Tafseer Ya Surah Falaq Na Surah Naas

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ ‎﴿١﴾‏ مِن شَرِّ مَا خَلَقَ ‎﴿٢﴾‏ وَمِن شَرِّ غَاسِقٍ إِذَا وَقَبَ ‎﴿٣﴾‏ وَمِن شَرِّ النَّفَّاثَاتِ فِي الْعُقَدِ ‎﴿٤﴾‏ وَمِن شَرِّ حَاسِدٍ إِذَا حَسَدَ ‎﴿٥﴾‏

Sema (Ewe Muhammad (sallallahu ‘alaihi wasallam): Najikinga kwa Mola Mlezi wa mapambazuko, na shari ya kila alichokiumba, na shari ya giza (la usiku) linapoingia, na shari ya wale wanaopuliza kwenye mafundo (wakati wa kufanya uchawi), na shari ya mwenye wivu anapohusudu.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ ‎﴿١﴾‏ مَلِكِ النَّاسِ ‎﴿٢﴾‏ إِلَٰهِ النَّاسِ ‎﴿٣﴾‏ مِن شَرِّ الْوَسْوَاسِ الْخَنَّاسِ ‎﴿٤﴾‏ الَّذِي يُوَسْوِسُ فِي صُدُورِ النَّاسِ ‎﴿٥﴾‏ مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ ‎﴿٦﴾‏

Sema (Ewe Muhammad (sallallahu ‘alaihi wasallam) Najikinga kwa Mola Mlezi wa wanaadamu, Mfalme wa wanaadamu, Mungu wa wanaadamu na shari ya mwenye kuweka wasiwasi anayerudi nyuma (pindi jina la Allah Ta’ala linapotajwa), mwenye kutia wasiwasi katika nyoyo za watu, kutoka kwa majini au wanaadamu.

Sura hizi mbili, Surah Falaq na Surah Naas, ziliteremshwa Madinah Munawwarah baada ya hijrah ya Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam). Kwa hiyo, surah hizi mbili zinaitwa ‘Surah za Madina’.

Sababu ya kuteremshwa kwa surah hizi mbili ni kwamba Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) alipatwa na sihr (uchawi).

Uchawi Ukifanyiwa Kwa Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam)

Katika mwaka wa 6 baada ya hijra, Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) na Maswahabah (radhiallahu ‘anhum) walisafiri kwenda Makka Mukarramah kwa nia ya kufanya Umra. Hata hivyo, walikataliwa kuingia Makka Mukarramah na makafiri wa Makka. Baada ya hapo, mkataba wa amani ulisainiwa na Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) na makafiri wakieleza kwamba kwa muda wa miaka kumi, hakutakuwa na vita wala mapigano baina ya majeshi hayo mawili. Mkataba huu uliitwa Sulh Hudaybiyyah (Mkataba wa Hudaybiyyah).

Baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) na Maswahabah (Radhiya Allaahu ‘anhum) walirejea Madinah Munawwarah katika mwezi wa Dhul Hijjah.

Mwezi mmoja baadaye, katika mwezi wa Muharram 7 AH, kundi la Wayahudi lilikuja kwa Labeed bin Aa’sam ambaye alikuwa mtaalamu wa uchawi. Mayahudi hawa walimwambia kwamba walikuwa wamejaribu bila kuchoka, mara nyingi, kumroga Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) na kumuua, lakini uchawi wao wote haukufaulu. Kwa hiyo, waliamua kumsogelea, wakijua kwamba yeye ni mtaalamu wa fani hii na kwamba hakuna mtu aliyemtaalamu kama yeye katika fani ya uchawi. Walimlipa dinari tatu (sarafu za dhahabu) ili kukamilisha kazi ya kumuua Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam).

Kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, Labeed alikuwa Myahudi, na riwaya zingine zinaonyesha kuwa alikuwa munaafiq (mnafiki), wakati riwaya zingine zinaonyesha kuwa alikuwa miongoni wa MaAnsaar wa Madinah Munawwarah.

