Bishr Haafi (rahimahullah) alikuwa mchamungu mashuhuri katika zama zake. Wakati mmoja, mtu fulani alimuuliza, “Umeipataje nafasi hii ya juu ya uchamungu na uadilifu tunayoiona?” Katika kujibu, Bishr (rahimahullah) alitaja yafuatayo:
Chochote ambacho nimebarikiwa nacho ni kupitia neema ya Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala). Hali yangu ya awali ilikuwa kwamba sikuwa mtu wa kujitolea kwa deen.
Siku moja, nilipokuwa nikitembea, niliona kipande cha karatasi chini. Pindi nilipoiokota, nikakuta jina la Allah Ta’ala limeandikwa juu yake. Niliinua macho yangu mbinguni na kusema, “Ewe Mwenyezi Mungu! Hili ni jina lako lililobarikiwa ambalo limetupwa chini!”
Kisha nilisafisha karatasi na kuiweka mfukoni mwangu kwa heshima zote.
Wakati huo, nilikuwa na dirham mbili tu. Nikaelekea kwenye duka la manukato, nikanunua manukato na kuipaka kwenye karatasi ile. Baada ya hapo, nilienda nyumbani, na kuiweka juu ya kabati.
Usiku ule, niliota ndoto ambayo ndani yake niliambiwa, “Ewe Bishr! Umeinuwa jina letu basi sisi tutainuwa jina lako duniani na akhera.” Ilikuwa ni kwa ajili ya kitendo hiki ambapo Mwenyezi Mungu alinipa nafasi hii.
Kutokana na tukio hili, tunaelewa kwamba wakati Bishr Haafi (rahimahullah) alionesha heshima kwenye jina la Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala), basi Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) akambariki tawfeeq ya kubadilisha maisha yake.
Mbali na hayo, Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) Akambariki na ufahamu wa kweli wa Quran na Hadithi za Mtume (Sallallahu alaihi wasallam). Kwa hiyo, alihesabiwa miongoni mwa Muhaddithin wa zama zake.
Huo ndio ulikuwa msimamo wake mkubwa hadi Imaam mkubwa wa zama zake Imam Ahmad bin Hanbal (rahimahullah) amesimulia Hadithi kutoka kwake na kufaidika na ujuzi wake wa kina.
Maulamaa wanaeleza kuwa kuonyesha heshima kwa kitu chochote kile inayohusishwa na Dini (yaani Quran Majeed, Hadith, Msikiti, Adhaan, Maulamaa (masheikhe) , Huffaaz (wenye kuhifadhi Quran, n.k.) ni njia ya kupata baraka kubwa na kukubaliwa na Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala).
Imam Ahmad bin Hanbal (rahimahullah) Akinufaika Kutoka Kwa Bishr Hafi (rahimahullah)
Tukio lifuatalo linatoa mwanga juu ya uelewa wa kina wa Dini na ma’rifa (utambuzi) wa Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) ambayo Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) Amembariki nayo Bishr Hafi (rahimahullah), ambayo kwa ajili yake Imam Ahmad bin Hambal (rahimahullah) alimuiga:
Wakati wa Imaam Ahmad bin Hambal (rahimahullah), kulikuwa na daktari fulani ambaye aliitwa Abdur Rahmaan At Tabeeb.
Alikuwa akimtibu Imam Ahmad bin Hanbal na Bishr Hafi (Rahimahumallah) walipokuwa wagonjwa. Anasema:
Wakati mmoja, Imam Ahmad bin Hanbal (rahimahullah) na Bishr Hafi (rahimahullah) walikuwa wagonjwa wote.
Wakati wa kuwatibu wote wawili, niliona tofauti katika majibu wakati niliwauliza hali zao.
Kila nilipomuuliza Bishr (rahimahullah) anajisikiaje, kwanza alikuwa akimtukuza Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) akisema “Alhamdulillah”, na kisha kunijulisha hali yake.
