Wakati wa Vita wa Uhud, miongoni ya misiba machingu aliyoipata Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) ilikuwa ni mjomba wake kipenzi hamza (Radhiyallahu anhu) kuuwawa kishahidi.
Aliyehusika kumuua Hamza (Radhiyallahu anhu) hakuwa mwingine ila Wahshi ibn Harb (Radhiyallahu anhu).
Wakati huo, hakuwa Mwislamu, lakini Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala)baadaye akambariki na Imaan na heshima ya kuwa Swahaaba. Tukio la kusilimu kwake ni kama ifuatavyo:
Baada ya Mwenyezi Mungu kumbariki Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) na maswahaabah kuiteka Makka Mukarramah, Wahshi (Radhiyallahu anhu) alikimbilia kwenda Taa’if, kwa sababu aliogopa kwamba Waislamu wangemkamata na kumuua kwa kulipiza kisasi kwa ajili ya yeye kumuua Hamzah (Radhiyallahu anhu).
Baada ya hapo, watu wa Taa’if walipotaka kusilimu, wakatuma wajumbe kwa Mtume (Sallallahu alaihi wasallam).
Wakati huo, Wahshi (Radhiyallahu anhu) pia alifuatana na kundi hili na akaja Makkah Mukarramah.
Alipofika mbele ya Mtume, Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akamuuliza: “Je, wewe ni Wahshi?” Wahshi akajibu,
“Ndiyo, mimi ni Wahshi.”
Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akasema, “Je, wewe ndiye mtu uliyemuua Hamzah (Radhiyallahu anhu)?
Wahshi (Radhiyallahu anhu) akajibu, “Ndio, suala (kuhusu mimi kumuua mjomba wako) ni kama vile ulivyosikia (yaani, mimi ndiye mtu niliyemuua mjomba wako).”
Licha ya Wahshi (Radhiyallahu anhu) kumuua mjomba wake Hamzah, Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) bado alikuwa na wasiwasi mkubwa juu ya maisha yake kuokolewa. Wasiwasi huu mkubwa ulitokana na mapenzi mazito aliyokuwa nayo Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) kwa kila ummati wake.
Hivyo basi, Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) mara moja alimpa wahshi da’wa kusilimu.
Wahshi (Radhiyallahu anhu) alitaka kusilimu, lakini alikuwa na wasiwasi kidogo moyoni mwake ambao ulikuwa ukimzuia kusilimu.
Kwa hiyo, akajibu: “Ewe Muhammad (Sallallahu alaihi wasallam)! muuwaji, mwenye kushiriki katika shirki au mwenye kuzini hatosamehewa na atapelekwa Jahannum? Allah Ta’ala Anasema:
وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّهِ إِلَٰهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ ۚ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ يَلْقَ أَثَامًا ﴿٦٨﴾ يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا ﴿٦٩﴾
Na wale ambao hawamuombi mungu mwengine pamoja na Allah Ta’ala, wala hawamuuwi mtu ambaye Mwenyezi Mungu ameharamisha isipokuwa kwa haki, wala hawazini; na mwenye kufanya haya (yaani kufanya dhambi hizi za shirki, kuua na zinaa), atakutana na adhabu (katika Jahannum). Atazidishiwa adhabu (katika Jahannamu) Siku ya Qiyaamah na atabaki humo akiwa amefedheheka.
Wahshi (Radhiyallahu anhu) akasema: “kuhusu mimi, basi nimeyatenda madhambi yote haya makubwa, basi je, kuna nafasi yoyote kwangu ya kupata msamaha?”
Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) alinyamaza na hakujibu, mpaka Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) akateremsha aya ifuatayo ya Qur-aan Majeed:
إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُولَٰئِكَ يُبَدِّلُ اللَّهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ ۗ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٧٠﴾
(Mwenye kuyafanya madhambi haya ya shirki, kuua na kuzini hatosamehewa na ataadhibiwa ndani ya Jahannam,) isipokuwa akitubia, akaleta Imaan, na akafanya matendo mema, kwa sababu Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) atabadilisha maovu ya watu hao kuwa mema, na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
Alipoisikia Aya hii, Wahshi (Radhiyallahu anhu) akajibu: “Ewe Muhammad (Sallallahu alaihi wasallam)! Ingawa katika Aya hii, Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) aliahidi kuwasamehe wale watu waliotenda dhambi hizi ambazo nimeyafanya, lakini msamaha wao una masharti.