Hafidh Ibnul Hajar (rahimahullah) anasuluhisha baina ya riwaya hizi kwa kueleza kwamba kabla ya hijra ya Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam), MaAnswaar walikuwa na mafungamano ya karibu na Mayahudi. Lakini, baada ya Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) kuhijiria Madinah Munawwarah, maAnswaar walisilimu na kukata mahusiano na Mayahudi. Miongoni mwao alikuwa Labeed bin Aa’sam. Kwa sababu ya uhusiano wake wa ukaribu na Wayahudi, watu wengine walimwona kuwa Myahudi.

Labeed alitoka kwenye kabila la Banu Zuraiq. Alijifanya kama muumini na kuhudhuria mikusanyiko ya Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam), huku Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) akijua kuwa yeye ni miongoni mwa munaafiqeen (wanafiki).

Baada ya Labeed kukubali malipo ya dinari tatu kutoka kwa Mayahudi, alikutana na kijana wa Kiyahudi ambaye alikuwa akitembelea nyumba ya Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) na alikuwa katika huduma wake. Alimuomba kijana huyo ampatie nywele zilizobarikiwa za Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam). Ili kumfanya mvulana amletee nywele, alitumia kisingizio cha uwongo ambacho alimweleza akimshawishi kwamba alitaka nywele kwa kusudi fulani nzuri. Kwa hiyo, kijana huyo alizipata nywele zilizobarikiwa na chanuo ya Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) na akamkabidhi.

Labeed alitumia nywele zilizobarikiwa za Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam), meno ya chanuo na mti wa tende katika uchawi aliyomtupia Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam). Riwaya nyingine pia zinaeleza kwamba alikuwa ametengeneza picha ya Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) kutumia nta na akachomeka sindano kumi na moja ndani yake.

Familia nzima ya Labeed bin Aa’sam ilihusika katika uchawi, hivyo akawatumia mabinti zake kumsaidia katika mchakato wa kumroga Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam). Baada ya kumaliza sihr, Labeed alichukua vitu hivi na kuviweka chini ya jabali ambalo lipo chini ya kisima fulani huko Madinah Munawwarah kilichoitwa Bir Zi Arwaan.

Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) anaeleza kwamba baada ya kutupiwa uchawi huo kwa Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam), aliugua na kuanza kusahau mambo mengi yanayohusiana na dunia. Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alikuwa akisahau zamu ya nani ilikuwa kutoka kwa wake zake waheshimiwa na kwenda kwenye nyumba ya mke mwingine. Pia alikuwa akipoteza hamu ya kula na kudhoofika. Hata hivyo, kwa kadiri mambo ya deeni yalivyokuwa, kama vile kufikishia ummah dini, kukumbuka wahi aliyoteremshiwa, basi uchawi huo haukumathiri kwa vyovyote vile. Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alikaa katika hali hii ya ugonjwa kwa takriban miezi sita.

Wakati Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alipokuwa akipatwa na tatizo hili, mwanzoni alihisi kwamba linahusiana na ugonjwa fulani. Kwa hiyo, Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alifanya hijama ili kujiponya, lakini alipoona kwamba hakuna unafuu wa hali yake, alitambua kwamba kulikuwa na jambo jingine ambalo lilikuwa linamuathiri.

Mazungumzo Kati Ya Malaika Wawili

Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) siku moja alizungumza na Aaisha (Radhiya Allaahu ‘anha) wakati wa ugonjwa wake na akamwambia, “Nimekuwa mgonjwa kwa muda mrefu, na niliendelea kumuomba Allah Ta’ala anifunulie ukweli wa hali yangu.

Pindi nilikuwa nimepumzika chini katika hali baina ya usingizini na kuwa macho, Allah Ta’ala alinitumia Malaika wawili ( Jibra’eel (‘alaihis salaam) na Mikaa’eel (‘alaihis salaam) mmoja alikaa pembeni mwa kichwa changu na mwingine kando ya miguu yangu.

