Waa’il bin Hujr (Radhiyallahu anhu) alikuwa sahaabi maarufu wa Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) ambaye alitoka katika nchi ya Yemen na kutoka katika kizazi cha wafalme.
Inaripotiwa kwamba wakati aliondoka Yemen kuja Madinah Munawwarah kusilimu, basi kabla ya kusiliku, Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) aliwajulisha maswahaabah kama amefika.
Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) aliwaambia maswahaabah (Radhiyallahu anhum), “Kuna mtu ambaye anakaribia kufikia Madinah Munawwarah kutoka nchi ya Hadramowt huko Yemen. Anakuja na nia ya Kusilimu, na anatoka katika kizazi cha wafalme. Jina lake ni Waa’il bin Hujr. ”
Alipofika, Rasulullah alimkaribisha, akamkirimu, na kumtandikia kitamba chake cha baraka ili akae. Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) akamuombea dua Maalum kwa ajili yake akisema, “Ewe Mwenyezi Mungu! Mjalie waail na baraka, na watoto zake na wajukuu. ” Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) akamchagua kama naibu wake juu ya watu wa Yemen.
Kabla ya kuondoka kutoka Madinah Munawwarah, alimuomba Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) ampe ardhi huko Yemen. Kwa ombi lake, Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) alimchagulia kiwanja cha Yemen, na akamwagiza Mu’aawiyah (Radhiyallahu anhu) aende naye Yemen ili am amkatie kiwanja chake na kumkabidhi.
Ipasavyo, waa’il na Mu’aawiyah (Radhiyallahu anhuma) aliondoka pamoja kutoka Madinah Munawwarah. Waa’l (Radhiyallahu anhu) alikuwa akisafiri kwenye ngamia, wakati Mu’aawiyah(Radhiyallahu anhu) alikuwa akisafiri kwa miguu. Wakati huo, Mu’aawiyah (Radhiyallahu anhu) alikuwa masikini sana hata hakuwa na viatu vya kuvaa kufunika miguu yake wakati wa safari.
Walipokuwa wakipitia jangwa la moto, mchanga wa moto ulianza kuchoma miguu ya Mu’aawiyah (Radhiyallahu anhu). Mwishowe, maumivu yalipokuwa makali kwake kuvimilia, alimgeukia waa’al (Radhiyallahu anhu) na akasema, “Tafadhali niruhusu kukaa nyuma yako, juu ya mnyama wako, na kupanda na wewe, kwa sababu mchanga wa jangwa unachoma miguu yangu”.
Lakini, waa’al (Radhiyallahu anhu) akajibu, “Haufai kukaa na wafalme juu ya wanyama zao.”
Mu’aawiyah (Radhiyallahu anhu) alimwomba amwazime viatu, lakini waail (Radhiyallahu anhu) akajibu, “Siwezi kukuazima viatu vyangu, lakini ikiwa unataka, unaweza kutembea kwenye kivuli cha ngamia wangu.” Kusikia jibu hili, Mu’aawiya (Radhiyallahu anhu) alikaa kimya na aliendelea kutembea bila viatu.
Kurudi Madinah Munawwarah, Mu’aawiyah (Radhiyallahu anhu) alimfahamisha Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) kuhusu yale yaliyokuwa yamepitiwa katika safari, na jinsi waa’il (Radhiyallahu anhu) alimfanyia.
Rasulullah alisema, “Ameshikilia Uislamu tu, na kwa hivyo bado ana sifa za Jaahiliyyah ndani yake. Puuzia yale amekufanyia na mfanyie wema.”
Kwa maneno mengine, kwa kuwa waai’l (Radhiyallahu anhu) alikuwa ndo kwanza amesilimu tu na alikuwa ametumia siku chache tu na Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam), sifa za Sunnah za Rasulullah zilikuwa bado hazijapatikana katika maisha yake. Kwa hivyo, katika hafla hii, alifanya hivyo. Lakini, baadaye katika maisha yake, alifikia kiwango kikubwa cha uchamungu na haki.
Mu’aawiyah (Radhiyallahu anhu), wakati huo, alikuwa akiishi maisha ya umaskini. Lakini, Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) aliamuru kwamba wakati utafika atatawala ulimwengu.
Baada ya hapo, Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) alipofariki, Abu Bakr (Radhiyallahu anhu) akawa Khalifah, akifuatiwa na Umar, Uthmaan (Radhiyallahu anhuma) na kisha Ali (Radhiyallahu anhu).
Hatimaye, wakati ukafika ambapo Mu’aawiyah (radhiyallahu anhu) aliteuliwa kama Khalifa wa Waislamu.
Wakati Waa’il (Radhiyallahu anhu) alipogunduwa kuwa Mu’aawiyah amekuwa Khalifah, alitoka kwenda kumtembelea na kutoa heshima zake kwake.
Aliposikia kwamba anakuja, Mu’aawiyah (Radhiyallahu anhu) alikuja kwenye mpaka wa mji ili kumheshimu na kumpokea. Mu’aawiyah (radhiyallahu anhu) kisha akamstarehesha, akamheshimu kwa kukaa naye kwenye sehemu yake na akampa zawadi nyingi.
