Machozi ya Toba – Maji ya Kusafisha Moyo

Shah Ruknuddeen (rahimahullah) alikuwa ni Mwanachuoni mkubwa na mchamungu aliyeishi Multan. Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) alimkubali sana miongoni mwa watu wake. Siku ya Jumu’ah, msikitini ilikua ikijaa na watu wanaokuja kutoka sehemu mbali mbali ili kunufaika kutoka kwake.

Siku moja, mfalme, Ghiyaathuddeen Tughluq, alimgeukia mshauri wake, Moulana Zaheeruddeen, na akamuuliza, “Nimeona kwamba karaamah (miujiza) ya Shah Ruknuddeen (rahimahullah) inajulikana sana miongoni mwa watu. Moulana Zaheeruddeen (rahimahullah) alijibu, “Ni karamah gani inaweza kuwa kubwa zaidi kuliko ukweli kwamba bila yeye kuwaalika watu, makundi ya watu wankusanyika kwake!”

Moulana Zaheerudden (rahimahullah) anataja:

Kwa kuwa mfalme alikuwa ameniuliza swali hili, nilihisi ni lazima nimpe jibu linalofaa. Walakini, ndani kabisa ya moyo wangu, sikuwa na uhakika na uchamungu wa Shah Ruknuddeen. Nilihisi kwamba labda watu hawaji kwake kwa sababu ya uchamungu wake. Badala yake, inawezekana kwamba ana amal (zoezi) ambalo kupitia hilo watu wanavutiwa naye. Kwa wazo hili akilini, niliamua kwamba niende kwa Shah Ruknuddeen (rahimahullah) siku iliyofuata ili kumjaribu na kubaini kama alikuwa mchamungu wa kweli au la.

Niliamua kwamba nikikutana naye, ningemuuliza kuhusu hekima nyuma ya sheria fulani za dini. Hasa, nilikusudia kumuuliza juu ya hekima ya kuosha mikono, kusugua mdomo na kuingiza maji kwenye pua mwanzo wa wudhu.

Baada ya kupanga hivyo, nilikwenda kulala, na nikiwa usingizini, niliona katika ndoto kwamba nilimtembelea Shah Ruknudden (rahimahullah). Nilipokutana naye, alinipokea kama mgeni na kunipa chakula kitamu ambacho nilikula.

Nilipoamka asubuhi iliyofuata, nilishangaa sana kuhusu ndoto niliyokuwa nimeona, na nilishangaa zaidi kugundua kwamba bado naweza kuonja chakula kitamu kinywani mwangu! Kwa kweli, ladha ya chakula ilibaki kinywani mwangu siku nzima!

Licha ya kuiona ndoto hii, moyo wangu haukuathirika na ndoto hio ya Shah Ruknudden (rahimahullah) na maoni yangu hayakubadilika. Niliwaza mwenyewe, “Watu huona ndoto kila wakati, na shetani ana uwezo wa kumfanya mtu aone ndoto kama hii. Kwa hivyo, sipaswi kuzingatia ndoto hii. Hivyo, niliamua kukutana naye, nikiwa na wasiwasi moyoni mwangu.

Nilipofika kwenye khanqah yake, alinisalimia na kufanya musaafahah (kusalimiana kwa mikono). Baada ya hapo, alinihutubia akisema, “Moulana! Nina furaha kwamba umekuja! Moyo wangu ulitamani kushiriki katika majadiliano ya kielimu, na kwa hiyo nimekuwa nikitafuta sheikhe wa dini kama wewe! Ni vizuri umekuja!”

Baada ya kunikaribisha kwa namna hii, alianzisha mjadala akisema, “Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) ametuneemesha na dini ya utakaso na usafi wa hali ya juu. Usafi wa dini hii ambayo hakuna mtu anayeweza kupinga amri yoyote ya shari’ah.

“Fikiria mfano wa wudhu, tunapofanya wudhu, Mwenyezi Mungu anatuelekeza tuoshe mikono yetu kwanza, kisha tusutue midomo yetu, na kisha tuingize maji kwenye pua zetu.

Wakati Shah Ruknuddeen (rahimahullah) anataja hili, Moulana Zaheeruddeen (rahimahullah) aligundua kwamba Shah Ruknuddeen (rahimahullah) alikuwa akijadili maswali yale yale ambayo alikuwa amepanga kumjaribu Shah Ruknuddeen usiku uliopita.

Shah Ruknuddeen (rahimahullah) kisha akaendelea na kusema, “Ikiwa mtu ni mjinga na hana ufahamu wa Dini, basi atajiuliza, ‘Kuna hikima gani nyuma ya maamrisho haya?’ Hata hivyo, kwa hakika, kuna hekima kubwa nyuma ya maamrisho haya.