Malaika aliyekuwa kichwani akamwuliza yule malaika aliye kuwa miguuni, “Kuna nini kuhusu mtu huyu?” Anaumwa ugonjwa gani?”

Malaika Mwingine akajibu, “Amepatwa na uchawi.”

Malaika ambaye yupo kichwani kisha akamwuliza malaika aliye kuwa miguuni, “Ni nani anayehusika na hili?” Malaika mwingine akajibu, “Labeed bin Aa’sam.”

Malaika aliyekuwa kichwani alimwuliza zaidi malaika huyo wa miguuni, “Ni vitu gani vilivyotumika kumroga?”

Malaika akajibu, “Uchawi ulifanyika kwenye nywele zake, meno za kitana chake na mti wa tende.”

Baada ya kusikia mazungumzo haya yaliyotokea baina ya hawa Malaika wawili (ambao kwa hakika ilikuwa ni mjumbe wa kumjulisha Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) kuhusu hali yake kutoka kwa upande wa Allah Ta’ala), Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) aliamka na akaamuru kundi la watu wanne kati ya Maswahaabah( Ali, Ammaar, Jubair ibn Iyaas na Qais bin Mihsan (radhiyallahu ‘anhum)) waende kwenye sehemu ambapo sihr (uchawi) iliwekwa na kuiondoa.

Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) pia alifahamishwa na Allah Ta’ala katika ndoto kwamba uchawi huo umewekwa kwenye kisima fulani. Imepokewa kwamba Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) pia alikwenda kisimani na uchawi vilivyofanyiwa vilitolewa kutoka chini ya jiwe chini ya kisima na kuletwa mbele ya Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam).

Ilikuwa ni katika wakati huu ambapo Jibra’eel (Alaihi Salaam) alishuka kutoka mbinguni na kuleta pamoja naye surah hizi mbili; Surah Falaq na Surah Naas, ambazo ziliteremshwa kwa Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) wakati huo. Jibraeel (alaihis salaam) alimuamuru Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) asome kila aya ya Surah hizi mbili kuanzia mwanzo hadi mwisho. Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alipokuwa akisoma kila aya, fundo kutoka kwenye utumbo lilifunguka na sindano kutoka kwenye sura wa nta wa Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) zilitolewa. Pindi sindano zilipokuwa zikitolewa, Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alihisi maumivu kidogo, lakini baadaye alipata nafuu kubwa.

Baadhi ya Ahaadith zinaeleza kwamba baada ya sihr (uchawi) kuondolewa, Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) alipata unafuu mkubwa sana kiasi kwamba ilikuwa kama alitolewa pingu baada ya kufungwa kwa muda mrefu.

Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alieleza hali ya miti na maji ya kisima kwa Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) akisema: “Ilikuwa ni kama maji yametiwa hina na kuyafanya kuwa meusi meusi, na yale miti yanayoota kutoka kwenye maji yalifanana na vichwa vya mashetani (riwaaya zingine zinaonyesha kwamba matawi ya miti yalifanana na vichwa vya nyoka). Hii ndipo ilikuwa sehemu ya kutisha ambapo uchawi ulifanyika kwa Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam).

Baada ya Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) kusoma mu’awwadhatain (Surah Falaq na Surah Naas), Jibra’eel (‘alayhis salaam) akasoma dua ifuatayo, ili kumtibu Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) kwa uchawi huo alioupata:

بِاسْمِ اللهِ أَرْقِيْكَ مِنْ كُلِّ شَيْءٍ يُؤْذِيْكَ مِنْ شَرِّ كُلِّ نَفْسٍ أَوْ عَيْنٍ حَاسِدٍ اللهُ يَشْفِيْكَ بِاسْمِ اللهِ أَرْقِيْكَ

Kwa jina la Allah Ta’ala ninakusomea maneno haya (na kukutibu kwa kutafuta tiba kutoka kwa Allah Ta’ala) kutokana na kila jambo linalokudhuru – kutokana na ubaya wa kila nafsi au jicho lenye husuda. Mwenyezi Mungu akupe tiba. Kwa jina la Allah Ta’ala ninasoma maneno haya juu yako (na kukutibu kwa kutafuta tiba kutoka kwa Allah Ta’ala).

