
Wahab bin Munabbih (rahimahullah) anasema:
Baada ya Abdullah bin Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa kipofu (katika uzee wake), niliwahi kumuongoza kwenye Haram huko Makka Mukarramah, ambapo alisikia kundi la watu wakizozana wao kwa wao. Akaniomba nimuongoze kwao.
Alipofika kwao, aliwasalimia kwa “Assalaamu Alaikum”. Walimuomba akaye lakini akakataa na akasema: Je! Niwajulisheni kuhusu nani ambaye ana daraja kubwa mbele ya Allah Ta‘ala? Wale ambao khofu ya Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) imewanyamazisha, ijapokuwa si wanyonge wala si mabubu. Kwa kweli, wanaweza kuzungumza vizuri sana na kuelewa vizuri. Hata hivyo, zikr ya Allah Ta’ala imewazidi nguvu kwa sababu hiyo hawazungumzi sana. Wanapozidiwa na kumkumbuka Allah Ta’ala, basi hukimbilia kwenye mambo ya kheri. Kwa nini mmekengeuka kutoka katika njia ya watu hawa?”
Wahab bin Munabbih (rahimahullah) anasema, “Baada ya mawaidha haya, sikuwahi kuona hata kundi la watu wawili wakiwa wamekaa pamoja kwenye Haram (na wakifanya mazungumzo ya kidunia).”
Inasemekana kwamba Ibnu Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alikuwa akilia sana kwa khofu ya Allah Ta‘ala kiasi kwamba machozi yaliyokuwa yakitiririka mashavuni mwake yalikuwa yameacha alama kwenye mashavu.
Sheikh Moulana Muhammad Zakariyya (rahimahullah) alitaja kuhusu tukio hilo hapo juu:
Katika tukio hili, Abdullah bin Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ameonyesha njia rahisi sana ya kufanya mambo mema. Huku ni kutafakari na kufikiria ukuu wa Allah Ta’ala. Hili likifanywa, inakuwa rahisi sana kufanya matendo mengine yote mazuri kwa uaminifu. Je, ni vigumu sana kutumia dakika chache, kati ya saa ishirini na nne za siku, kufikiria juu ya ukubwa wa Allah Ta‘ala?
(Fazail-ul-A’maal 43-44,)
Alislaam Juhudi za Kuleta uislam ndani ya maisha yetu