Mu’aawiyah (radhiyallahu anhu) kisha akamwambia, “Je, unakumbuka siku tuliyosafiri pamoja?” Waa’il (Radhiyallahu anhu) alipokumbuka tukio hilo, na akaona heshima kubwa na wema ambao Mu’aawiyah (radhiyallahu anhu) alikuwa akimwonyesha sasa, basi alihisi majuto makubwa juu ya mwenendo wake wa hapo awali.
Alionyesha majuto yake mbele ya Mu’aawiyah (radhiyallahu anhu) na alikiri kosa lake akisema, “Ewe Ameerul Mu’mineen! Wakati huo, nilikuwa Mwislamu mpya ambaye nilikuwa nimetoka tu kutoka kwenye ukafiri na Jaahiliyyah!
Baadaye, wakati akisimulia tukio hili, Waa’il (Radhiyallahu anhu) alisema, “Wakati huo, nilitamani kama ningemfanya akaye mbele yangu juu ya yule mnyama!”
Katika tukio hili, tunaona kwamba pamoja na matendo ambayo Mu’aawiyah (radhiyallahu anhu) alifanyiwa na Waa’il (Radhiyallahu anhu), hakuwa na kinyongo au hisia zozote mbaya moyoni mwake. Badala yake, alifikia kiwango cha kumwonyesha heshima kubwa, upendo na fadhili.
Hii ilikuwa ni kwa ajili ya yeye kushikamana na ushauri wa Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) kwa kupuuzia kosa la Waa’il (Radhiyallahu anhu) na bado ashughulike naye kwa njia nzuri. Hii ilikuwa ni Sunnah ya Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam)– kwamba siku zote alipuuzia makosa ya watu na kuwasamehe wale waliomuudhi na kumsababishia maumivu.
Allah (subhaanahu wata’alah) Atujaalie sote uwezo na moyo wa kupuuzia makosa ya watu na kuyashughulikia kwa mujibu wa Sunnah na tabia iliyobarikiwa ya Mtume (Sallallahu alaihi wasallam).
Haki Za Majirani
Ili ulimwengu ufanye kazi vizuri na kwa usawa, ni muhimu kwa kila mtu kutimiza haki anazostahili kwa wengine.
Ikiwa haki za watu hazizingatiwi na kutimizwa, basi machafu na mabaya yatatawala duniani. Wizi na unyang’anyi wa mali utakuwa mwingi na dhulma na uadui ndio yatakuwa mambo ya siku zote.
Watu watadhulumu haki za wanyonge na wazee, wanawake na watoto, na kuzinufaisha kwa sababu ya wao kutokuwa na uwezo wa kujisimamia wenyewe na kutetea haki zao.
Hivyo basi, shari’ah imebainisha haki za watu na pia kueleza namna ambavyo haki zao zinapaswa kutekelezwa.
Amri Ya Quraan Majeed Kuhusu Majirani
Ndani ya Qur-aan Majeed, Allah Ta’ala Anasema: “Wafanyie wema wazazi wawili, ndugu, mayatima, masikini, jirani wa karibu na aliye mbali na rafiki yako wa pembeni.”
Katika aya hapo juu, miongoni mwa haki za watu ambazo Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) ametaja ni haki za majirani.
Katika hadithi, Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) ameweka msisitizo mkubwa wa kuzingatia haki za majirani.
Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) amesema: “Muumini wa kweli si yule anayekula na kushiba hali ya kuwa anajua kuwa jirani yake amebaki na njaa.
Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) Akifafanua Haki Za Majirani
Mu’aawiyah bin Haydah (Radhiyallahu anhu) anaripoti kwamba wakati fulani alimuliza Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) ni zipi haki za jirani zangu?
Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akajibu, “Unapaswa kumtembelea (na umuonyeshe kumjali) anapoumwa, uhudhurie mazishi na kilio chake anapofariki, umsaidie mkopo akikuomba, na akipatwa na matatizo kwa kuwa masikini, basi ufiche umaskini wake (yaani. kwa kumsaidia kwa njia ambayo hakuna mtu mwingine atakayejua).
“Ikiwa kitu kizuri kinakuja kwake, basi unapaswa kumpongeza, na akipata msiba basi muhurumieni.
“Zaidi ya hayo, usipandishe jengo lako juu zaidi kuliko lake, na hivyo kuwa njia ya kuzuia uingizaji wa hewa nyumbani kwake.
“Usimletee usumbufu kwa harufu ambayo hutoka kwako (wakati wa kupika, yaani kwa sababu ya yeye kutokuwa na uweo wa kupika chakula cha aina hii, usimletee uchungu juu ya umaskini wake kwa kuruhusu harufu imfikie kwa mfano kuchoma manyama) isipokuwa kama utakusudia kumpa baadhi ya chakula na kumgawia na yeye pia.”
Abdullah bin Amr (Radhiyallahu anhuma) Akipeleka Chakula kwa Jirani Yake Myahudi
Maswahaabah (Radhiyallahu anhum) na wachamungu wa zamani walikuwa wanawajali sana majirani zao kwa sababu ya kufahamu nafasi ya juu anayoipata jirani katika dini.