Tabia Bora Ya Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam)

Baada ya ule uchawi kuondolewa na Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) akapata utulivu mkubwa, Aaishah (radhiya allaahu ‘anha) alipendekeza kwake awaite watu na aweke wazi mtu aliyemfanyia uchawi huo na aunguze uchawi huo na moto mbele ya watu. Baadhi ya riwaya zinataja kwamba alipendekeza kwa Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) kumfukuza mtu huyo (Labeed bin Aa’sam) kutoka Madinah Munawwarah.

Hata hivyo, jibu la haraka la Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) lilikuwa, “Ewe Aaishah! Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) ameniponya, kwa hivyo hakuna haja ya mimi kufanya hivyo. Adhabu atakayompa Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) inatosha kwake.” Kwa hio, Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) aliamrisha kwamba kisima hicho lizikwe na kufungwa kabisa.

Ilikuwa ni tabia iliyobarikiwa ya Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) na onyesho la tabia yake ya hali ya juu kwamba hakuwahi kulipiza kisasi kwa kitendo chochote kilichofanywa dhidi ya nafsi yake binafsi. Badala yake, sikuzote aliwasamehe wale waliomtendea vibaya au hata kumdhulumu. Labid bin Aa’sam alikuwa akihudhuria majaalis (mikusanyiko) ya Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam), kama alivyokuwa miongoni ya wanafiki, lakini imenukuliwa kwamba hata baada ya kutokea tukio hili, Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) hakuwahi kumhutubia kuhusu hilo, wala kumtendea tofauti.

Lengo Na Madhumuni Ya Kuteremshwa Kwa Sura Hizi Mbili

Sura hizi mbili, kama ilivyoelezwa hapo mwanzoni, ziliteremshwa wakati ambapo uchawi ulitumwa kwa Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam). (Surah hizi mbili) Ziliteremshwa na Allah Ta‘ala hasa kwa ajili ya tiba na ulinzi wa Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam), na kwa ajili ya ulinzi wa Umma wa Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) kwa ujumla.

Maulamaa wanaeleza kwamba Sura ya kwanza (Surah Falaq) iliteremshwa ili kumwokoa mtu kutokana na madhara na hatari yote ya kimwili hasa, na Sura ya pili (Surah Naas) iliteremshwa hasa ili kumuokoa mtu kutokana na madhara na hatari zote za kiroho.

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ ‎﴿١﴾‏

Sema (Ewe Muhammad (Sallallahu ‘alaihi wasallam): Najikinga kwa Mola Mlezi wa mapambazuko

Katika aya hii, Allah Ta’ala ametaja makhsusi neno ‘mapambazuko’, kumaanisha wakati wa alfajiri ambapo nuru inaonekana baada ya giza.

Katika hili kuna ujumbe kwa Mtume (sallallahu alaihi wasallam) na Ummah, kuwafahamisha kwamba kama jinsi giza la usiku linavyofuatwa na mwangaza wa alfajiri, hivyo baada ya kipindi cha dhiki na shida, nusra ya Allah Taala bila ya shaka itafuata.

Mara tu msaada wa Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) ukifika, huondoa tabaka zote za giza na kusababisha mwanga kuonekana kila mahali. Hivyo basi, mtu akipambana na matatizo na dhiki, anatakiwa kurejea kwa Allah Ta’ala na asipoteze matumaini ya rehma zake wakati wowote.

