وَالنَّازِعَاتِ غَرْقًا ﴿١﴾ وَالنَّاشِطَاتِ نَشْطًا ﴿٢﴾ وَالسَّابِحَاتِ سَبْحًا ﴿٣﴾ فَالسَّابِقَاتِ سَبْقًا ﴿٤﴾ فَالْمُدَبِّرَاتِ أَمْرًا ﴿٥﴾
Ninaapa kwa wale (malaika) ambao wanao toa (roho za makafiri) kwa nguvu, na kwa wale (malaika) wanao toa (roho za waumini) kwa upole, na kwa wale (malaika) ambao wanapaa (angani) kwa haraka, na kwa wale (malaika) ambao wanashindana mbio (kutimiza amri za Allah Ta’ala), na wale (malaika) ambao wanasimamia mambo (wameamriwa kutimiza na Mwenyezi Mungu subhaanahu wata’ala,)
Kama vile Surah iliopita – Surah Naba – iliteremshwa kuthibiti imani ya siku ya Qiyamaah, hivyo Surah hii pia iliteremshwa kujadili mambo kadhaa ya Qiyaamah.
Katika Surah hii, Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) anaanza na kuchukua viapo juu ya sifa fulani za malaika ili kudhibitisha kwamba siku ya Qiyaamah ni hakika. Kwa hivyo, katika aya ya sita, baada ya kuchukua kiapo juu ya sifa za malaika, Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) anasema juu ya siku ya Qiyaamah.
Sababu dhahiri ya Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) kuchukua viapo kwa malaika ambao huondoa roho za watu ni kumjulisha mwanadamu kwamba kila mtu qiyaamah yake itaanza baada ya kufariki. Kwa hivyo, inasemekana, “Yule anayefariki, Qiyaamah yake inaanza.”
Ingawa Qiyaamah halisi kwa viumbe wote itafanyika mwishoni mwa ulimwengu, hata hivyo kwa kuwa maisha ya aakhera ya kila mtu itaanza wakati wa kifo chake, kifo cha kila mtu kinahesabiwa kuwa Qiyaamah yake.
Kwa jumla, katika aya hizi, Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) anaangazia sifa tano za malaika. Sifa tano ni hizi zifuatavyo:
Sifa ya kwanza ya malaika
وَالنَّازِعَاتِ غَرْقًا ﴿١﴾
Ninaapa kwa wale (malaika) ambao hutoa (roho za makafiri) kwa nguvu
Katika aya hii, Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) anaongea juu ya malaika wa kifo ambao hutoa roho za makafiri kwa nguvu na kwa ukali, kwa nguvu kamili, bila kuwaonyesha huruma yoyote. Malaika ambao huondoa roho za makafiri ni malaika wa adhabu, na neno “kwa nguvu” katika aayah linamaanisha maumivu ya kiroho, sio maumivu ya mwili. Kwa hivyo, watu ambao wapo karibu na mtu anayekufa hawawezi kuona maumivu ya mtu anayekufa kwa sababu maumivu yanahisi na roho ya mtu anayekufa, na sio mwili wake.
Wakati mwingine, inaonekana ingawa roho ya kafiri inatoka kwenye mwili wake kwa urahisi, lakini kwa ukweli sio hivyo, kama ilivyo katika aya hii, Allah Ta’ala anatuarifu juu ya uchungu mkubwa na mateso ambayo roho ya kafiri hupitia wakati wa kifo.
Sifa Ya Pili Ya Wa Malaika
وَالنَّاشِطَاتِ نَشْطًا ﴿٢﴾
na kwa wale (malaika) wanao toa (roho za waumini) kwa upole
Katika aya hii, Allah Ta’ala anasema kuhusu wamalaika ambao hutoa roho za waumini vizuri na kwa upole. Malaika ambao huondoa roho za waumini ni malaika wa huruma. Wameamriwa na Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) kushughulika na waumini kwa njia ya fadhili na upole.
Neno “النَّاشِطَاتِ“ limetoka kwenye neno “نشطَ” ambalo linamaanisha “kufungua fundo”. Hii inaashiria “kuondoa fundo la kitu ambacho kina maji au hewa, ili maji au hewa iweze kutolewa kwa urahisi”. Hii ni mfano wa kutoa roho za waumini kwa upole, tofauti na roho za makafiri ambao hutolewa kwa ukali. Ni kama roho ya muamini ilikuwa imefungwa ndani ya mwili wake, na mwili ulihitaji kufunguliwa kwa roho kutolewa.
Katika kesi hii pia, neno نَشْطًا ambalo hutafsiri kama “vizuri” au “kwa upole” linamaanisha kwa ulaini au upole, na sio uzoefu wa mwili. Wakati mwingine, mwamini mcha Mungu huonekana akipitia ugumu wa aina fulani wakati wa kifo chake, lakini hii haimaanishi kuwa anapitia ugumu wa kiroho au adhabu, ingawa kimwili inaweza kuonekana kwa wale waliopo karibu naye.
Wakati roho ya makafiri inapotolewa, eneo lote la adhabu ya Barzakh (maisha baada ya kifo) linakuja mbele yake. Ni wakati wa hofu kubwa na ya kutisha, na mtu anayekufa amezidiwa na hali hiyo. Kwa hivyo roho ikiwa na hofu sana na adhabu, huanza kutoka kwenye mwili wote, kujaribu kujificha au kutoroka adhabu. Lakini Malaika wa Kifo huondoa roho yake kwa nguvu na kwa ukali kutoka mwili wake, kama vile chuma hutolewa kwa nguvu kwenye uzi la kurowa (kama ilivyoelezewa katika Hadith ya Baraa bin Aazib (Radhiyallahu ‘Anhu) iliyorekodiwa katika Musnad-Ahmad).
Kwa upande mwingine, wakati roho ya mwamini inapotolewa, thawabu kubwa na baraka za Akhera ambazo ziko karibu kwake zinawasilishwa mbele yake na anapewa habari njema, kwa hivyo, roho yake inaacha mwili wake kwa urahisi na furaha.