“Sharti ni kwamba watubu, walete Imaan na watekeleze matendo mema katika maisha yao. Nitajuaje kama nitaweza kutimiza sharti hili (na hivyo kupata msamaha wa Allah Ta’ala)?”
Kisha Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) akateremsha Aya ifuatayo:
إِنَّ اللَّهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ
Hakika Allah Ta’ala hasamehi kushirikishwa, lakini husamehe madhambi yote kwa amtakaye.
Aliposikia Aya hii, Wahshi (Radhiyallahu anhu) akajibu, “Ewe Muhammad (Sallallahu alaihi wasallam)! Naona kwamba katika Aya hii, Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) Ametaja kwamba Atasamehe madhambi ya amtakaye.Hata hivyo, sijui kama Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) Atanisamehe au la. Je, kuna kitu kingine chochote ambacho unaweza kuniambia (hivyo litanipa matumaini ya kusamehewa)?”
Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) alinyamaza na hakujibu, mpaka Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) akateremsha aya ifuatayo ya Qur-aan:
۞ قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّهِ ۚ إِنَّ اللَّهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ ﴿٥٣﴾
Enyi waja wangu mliojidhulumu nafsi zenu! Msikate tamaa na rahma ya Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah). Mwenyezi Mungu(subhaanahu wata’ala) husamehe dhambi zote, hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
Wakati Wahshi (Radhiyallahu anhu) alivyoisikia aya hii, alisema, “Ndio! Aya hii (ndiyo aya ambayo imenipa matumaini ya mimi kupata msamaha)!” Kwa kusema hivi, mara moja akasilimu.
Maswahaabah (Radhiyallahu anhum) kisha wakauliza kutoka kwa Mtume (Sallallahu alaihi wasallam): “Ewe Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam)! katika aya hii, Allah Ta‘ala ameahidi kuwa atawasamehe wale ambao watarudi kwake kuomba msamaha. Je hii ahadi inatuhusu na sisi?
Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akajibu: “Ahadi hii inawahusu Waislamu wote (wanaotubia kwa Mwenyezi Mungu).
Kutokana na tukio hili, tunaona mapenzi makubwa aliyonayo Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) kwa waja wake.
Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) anapenda kuwasamehe waja wake. Haijalishi mtu yuko mbali na dini kiasi gani, na dhambi zake zinavyokuwa nyingi kiasi gani na mbaya kiasi gani, ikiwa atarejea kwa Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) na toba ya kweli na akaweka dhamira thabiti ya kurekebisha hali yake, basi hakika Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) atamsamehe.
Rehma Kubwa na Msamaha wa Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah)
Imepokewa katika Hadith Qudsi kwamba Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) Anasema, “Ewe bin Aadam (alaihis salaam)! maadamu mnatubia kwangu na kuwa na matumaini na msamaha wangu, nitawasamehe madhambi zenu, wala sijali (hakuna wa kuuliza mamlaka wangu).
“Ewe bin Aadam (alaihis salaam) Hata madhambi zenu zikifika kwenye mawingu ya mbingu, kisha ukatubu kwangu kwa kuomba msamaha, nitakusamehe na wala sijali (hakuna wa kuuliza mamlaka wangu).
“Ewe bin Aadam (alaihis salaam)! Ukinijia na dunia iliyojaa na madhambi na ukaja kwangu hali ya kuwa hunishirikishi, nitakujia na dunia yenye imejaa na msamaha.”
Hivyo, Muumini hapaswi kamwe kukata tamaa na kupoteza matumaini kwenye rehma ya Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah). Maadamu kuna maisha basi kuna matumaini.
Allah Ta’ala Atujaalie sote tawfeeq ya kurejea Kwake mara kwa mara katika toba, ameen.
Alislaam Juhudi za Kuleta uislam ndani ya maisha yetu