“Sababu ni kwamba shari’ah imetuwajibikia sisi kusafisha miili yetu kwa maji masafi. Maji masafi ni yale maji ambayo hayana rangi, ladha na harufu. Ikiwa tunachunguza matendo matatu ya kwanza ya wudhu, tutaona kwamba yanatusaidia kuamua kama maji yana sifa hizi tatu (hayana rangi, ladha na harufu), hivyo basi kustahiki udhu.

“Sifa ya kwanza ni rangi ya maji. Kwa kuchukuwa maji ya kunawa mikono, mtu ataweza kuona ikiwa rangi ya maji imebadilika kwa njia yoyote.

“Sifa ya pili ni ladha. Kwa kusutuwa mdomo, mtu atakuwa na uwezo wa kuonja ladha ya maji.

“Sifa ya tatu ni harufu ya maji, na kwa kuingiza maji puwani, mtu ataweza kujua kama harufu ya maji imebadilika.

“Huu ndio uzuri wa shari’ah yetu– kuna manufaa makubwa na hekima nyuma ya kila amri iwe kubwa au ndogo (baadhi tunayaelewa, na mengine ambayo hatuyaelewi). Hiyo ndiyo hekima iliyo nyuma ya shari’ah yetu hadi kwamba akili ya mtu kamwe haiwezi kuipinga shari’ah.”

Kisha Shah Ruknuddeen (rahimahullah) akasema, “Moulana hili ni amri ya shari’ah kuhusu mtu ambaye hana wudhu – kwamba atoharishe baadhi ya viungo na maji.

“Ama mtu ambaye yuko katika hali ya janaaba, basi shari’ah inamuamuru kufanya ghusl na kuosha mwili wake wote. Tukichunguza agizo hili, basi kwa nje, inaonekana kuwa kitu cha kushangaza.

Mtu akifanya tendo la ndoa na mke wake, hili linasababisha mwili wake wote kuingia katika hali ya janaba, na utakaa katika hali hii hadi afanye ghusl. Hili linajulikana kwa watu wote.

“Hata hivyo, janaabah ni aina tu ya uchafu wa kimwili ambayo mwili utahitaji utakaso. Kwa kulinganisha na hii, kuna aina nyingine ya uchafu – uchafu wa moyo – na hii pia inahitaji utakaso. Basi ni kitu gani kinachosababisha uchafu wa moyo?

“Tumeona kwamba mtu anapoingiliana na mke wake, ambaye ni halali kwake, humfanya mwili wake wote kuwa najisi. Hali inapokuwa hivi, basi fikiria athari kwenye moyo wa mtu anapobaki katika kundi la watu waovu na wakutenda madhambi na watu walio mbali na Dini na hawakushikamana na shari’ah? Hebu wazia uchafu mkubwa unaopatikana moyoni mwake!

“Hata hivyo, swali ni, ‘Tunajua jinsi ya kuitakasa miili yetu na wudhu na ghusl, lakini je ‘Tunazitakasa vipi nyoyo zetu wakati mioyo zetu zinapozama katika madhambi?’”

Katika hatua hii, Moulana Zaheeruddeen (rahimahullah) hakuweza tena kuzuia machozi yake na akaanza kulia. Alitambua kwamba bila yeye hata kutaja maswali yake, Shah Ruknuddeen (rahimahullah) alikuwa ameanza kuyajadili na alikuwa ameshughulikia pingamizi zote akilini mwake.

Alitambua kwamba Shah Ruknuddeen (rahimahullah) alikuwa hakika mchmungu mkubwa na hivyo akajihisi mwenye kujuta juu ya mwenendo wake na maoni mabaya aliyokuwa nayo kuhusu yeye.

Moulana Zaheeruddeen (rahimahullah) alimgeukia Shah Ruknuddeen na kusema, “Sheikhe! Mimi sijui kabisa kuhusu mambo ya moyo na utakaso wa moyo. Tafadhali, niambie jibu!”

Shah Ruknuddeen akajibu, “Mwili unapokuwa najisi, basi maji masafi hutumika kuusafisha. Ama mtu ambaye moyo wake ni mchafu, basi naye anahitaji ‘maji’ kuusafisha.

“Lakini, ‘maji’ anayohitaji kusafisha moyo ni “machozi” ya macho. Mja anapomlilia Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) kutubia na kujuta juu ya dhambi zake, basi kwa kulia kwake kwa majuto, Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) Huusafisha moyo wake.”

About admin

Check Also

Kamwe Usipoteze Matumaini Katika Kumrekebisha Mtu Yoyote

Kamwe Usipoteze Matumaini Katika Kumrekebisha Mtu Yoyote Abdullah bin Maslamah Qa’nabi (rahimahullah) alikuwa miongoni mwa …