Kinyume chake, kila nilipomuuliza Imam Ahmad bin Hanbal (rahimahullah), jinsi gani anavyojisikia, alikuwa akijibu tu kwamba alikuwa mzima. Hakunieleza ugumu halisi aliokuwa akipitia.
Siku moja, nilimwambia Imaam Ahmad (rahimahullah) na kusema, “Ndugu yako, Bishr (rahimahullah), ni mgonjwa, na ninapomuuliza hali yake, huanza kwa kumhimidi Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) na kisha kunijulisha hali yake.
“Lakini, ninapokuuliza kuhusu hali yako, unasema tu kwamba upo mzima.”
Imaam Ahmad (rahimahullah) aliposikia haya, alisema, “Muulize Bishr (rahimahullah) ni kwa nani amejifunza haya.”
Nilijibu, “Ninahisi vigumu kumuuliza swali kama hilo.” Imaam Ahmad (rahimahullah) akaniambia, “Mwambie, ‘Ndugu yako, Abu Abdillah (Imaam Ahmad) anataka kukuuliza ni kwa nani umejifunza haya.”
Nilijibu, “Ninahisi vigumu kumuuliza swali kama hilo.”
Imaam Ahmad (rahimahullah) hivyo akaniambia, “Mwambie, ‘Ndugu yako, Abu Abdillah (Imaam Ahmad) anataka kukuuliza ni kwa nani umejifunza haya.”
Nilipokwenda baada ya hapo kwa Bishr (rahimahullah), nilimpelekea swali la Imaam Ahmad (rahimahullah).
Aliposikia swali hilo alisema: “Njia ya Ahmad ni kwamba hatekelezi amali ya elimu yoyote bila ya kuthibitisha chanzo chake.”
Kisha Bishr (rahimahullah) akasema, “Azhar (rahimahullah) anasimulia kutoka kwa Ibnu Awn (rahimahullah), ambaye anasimulia kwamba Ibnu Sirin (rahimahullah) alisema, ‘Mja anapomhimidi Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) kabla ya kueleza shida na hali yake, basi usemi wake hauchukuliwi kama malalamiko (kinyume na maqadara ya Mwenyezi Mungu).’”
Bishr (rahimahullah) akasema: “Wakati wowote utakaponiuliza kuhusu hali yangu, na nikakujulisha shida ninayopitia, basi nafanya hivyo tu ili kudhihirisha udhaifu wangu na kukuonyesha uwezo alio nao Mwenyezi Mungu juu yangu.
Baada ya kupata jibu hili, nilikwenda kwa Ahmad (rahimahullah) na akamjulisha yale Bishr (rahimahullah) amesema.
Kuanzia siku hiyo na kuendelea, kila nilipokuwa nikimwendea Ahmad na kumuuliza kuhusu hali yake, kwanza alikuwa akimtukuza Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) na baada ya hapo kunijulisha hali yake.
Kutoka tukio hili, tunaelewa yafuatayo:
1. Elimu ya Dini inapaswa kuthibitishwa kutoka kwa Maulamaa walioongoka kabla mtu hajaitekeleza.
2. Mtu anapopitia shida yoyote, anatakiwa amsifu Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) kwa kusema ‘Alhamdulillah’, akimuonyesha Mwenyezi Mungu kuwa ameridhika na hukumu yake, pamoja na ugumu anaoupata.
3. Wakati wa shida, mtu anapaswa kusema ‘Alhamdulillah’, kwa hivyo kukumbuka neema zisizohesabika za Mwenyezi Mungu juu yake na kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu hata wakati huu.
4. Mtu anaposema ‘Alhamdulillah’ kabla ya kueleza ugumu wake, ni wazi kwamba mtu halalamikii hukumu ya Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala).
5. Ni Sunnah kwa mtu kuchukua njia za halali katika kutibu maradhi yake.
Allah Ta’ala Atujaalie ufahamu wa kweli wa Dini na tawfeeq ya kukanyaga nyayo za wachamungu wetu waliotangulia.
Alislaam Juhudi za Kuleta uislam ndani ya maisha yetu