Siku ya Qiyaamah – Siku ya Majuto kwa Wengi

Ndani ya Quran Majeed, Siku ya Qiyaamah imetajwa na majina mbalimbali. Baadhi ya majina hayo ni “Siku ya Malipo”, “Siku ya Kukusanywa”, “Siku ya Hasara na Faida” (yaani hasara kwa makafiri na faida kwa waumini), na “Siku ya Mkutano” (yaani kukutana na Allah Ta‘ala).

Tunapochunguza majina haya, tunaelewa kwamba kila jina linaonyesha hali siku ya Qiyaamah itakuwepo.

Miongoni mwa majina ya Siku ya Qiyaamah pia ni “Siku ya Majuto.” Siku hii itakuwa ni siku ya majuto makubwa kwa makafiri, kama jinsi Allah Ta’ala Anavyoeleza katika Quraan Majeed:

(Ewe Muhammad !) Waonye (makafiri) kuhusu Siku ya Majuto, itakapopitishwa uamuzi (yaani waingizwe katika Moto wa Jahannam na wakae humo milele).

Kutokana na hili, tunaelewa kwamba Siku ya Qiyaamah itakuwa ni siku ya majuto yasiyofikirika kwa makafiri.

Hata hivyo, kama vile itakavyokuwa siku ya majuto makubwa kwa makafiri, pia itakuwa, kwa kiasi fulani, siku ya majuto kwa baadhi ya waumini.

Majuto Pekee ya Watu wa Jannah

Kuhusiana na majuto ya Waumini, Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) amesema: “(Kabla ya kuingia Jannah), majuto pekee ambayo watu wa Jannah watakuwa nayo ni nyakati zilizopita (duniani) bila ya wao kumdhukuru Allah Ta’ala.”

Wakati Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) Atakapokuwa akiwapa waja Wake malipo makubwa na adhimu kwa muda walioutumia katika kumkumbuka, waumini wengine watajawa na huzuni na majuto juu ya muda na fursa zenye thamani walizozipoteza duniani bila kumdhukuru Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala).

Tukio la Maysarah bin Masrooq Abasi

Ifuatayo ni tukio ambalo linaangazia thamani kubwa ya Imaan na maisha, na umuhimu wa kutoghairisha katika kutekeleza amali njema.

Abdullah bin Waabisah Abasi anaripoti tukio lifuatalo kutoka kwa babu yake. Tukio hili lilijiri kabla ya babu yake kusilimu. Anataja:

Wakati mmoja, katika siku za mwanzo za Uislamu, Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) ametujia tukiwa kwenye kambi yetu ya Mina. Wakati Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) alipotujia, alikuwa akiendesha usafiri wake huku Zaid bin Haarithah akiwa amekaa nyuma yake. Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) kisha akazungumza nasi na akatuita kwenye Uislamu.

Hata hivyo, Wallahi, hatukukubali mwaliko wake, na wema haukuandikiwa wakati huo. Tuliwahi kumsikia kabla ya haya na pia tulimsikia akiwalingania watu kwenye Uislamu katika siku za hajj. Sasa aliposimama mbele yetu na kutulingania katika Uislamu, hatukuitikia na kuukubali ujumbe wake.

Miongoni mwa kundi letu alikuwemo mtu anayeitwa Maysarah bin Masrooq Abasi. Baada ya kuusikia ujumbe na mwaliko wa Mtume (Sallallahu alaihi wasallam), aliwaeleza watu wake, “Ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu! Iwapo tutaukubali ujumbe wa mtu huyu na tukamchukua pamoja nasi, mpaka tumfanye kukaa kati yetu na kuishi kati yetu, basi tutakuwa tunafanya yale ambayo ni ya busara na manufaa kwetu! Ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu na ninahisi kwamba ujumbe wake utashinda na kwenda mbali zaidi!”

Hata hivyo, watu wa ukoo wake wakasema, “Tuache katika hili na usituhusishe katika jambo ambalo liko nje ya uwezo wetu wa kulisimamia.” Hata hivyo, kwa kuona kwamba alikuwa ameonyesha mwelekeo fulani, Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akawa na matumaini na Maysarah kuukubali Uislamu na hivyo kuzungumza naye zaidi.