Abdullah bin Amr (Radhiyallahu anhuma) alikuwa na jirani ambaye alikuwa Myahudi. Wakati mmoja, mbuzi alichinjwa nyumbani kwa Abdullah bin Amr (Radhiyallahu anhuma) na nyama yake ikatayarishwa.
Alipofika nyumbani, aliuliza kutoka nyumbani kwake, “Je, mlimpelekea nyama kwa jirani yetu Myahudi? Nilimsikia Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akisema, ‘Jibra’iil (alaihis salaam) aliendelea kusisitiza juu ya haki za jirani zangu kiasi kwamba nilifikiri (kwamba kwa ajili ya haki kubwa alizonazo katika Dini), pengine Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) atamjumuisha miongoni mwa warithi wa mtu.’”
Tukio la Hasan Basri (Rahimahullah) na Jirani wake Mkristo
Imepokewa kuhusu Hasan Basri (Rahimahullah) kwamba alikuwa na jirani ambaye alikuwa Mkristo.
Hasan Basri (Rahimahullah) aliishi kwenye ghorofa la chini katika mjengo huo na jirani wake Mkristo akiishi juu yake kwenye gorofa la juu.
Maji machafu ya chooni kutoka kwa jirani wake Mkristo juu yake yalikuwa yakivuja ndani mwake. Hata hivyo, Hasan Basri (Rahimahullah) hakuwahi kulalamika kwa jirani yake wala kumfahamisha kuhusu hili.
Hasan (Rahimahullah) aliagiza kwamba chombo kiwekwe chini kwenye sehemu maji hayo yanavuja ili yaangukie humo na yasiharibu nyumba yake.
Kila usiku, wakati amna mtu akiwepo kuona kinachotokea, alikuwa akitoa chombo nje kwake na kutupa maji hayo machafu.
Siku moja, Hasan (Rahimahullah) alipokuwa mgonjwa, jirani yake Mkristo alikuja kumtembelea. Alipoingia nyumbani kwa Hasan (Rahimahullah) na kuona chombo kimejaa na maji machafu ya chooni, alitambua kwamba yalikuwa yanatoka nyumbani kwake.
Kwa aibu aliuliza, “Haya maji machafu yana vuja kwa muda gani?” Hasan Basri (Rahimahullah) alijibu, “Kwa miaka ishirini.”
Aliposikia hivyo, jirani huyo alishangazwa sana na tabia ya Hasan Basri (Rahimahullah) hadi kwamba alivua vazi lake la Kikristo na akasilimu mara moja.
Maonyo Ndani Ya Hadith Kwa Wale Wanaowadhulumu Majirani Zao
Kama jinsi kuna msisitizo mkubwa katika hadith kwa ajili ya kutimiza haki za jirani, hivyo hivyo kuna maonyo makali kuhusu kusababisha usumbufu kwa jirani.
Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiyallahu anhu) kwamba Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) amesema: “Mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala) na Siku ya Qiyaamah, asimletee usumbufu jirani yake.”
Katika hadithi nyingine imepokewa kwamba Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) alirudia kauli ifuatayo mara tatu: “Naapa kwa jina la Allah Ta’ala, mtu kama huyo kamwe hawezi kuwa muumini kamili.
Swahaba mmoja akauliza, “Ewe Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam)! Unamkusudia nani? Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akasema: “Yule ambaye jirani yake haepushwi na shari na mauvu yake.”
Wakati mmoja, mtu mmoja alikuja kwa Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akasema: “Ewe Rasulullah! Kuna mwanamke fulani ambaye anajulikana sana kwa kuswali swala nyingi za nafl, kutoa sadaka na kufunga nafl, lakini anamletea madhara jirani zake.”
Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akasema: “Atakuwa motoni (yaani ataadhibiwa na Mwenyezi Mungu kwa kuwafanyia ubaya jirani zake).
Kisha yule mtu akasema: “Ewe Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) namjua mwanamke mwingine ambaye hashiriki katika swalah nyingi za nafli, wala hafungi nafli nyingi, wala hatoi sadaka nyingi, bali anawagawia majirani zake jibini (cheese) kwa njia ya sadaqah na wala hawadhuru jirani zake (yaani hutimiza haki zote za jirani zake)
Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akasema: “Atakuwa katika Jannah (yaani kwa sababu ya kuwatendea wema majirani zake, atalipwa Jannah).”
Kutokana na Hadith hizo hapo juu, tunaelewa kwamba Uislamu umetoa umuhimu mkubwa katika haki za majirani.
Kwa hivyo, tunapaswa kujaribu wakati wote, kutimiza haki za majirani na tunapaswa kuhakikisha kwamba hatuwasababishii usumbufu au madhara yoyote wakati wowote.
Allah Ta’ala Atujaalie tawfeeq ya kutimiza haki za majirani zetu pamoja na haki tunazodaiwa na waja wengine wa Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala).
Alislaam Juhudi za Kuleta uislam ndani ya maisha yetu