Ushauri wa Mwisho wa Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) kwa Mu’aaz (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipomtuma Yemen.

Wakati Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) alipokuwa akimtuma Mu’aaz bin Jabal (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwenda Yemen kuwafundisha watu Dini na kuwatawala, Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akamshindikiza mpaka nje ya Madina Munawwarah huku akimpa ushauri wake wa mwisho.

Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) alimuamrisha kufanya baadhi ya matendo mema, na akamuamrisha kujiepusha na vitendo fulani. Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akamwambia:

“Ewe Mu’aaz! Nakunasihi kama vile ndugu mkweli na mwenye huruma anavyomshauri ndugu yake. Nakunasihi umche Mwenyezi Mungu siku zote, useme ukweli, utimize ahadi zako, utekeleze amana uliyopewa, ujiepushe na khiana na udanganyifu, uwemkarimu kwa mayatima, ulinde haki za ma jirani, kuzuia hasira yako, kuwa mnyenyekevu daima, kutoa salaamu (kwa wale unaokutana nao), kuzungumza kwa adabu, kuwa na msimamo katika Imaan, kutafakari kwa kina juu ya Qur-aan. (ifuate kwa usahihi), kuwa na mapenzi ya Akhera (ndani ya moyo wako), kuogopa hisabu na uwajibikaji (mbele ya Mwenyezi Mungu Siku ya Qiyaamah), kuzuia matarajio na matamanio yako ya dunia, na kuzidisha kutenda mema.

Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) pia akamwambia: “Ninakukataza kumtukana Muislamu, kumkanusha mkweli, kuamini habari za mwongo, na kumuasi kiongozi muadilifu ambaye ameteuliwa juu yenu (yaani wakati wowote katika maisha yako, ikiwa mtu atawekwa juu yenu na khalifah, basi mnapaswa kumtii).

“Ewe Mu’aaz! Mkumbuke Mwenyezi Mungu kwenye kila jiwe na kila mti (yaani unapotembea juu ya ardhi, unapopita karibu na jiwe au mti, daima mkumbuke Allah Ta’ala kila wakati). Ikiwa utafanya dhambi (kutokana na udhaifu wa kibinadamu), basi mara moja rekebisha kwa kufanya tawbah. Ikiwa dhambi imefanywa kwa siri, basi fanyeni tawbah kwa siri, na ikiwa dhambi hiyo imefanywa hadharani, basi tawbah hadharani.”

Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akaongeza: “Siku zote watembelee wagonjwa, harakisha kuwatimizia wajane na Waislamu wanyonge, baki katika kundi la masikini, watendee haki watu hata kama inakuhusu wewe (yaani. hata kama inahusiana na haki zako), ongea ukweli daima, na katika njia ya Mwenyezi Mungu msiwe na wasiwasi juu ya ukosoaji wa mtu yoyote.” (Hilyatul Awliyaa 1/240)

Kwa mujibu wa riwaya nyingine, kabla ya kumuaga Mu’aaz (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa buriani, Nabii. (Sallallahu alaihi wasallam) akamwambia: “Pengine hutanikuta baada ya mwaka huu (kwa maneno mengine, huu ndio mkutano wetu wa mwisho) Huenda (utakaporudi Madinah) utapita kwenye msikiti wangu au kaburi langu.

Mu’aaz (Radhiya Allaahu ‘anhu) alielewa hii kuwa ni dalili ya wazi kwamba Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) atafariki dunia na kwamba hakutakuwa na fursa nyingine ya yeye kuonana na kukutana na Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) baada ya hapa. Aliposikia hivyo, Mu’aaz (Radhiya Allaahu anhu) alianza kulia kwa huzuni baada ya kutengana na Mtume (Sallallahu alaihi wasallam).

Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) hakutaka kuutazama uso wake huku akilia, na hivyo akauelekeza uso wake wa baraka kuelekea upande wa Madinah Munawwarah. Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) akamfariji akisema: “Hakika watu walio karibu nami ni wale ambao wana taqwa (yaani kumcha Mwenyezi Mungu katika maisha yao) popote walipo.” (Musnad Ahmad #22052)

Kwa maneno mengine, Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) alimueleza kwamba ikiwa utashikamana na taqwa na sunnah zangu, basi licha ya kuishi mbali nami katika ardhi nyingine, utakuwa karibu nami. Badala yake, ikiwa unaishi karibu nami (kama Madinah Munawwarah), lakini huna taqwa na sunna katika maisha yako, basi ingawa wewe kimwili unaishi karibu nami, kwa hakika, uko mbali nami.

About admin