Baadhi ya Mufassireen wanaeleza kwamba neno “Falaq” linamaanisha bonde katika Jahannam. Ukali wa bonde hili ni kwamba Jahannam yenyewe inajikinga nayo kwa Allah Ta‘ala kila siku. Tunaweza kufikiria vizuri hali ya wale ambao watatupwa katika sehemu kama hiyo katika Jahannam.

Kwa hiyo, kupitia Allah Ta’ala kutaja bonde hili katika Jahannam na kutaja kuwa Yeye ndiye Mola Mlezi wa bonde hili, kuna dalili juu ya kipengele hiki kwamba wakati Allah Ta’ala ndiye Muumba wa chanzo cha huzuni, machungu na dhiki hizo ambazo mtu hawezi kufikiria tatizo lolote naugumu zaidi kuliko hayo; basi mwanadamu atambue kuwa hakuna sehemu kukimbilia na sehemu takatifu kwake isipokuwa kurejea kwa Allah Ta’ala. Yeye peke yake ana suluhisho la matatizo yote, majibu ya maswali yote na njia ya kuepuka matatizo yote.

مِن شَرِّ مَا خَلَقَ ‎﴿٢﴾

na shari ya kila alichokiumba

Aya hii inajumuisha kila aina ya ugumu au uovu unaoweza kufikiriwa, pamoja na yale ambao hayawezi kufikiriwa kibinadamu. Kimbilio linatafutwa kwa Allah Ta’ala kutokana na kila aina ya madhara au shari.

Katika aya hii, Allah Ta’ala anaelekeza mazingatio yetu kwake Yeye kuwa ni Muumba wa maovu. Kwa hivyo, wakati yeye ni Muumba wa maovu, basi tunapaswa kutafuta hifadhi kwake ili kuondoa maovu. Hivyo tunapoomba kuhifadhiwa tumuombe Mola wa mapambazuko kutokana na shari ya viumbe vyake.

Katika hili, Allah Ta’ala anatusisitiza kwamba wakati kila kitu ni kiumbe Chake, basi kwa vyovyote utakavyoonekana kuwa ndogo au wa uharibifu kiasi gani machoni mwetu, tukumbuke kwamba wote ni viumbe wake na yeye ana udhibiti kamili juu yao. .

Kwa hiyo, mtu hatakiwi kuzidiwa nguvu na tatizo na hali aliyonayo, bali anapaswa kumwangalia Muumba ambaye ameumba kila kitu na ana udhibiti wa kila kitu.

Kimsingi, muumini anapaswa kutambua kwamba Yule ambaye ana uwezo wa kuumba kitu pia ana uwezo wa kukiangamiza na kukisahaulisha kabisa. Wakati mwingine mtu hufikiria sana na tatizo alilo nalo hadi kwamba anasahau kwamba kuna Muumba ambaye ndiye mwenye mamlaka kamili juu ya kila kitu.

Baada ya kujikinga kwa Allah Ta‘ala kutokana na madhara yote kwa ujumla, Allah Ta’ala anatufundisha kujikinga Kwake kutokana na madhara matatu makhsusi katika Aya tatu zifuatazo:

 وَمِن شَرِّ غَاسِقٍ إِذَا وَقَبَ ‎﴿٣﴾‏ وَمِن شَرِّ النَّفَّاثَاتِ فِي الْعُقَدِ ‎﴿٤﴾‏ وَمِن شَرِّ حَاسِدٍ إِذَا حَسَدَ ‎﴿٥﴾‏

na shari ya giza (la usiku) linapoingia, na shari ya wale wanaopuliza kwenye mafundo (wakati wa kufanya uchawi), na shari ya mwenye wivu anapohusudu.

Maulamaa wanaeleza kwamba mmoja kati ya sababu ya shari hizi tatu kutajwa na kuangaziwa hasa ni kwamba shari hizi tatu yalipatikana katika tukio ambalo lilikuwa ni sababu ya kuteremshwa kwa surah hizi mbili (yaani. uchawi uliofanyiwa kwa Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam).

