mkali unaowangojeeni huko Akhera.

Abu Lahab (mmoja kati ya wajomba wa Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam)) aliposikia ujumbe huu kutoka kwa Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam), alikasirika, na kwa hasira, alimwambia Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) akisema, تبا لك ألهذا جمعتنا” – Na uangamie! Je! hili ndilo kusudi pekee ambalo umetukusanya hapa?”

Ilikuwa katika tukio hili kwamba surah hii iliteremshwa.

Katika surah hii, Allah Ta’ala anaijibu laana ya Abu Lahab aliyeitoa kwa Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) kwa maneno yale yale ambayo Abu Lahab aliyatumia kumlaani Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam).

Allah Ta’ala Anasema,

تَبَّتْ يَدَا أَبِي لَهَبٍ وَتَبَّ ‎﴿١﴾

Na iangamie mikono miwili ya Abu Lahab, na aangamie!

Katika aya hii, neno “yad” lilitajwa. Neno “yad” kihalisi linamaanisha “mkono”.

Sababu ya mkono kutajwa ni kwamba mkono una nafasi muhimu sana katika ukamilifu wa kazi na matendo ya mwanadamu.

Kwa hiyo, katika aya hii, Allah Ta‘ala anahusisha laana ma mikono ya Abu Lahab.

Kuna wakati katika lugha ya Kiarabu, neno mkono unatajwa, lakini mtu mwenyewe anakusudiwa.

Katika aya hii, mikono ya Abu Lahab imetajwa, lakini nafsi yake yote imekusudiwa, kwani mwili wake wote utapata adhabu na utaungua katika moto wa Jahannum.

Katika baadhi ya riwaya, imepokewa kwamba surah hii iliteremshwa wakati Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) na Maswahaabah (radhiya allaahu ‘anhum) walipokuwa wakisusiwa katika bonde la Abu Taalib. Ilikuwa ni wakati huo ambapo Abu Lahab alikutana na watu fulani na kuwaambia, “Muhammad (sallallahu ‘alaihi wasallam) anatuonya juu ya mambo mengi yatakayotokea baada ya kifo (kama adhabu kaburini n.k.) lakini sioni lolote kati ya haya likitokea kwa waliokufa miongoni mwetu (ambao hawajaikubali dini yake). Mikono yangu itapata adhabu gani?” Kisha akapulizia kwenye mikono yake na kusema: “Uangamie, lakini hakika, sioni anachokisema Muhammad (sallallahu ‘alaihi wasallam) kuwa ni kweli.” Baada ya hapo, surah hii iliteremshwa.

Abu Lahab aliendelea kumtukana Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam), kumdhalilisha na kumzuwia kuwafikishia Dini kwa watu, lakini Allah Ta’ala aliilinda heshima na uadilifu wa Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) na akamlaani Abu Lahab katika Qur’an Takatifu.

Kwa hivyo, tunaona kwamba hata baada ya kuteremshwa kwa surah hii, hakuacha uovu wake na aliendelea kusababisha madhara kwa Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) na Waislamu, akijaribu awezavyo kukatisha kazi ya Uislamu.

Tunaona kwamba ingawa alikuwa amempinga Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) katika kipindi chote cha utume wake, taabu yake iliendelea tu kuzidi, mpaka wiki moja baada ya Vita vya Badr, alipata aina ya ugonjwa wa virusi ambao ulisababisha kuleta vidonda mwilini mwake kote.

Familia yake na watoto wote walimwacha na kumtenga hadi kulikua hakuna aliyetaka hata kumkaribia. Kwa hivyo, alikufa kwa kutengwa katika hali ya taabu na unyonge.

Baada ya kufa mwili wake uliachwa kuoza kwa sababu hakuna aliyetamani hata kuugusa mwili huo kutokana na hofu ya wao kupata ugonjwa huo.

Hatimaye, watu wa mji huo walisisitiza kwamba mwili huo unapaswa kutupwa mahali fulani. Hivyo, baadhi ya watumwa waliajiriwa kuchimba shimo na kutupa mwili ndani yake. Hata wale watumwa hawakuthubutu kuugusa mwili huo kwa mikono mitupu, hivyo walitumia magogo kuusukuma mwili wake ndani ya shimo kisha wakaufunika na mawe.