Baada ya kusikia maneno yenye baraka na ujumbe wa Mtume (Sallallahu alaihi wasallam), Maysarah akajibu akisema, “Jinsi gani maneno yako yalivyo bora na jinsi yanavyong’aa na noor! Ikiwa ukoo wa mtu hauko tayari kumsaidia, basi kuna uwezekano mkubwa zaidi kwamba ataweza kupata usaidizi kutoka kwa wengine.”

Alipopokea majibu haya, Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) aligeuka na kuondoka na ukoo wa Banu Abas nao wakaondoka, wakarudi kwa familia zao.

Katika safari ya kurudi, Maysarah aliwaambia watu wake, “Tupitie njia ya Fadak, kwa sababu Mayahudi wanaishi humo na tutaweza kuwauliza kama wana ujuzi wowote kuhusu mtu huyu aliyedai utume.”

Watu wa ukoo wake walikubali, na hivyo wakaenda Fadak.

Walipofika Fadak na kuwauliza Mayahudi. Mayahudi wakatoa sehemu ya Kitabu chao kitakatifu, Taurati na kisha kuanza kusoma maelezo ya mtume (Sallallahu alaihi wasallam) wa mwisho ambayo ilirekodiwa ndani ya maandiko yao.

Maelezo waliyosoma yalikuwa:

Nabii wa mwisho atakuwa hana ujuzi wa kusoma na atatoka katika ardhi ya Uarabuni. Atatumia ngamia kama usafiri wake na atatosheka na vipande vichache vya mkate kuwa chakula chake. Hatokuwa mrefu kupita kiasi wala mfupi sana (lakini urefu wa wastani). Nywele zake hazitakuwa za pilipili wala za kunyooka. Macho yake yatakuwa na uwekundu (yaani uweupe ya macho yake yatakuwa na wekundu).

Basi Wayahudi wakasema, “Ikiwa yule aliyekualika kwenye dini anafuatisha maelezo haya, basi ukubali ujumbe wake na kuikumbatia dini yake.

“Kwa jinsi tulivyo basi hatutamfuata kwa sababu mioyo zetu imejazwa na wivu juu yake, tunajua tutapigana vita dhidi yake sehemu mbalimbali pia. Kutoka kwa Waarabu, kila mtu atamfuata au atapigana naye, basi hakikisha kwamba wewe ni miongoni mwao wanaomfuata.”

Maysarah aliposikia haya, alizungumza na ukoo wake na kusema, “ Enyi watu! Suala hili, la je Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) ni Mtume wa kweli wa Allah, sasa liko wazi kabisa!” Lakini, watu wake walikawia na kusema, “Tutakaporudi kuhiji mwaka ujao, tutakutana naye na kusilimu.”

Hivyo wakarudi katika nchi yao, na watu wengine wa ukoo wao haukukubali walichosema na hawakutaka kufanya kama walivyopendekeza. Kwa namna hii, miaka ilipita, mpaka Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akahijiria Madina Munawwarah. Hatimaye, Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) aliporudi Makkah Mukarramah kufanya hajj ya kuaga), Maysarah alikutana naye na akamtambua.

Maysarah alikuja kwa Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akasema: “Ewe Rasulullah! Toka ule wakati ulipopita kwetu na usafiri wako kuongea na sisi, niliendelea kutamani nije kwako na kusilimu na kukufuata. Lakini, kulikuwa dharura ikijitokeza kila wakati, na kwa namna hii muda uliendelea kupita. Kwa hiyo, kama unavyoona, kusilimu kwangu kumecheleweshwa hadi sasa.

“Ama kuhusu jamaa zangu wengine uliozungumza nao huko Mina, wote wamefariki, niambie ewe Nabii wa Mwenyezi Mungu! Makazi yao ipo wapi, Jannah au Jahannamu.

Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akajibu: “Kila mtu atakayekufa katika dini isiyokuwa ya Uislamu atakuwa ndani ya Jahannam. Kusikia hivyo, Maysarah akasema, “Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliyeniokoa na Jahannum!”

Baada ya hapo alisilimu na akawa Mwislamu mchamungu, mkweli, kiasi kwamba aliheshimiwa sana na Abu Bakr (radhiyallahu anhu) katika kipindi cha Ukhalifa wake.

About admin

Check Also

Mchamungu wa Wakati Wake – Bishr Haafi (rahimahullah)

Bishr Haafi (rahimahullah) alikuwa mchamungu mashuhuri katika zama zake. Wakati mmoja, mtu fulani alimuuliza, “Umeipataje …