  • Shari la usiku wa giza limetajwa kwa sababu uchawi ulifanyika usiku.
  • Shari ya wale wanaopuliza kwenye mafundo ulitajwa kwa sababu waliohusika katika uchawi huo walikuwa mabinti wa Labeed bin Aa’sam, ambao walipuliza ndani ya mafundo wakati walipokuwa wamefanya uchawi.
  • Shari la husda ulitajwa kuwa chanzo cha Mayahudi kufanya uchawi huo ni husda waliyokuwa nayo nyoyoni mwao kwa Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) na wao kutokutaka kusambazwa lengo lake na ujumbe wake (wa Uislamu).

Kwa hivyo, kingo hutafutwa makhsusi kutokana na aina hizi tatu za madhara:

1. Usiku ambao giza lake linatanda.

2. Shari la wale wanawake ambao walipuliza kwenye mafundo.

3. Shari la mwenye wivu anapohusudu.

Kutokana na madhara hizi tatu, tunaona kwamba madhara ya kwanza na ya tatu yameonganishwa na kitu. Kwenye madhara ya kwanza, shari la usiku umetajwa na sharti la giza lake kutandaza, na kwenye madhara ya tatu, shari la chuki umetajwa na sharti ya kuonyesha husuda yake.

Kuhusu madhara ya pili, basi tunaona kwamba haijaonganishwa na sharti lolote. Sababu ni kwamba shari la usiku unapatwa kwenye giza lake. Giza linapoondoka kwa kupambazuka kwa mapambazuko, basi shari la usiku huisha. Mashambulizi ya wezi na wachawi, na madhara yanayosababishwa na viumbe na wanyama mbalimbali, kawaida hupatikana usiku. Kwa hivyo, inapoombwa kinga kwa Allah Ta’ala kutokana na shari ya usiku, madhara yote haya yanajumuishwa humo.

Vile vile shari la chuki huonekana pale tu anapoonyesha husuda yake, la sivyo husuda yake itamfanya tu kuathirika kutoka ndani na haitamuathiri yule anayemwonea wivu. Hivyo basi, ulinzi na usalama hutafutwa kwa mwenye wivu wakati anapotaka kujieleza na kudhihirisha wivu wake, kwa sababu huu ndio wakati anasababisha madhara kwa wengine.

Kuhusu uchawi, huathiri mtu mchana na usiku. Kwa hivyo, hakuna kifungu au sharti lililoonganishwa na shari hio.

Akitoa maoni yake juu ya aya hizi, Hafidh Ibn Qayyim (rahmatullahi alaih) alitaja kwamba sababu ya madhara yote, iwe ya kimwili au ya kiroho, yanaweza kuingizwa katika sababu mbili:

1) Maumivu halisi ya kimwili, balaa au bahati mbaya ambayo mtu hupata.

2) Sababu inayoleta maumivu. Katika kesi ya maumivu ya kimwili, ni sababu ya kimwili, na katika kesi ya maumivu ya kiroho, ni sababu ya kiroho. Kwa mfano, kufr, shirki, kumuasi Allah Ta‘ala n.k. ni sababu za kurudi nyuma kiroho na madhara.

Sura hii, kupitia aya مِنۡ شَرِّ مَا خَلَقَ , inajumuisha aina zote mbili za sababu na inatufundisha kutafuta ulinzi kutokana na sababu zote mbili za shari na madhara.

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ ‎﴿١﴾‏ مَلِكِ النَّاسِ ‎﴿٢﴾‏ إِلَٰهِ النَّاسِ ‎﴿٣﴾‏ مِن شَرِّ الْوَسْوَاسِ الْخَنَّاسِ ‎﴿٤﴾‏ الَّذِي يُوَسْوِسُ فِي صُدُورِ النَّاسِ ‎﴿٥﴾‏ مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ ‎﴿٦﴾

Sema (Ewe Muhammad (Sallallahu ‘alaihi wasallam) Najikinga kwa Mola Mlezi wa wanaadamu, Mfalme wa wanaadamu, Mungu wa wanaadamu na shari ya mwenye kuweka wasiwasi, anayerudi nyuma (pindi jina la Allah Ta’ala linapotajwa), mwenye kutia wasiwasi katika nyoyo za watu, kutoka kwa majini au wanaadamu.