Hii ilikuwa ni taabu na fedheha aliyoipata katika dunia hii, na unyonge na laana aliyokumbana nayo baada ya kifo.

Zaidi ya hayo, adhabu inayomngoja huko Akhera itakuwa mbaya zaidi, kama ilivyoelezwa katika Sura hii.

مَا أَغْنَىٰ عَنْهُ مَالُهُ وَمَا كَسَبَ ‎﴿٢﴾

Mali yake hayakumnufaisha wala aliyo yachuma.

Abu Lahab daima alikuwa akijigamba juu ya mali yake iliokuwa nyingi na kuhusu watoto wake ambao walisimama pamoja naye wakimuunga mkono. Alikuwa akisema, Ikiwa anachosema Muhammad (Sallallahu ‘alaihi wasallam) ni kweli kuhusiana na mimi kuadhibiwa katika maisha ijayo, basi hakuna haja ya mimi kuwa na wasiwasi kwani mali yangu na watoto wangu watakuja kunisaidia katika maisha ijayo.”

Allah Ta’ala anajibu kauli hii kwamba watoto wake na mali zake hazitamfaa kitu Akhera na wala hataweza kutumia vitu hivi kujiokoa na adhabu ya milele ya Akhera.

Hata kabla ya kuondoka hapa duniani, Allah Ta’ala alimuonyesha kidogo ya yale atakayokumbana nayo Akhera, kwa sababu mali yake yote na watoto wake hawakuwepo kwa ajili yake wakati alipokuwa akiwahitaji zaidi.

Hakukuwa na mtu yoyote pembeni yake wakati alipokuwa amelala kwenye kitanda chake cha kifo kwa ugonjwa. Wote walikuwa wamemtenga na kumwacha afe peke yake.

سَيَصْلَىٰ نَارًا ذَاتَ لَهَبٍ ‎﴿٣﴾‏ وَامْرَأَتُهُ حَمَّالَةَ الْحَطَبِ ‎﴿٤﴾‏

Hivi karibuni ataingia kwenye moto uliojaa miali ya moto, pamoja na mke wake, mchukuzi mbaya wa kuni.

Mke wa Abu Lahab, Ummu Jamiil, kama mumewe, alikuwa adui mkubwa wa Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam). Alimuunga mkono mume wake kwa jitihada kwenda kinyume na Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) na Uislamu.

Kwa hiyo, katika Aya hii, Allah Ta’ala vile vile anamtahadharisha kuhusu adhabu kali ya Akhera inayomngoja.

Allah Ta’ala anamtaja kama ‘mchukuzi mbaya wa kuni’.

Kwa mujibu wa baadhi ya riwaaya, alikuwa akikusanya matawi ya miiba kutoka msituni na kuyaweka kwenye njia ya Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) ili kumdhuru. Hii ni moja ya maelezo ya msemo ‘mbeba kuni’.

Kwa mujibu wa mufassireen wengine, ‘mchukuzi wa kuni’ ni usemi unaotumiwa na Waarabu kwa mtu anayevunja uhusiano na kuwasha moto wa uadui baina ya watu kwa kusengenya.

Sababu ya Ummu Jameel kupokea jina hili ni kwamba alikuwa akitangaza vitu vya uwongo visio na msingi kuhusu Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) ili kuwasha moto wa chuki dhidi yake.

فِي جِيدِهَا حَبْلٌ مِّن مَّسَدٍ ‎﴿٥﴾‏

Shingoni mwake kuna (kola ya chuma kama) kamba ya nyuzi iliyosokotwa ya majani ya mitende.

Huu ndio msimamo ambao atafufuliwa siku ya Qiyaamah, kwamba shingoni mwake kutakuwa na kola ya chuma kama kamba ya nyuzi iliyosokotwa ya majani ya mitende.

About admin

Check Also

Tafseer Ya Surah Nasr

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ إِذَا جَاءَ نَصْرُ اللَّهِ والْفَتْحُ ‎﴿١﴾‏ وَرَأَيْتَ النَّاسَ يَدْخُلُونَ فِي دِينِ اللَّهِ …