Kununua Ardhi kwa ajili ya Upanuzi wa Masjid-ul-Haram

Wakati mmoja, Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) alimwendea mtu fulani huko Makka Mukarramah na kumwambia, “Ewe fulani! Je, utaniuzia nyumba yako, ili nipanue eneo la msikiti karibu na Al-Ka’ba, na kwa malipo ya tendo hili jema, nitakudhaminia kasri katika Jannah (yaani zaidi ya pesa utakazopokea ya nyumba hii)?”

Yule mtu akajibu, “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu (sallallahu ‘alaihi wasallam)! Wallahi, hii ndiyo nyumba pekee niliyo nayo! Nikikuuzia nyumba, sitokuwa na chochote hapa makka mukarramah kuwahifadhi watoto wangu na mimi mwenyewe.”

Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) akamhimiza tena mtu huyo akisema, “Pamoja na hayo uliyoyataja, niuzie nyumba yako, ili nipanue eneo la msikiti karibu na Ka’ba, na kwa malipo ya kitendo hiki kizuri, nitakudhaminia kasri katika Jannah.” Yule mtu akajibu, “Wallahi! Sina nia ya kuuza nyumba yangu.”

Uthmaan (radhiya allaahu ‘anhu) baada ya hapo alikuja kufahamu yaliyotokea. Hivyo akaenda kwa mtu huo, ambaye alikuwa rafiki yake toka zama za kabla ya Uislamu, na akasema, “Ewe fulani! Nimekuja kujua kama Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) alikusudia kununua nyumba yako, kupanua eneo la msikiti karibu na Ka’bah, na kwa malipo ya kitendo hiki kizuri, alikuhakikishia kasri huko Jannah, na ukakataa ombi hili.” Huyo mtu akajibu, “Ndiyo, nilikataa.”

Uthmaan (radhiya allaahu ‘anhu) kisha akaendelea kumhimiza kuiuza nyumba yake, mpaka hatimaye alikubali na Uthmaan (radhiya allaahu ‘anhu) kisha akainunua kutoka kwake kwa Dinari 10,000 (fedha za dhahabu).

Kisha Uthmaan (radhiya allaahu ‘anhu) akaelekea kwa Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) na kusema, “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu (sallallahu ‘alaihi wasallam)! Nilikuwa nimekuja kujua kwamba ulikusudia kununua nyumba ya fulani, kupanua eneo la msikiti karibu na Ka’bah, na ulikuwa umemhakikishia mwenye nyumba kasri huko Jannah. Sasa nyumba hiyo ni yangu, nimeinunua kutoka kwa mwenye nyumba, je, utaipokea kutoka kwangu bure na unihakikishie kasri katika jannah”?

Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) akajibu kwa kukubali na akaipokea nyumba hiyo kutoka kwa Uthmaan (radhiya allaahu ‘anhu), akimdhaminia kasri katika Jannah na kuwafanya maswahaabah (radhiyallahu ‘anhum) kuwa mashahidi kwa hilo.

About admin

Check Also

Mshale Wa Kwanza Kurushwa kwa Ajili Ya Uislamu

Sa’d (radhiya allaahu ‘anhu) alikuwa miongoni la kundi la Maswahabah ambao Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) …