Katika surah iliyotangulia (Surah Falaq), kimbilio lilitafutwa hasa na kimsingi kutokana na madhara ya kimwili (ingawa madhara ya kiroho yalijumuishwa pia kwa ujumla kwenye Aya مِنۡ شَرِّ مَا خَلَقَ – shari ya vitu vyote alivyoviumba Allah Ta’ala). Katika surah hii, kimbilio linatafutwa kutokana na madhara ya kiroho na maovu, yaani madhara ya Shetani.

Kwa vile madhara ya kiroho ni mabaya zaidi na makubwa zaidi kuliko madhara ya kimwili, Qur’an Takatifu inamalizika na surah hii. Katika kesi ya madhara ya kimwili ambayo yanaathiri mtu, madhara yanabaki hapa duniani. Pindi tu anapoaga dunia, hali ngumu aliyokuwa akiapitia yanaisha. Kuhusu madhara ya kiroho, yanaendelea na kuvuka maisha ya dunia hadi maisha ya Akhera. Kwa hiyo, tunaelewa kwamba madhara ya kiroho ni makubwa zaidi yakilinganishwa na madhara ya kimwili ya ulimwengu huu.

Katika surah hii, neno “An-Naas” limerudiwa mara tano. Kawaida katika khutba, ikiwa maelezo yanafanywa kwa kitu ambacho tayari kimetajwa wazi mwanzoni, basi mtu anaeleza kwa ishara tu. Lakini katika aya hii, neno (An-Naas) limerudiwa mara kwa mara.

Baadhi ya Maulamaa wanaeleza kwamba sababu ya An-Naas kurudiwa mara tano ni kuonyesha hatua tano tofauti ambazo mwanadamu hupitia wakati wa uhai wake.

Mwanzo kabisa, yeye ni mtoto na ni muhitaji zaidi kwa Allah Ta’ala. Kwa hivyo, Allah Ta’ala anatufundisha kwamba tunatafuta ulinzi na hifadhi Kwake. Allah Ta’ala Anasema,

قُلْ اَعُوۡذُ بِرَبِّ النَّاسِ Sema, najikinga kwa Mola wa watu (Allah Ta‘ala).

Neno (Rabb) Mola inamaanisha yule mwenye kusimamia mambo ya kila kiumbe, akiwasaidia wanapoendelea na kusonga mbele kutoka hatua hadi hatua, na kuona maslahi na mahitaji yao kila wakati. Hivyo basi, hapo mwanzoni, mtoto anapokuwa katika hatua zake za kukua, neno (Rabb) Mola lilifaa zaidi kutumika katika kueleza haja ya mwanadamu kwa Allah Ta’ala.

Binadamu anapoendelea, anafika hatua ya kuwa kijana. Ni katika hatua hii ambapo anakuwa na hofu kwa mtawala na mamlaka. Hivyo, kupitia neno مَلِکِ النَّاسِ, Allah Ta‘ala anaashiria kwamba tunapaswa kutafuta ulinzi kwa mfalme halisi na mamlaka kuu ya mwanadamu yaani Allah (Subhaanahu Wata’aala).

Hatua ya tatu ya maisha ya mwanadamu ni wakati anafikia uzee. Kwa ujumla, mtu anayekaribia mwisho wa maisha anatambua kwamba anahitaji kurejea zaidi kwa Allah Ta‘ala katika ibada na utiifu, na hivyo anajibidiisha zaidi katika haki na ibada ya Allah Ta‘ala. Kwa hiyo, kuhusu hatua hii, neno اِله النَّاسِ lilitumika. Kwa maneno mengine, mwanadamu anatakiwa kurejea zaidi kwa Allah Ta‘ala na kutafuta hifadhi Kwake, kwa sababu yeye ndiye اِله wa watu, Mola wa pekee.

Sifa hizi tatu na sifa za Allah Ta‘ala yaani Mola, Malik  na Ilaah, zote zinaonyesha uwezo wa kulinda.

Kuhusu neno Rabb, kwa Kiarabu linaponasibishwa na jambo fulani, basi linatoa maana ya umiliki. Kwamfano رب الدار– mwenye nyumba na رب العبد – mmiliki wa mtumwa. Kwa hiyo, neno “rabb” linaonyesha kulinda kwa vile mwenye kumiliki kitu Kawaida anahangaikia mali zake na anahangaikia kuzitunza na kuzilinda.

Neno malik (mfalme) linaashiria maana ya kulinda kwa sababu kwa ujumla mfalme anajali ustawi na ulinzi wa raia wake.

Na vile vile neno Ilaah (Mungu) linaonyesha kulinda kwa sababu Ilaah (Mungu) anajali kuhusu uumbaji Wake. Hivyo basi, Allah Ta’ala anapokuwa na sifa zote hizi tatu, basi inadai kwamba Allah Ta’ala atavilinda viumbe vyake, na hakutakuwa na ulinzi mkubwa zaidi kuliko ulinzi wa Allah Ta’ala.

Mara ya nne lilipotajwa neno An-Naas, linarejelea hali anayopitia mwanadamu katika maisha yake yote, ambapo Shaytwaan daima hujaribu kumpoteza kwa kuingiza mawazo maovu na minong’ono ndani ya moyo wake. Hivyo basi, mwanadamu anafundishwa kwamba anapaswa kuendelea kutafuta ulinzi na usalama wa Allah Ta‘ala dhidi ya Shetani.

Mara ya tano An-Naas inarudiwa, inarejea kwa mawakala na wasaidizi wa Shaytwaan wanaomsaidia Shaytwaan katika kazi yake ya kupotosha viumbe. Miongoni mwa mawakala wake ni shayateen wengine pamoja na watu waovu. Kama inavyoonekana kwa ujumla, kundi na marafiki mtu anaokuwa nao una ushawishi mkubwa juu ya mawazo yake na tabia, na ujumbe hupitishwa kutoka moyo hadi moyo, ambayo husababisha mtazamo na mawazo ya mtu kubadili maisha yake

Shaytwaan, Menye kutia Waswasa

Katika surah hii, Allah Ta‘ala anamtaja Shaytwaan kama الْوَسْوَاسِ Neno الْوَسْوَاسِ maana yake halisi ni ‘kutia waswasa’, (ambalo katika lugha ya Kiarabu, linamaanisha halisi wa neno ambalo vitenzi vyote hutoka). Kwa hiyo, Allah Ta’ala anamwita Shaytwaan kwa jina hili, kwa kutumia neno halisi, kuashiria uwezo mkubwa alionao katika kumpoteza mwanadamu kupitia waswasa zake.

Maulamaa wanaeleza kwamba katika moyo wa kiroho wa mwanadamu kuna sehemu mbili. Katika sehemu moja, kuna malaika ambaye humsukuma mwanadamu kuelekea na kufanya mema. Hii ni upande wa kulia wa moyo wa mwanadamu. Upande wa kushoto wa moyo wa mwanadamu, kuna sehemu nyingine ambayo ndani yake kuna Shaytwaan ambaye humhimiza na kumshawishi mwanadamu kwenye maovu.

About admin

Check Also

Tafseer Ya Surah Nasr

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ إِذَا جَاءَ نَصْرُ اللَّهِ والْفَتْحُ ‎﴿١﴾‏ وَرَأَيْتَ النَّاسَ يَدْخُلُونَ فِي دِينِ اللَّهِ …