
Abdullah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa ni kijana mdogo, akikuwa akichunga mbuzi za Uqbah bin Abi Mu’ait katika eneo la Makkah Mukarramah. Siku moja akiwa anachunga mbuzi, Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) walipita huku wakiwa wakiwakimbia wamushrikeen.
Kwa kuwa ilikuwa ni desturi ya Waarabu kuwakirimu waliokuwa safarini na maziwa, basi walipoona mbuzi, Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) walimuomba
wapewe maziwa.
Wakamwambia, “Ewe kijana! Una maziwa ya kutupa?” Akajibu, “Ndiyo, kuna maziwa, lakini mbuzi hawa ni amana chini ya ulinzi wangu, na sitaki kuwapeni maziwa.”
Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akamwambia: “Niletee mbuzi wa kike ambaye hajaza (yaani hana maziwa). Hivyo nikaleta mbuzi wa kike kwa Mtume (Sallallahu alaihi wasallam).
Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimshika mbuzi huyo mbele ya Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam). Kisha Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akaanza kupitisha mikono yake iliyobarikiwa juu ya chuchu zake (za mbuzi) huku akisoma sehemu ya Qur’an Majeed na kuomba dua kwa Allah Ta’ala ajalie maziwa. Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) akifanya hivyo, chuchu za mbuzi zilianza kujaa maziwa kimiujiza.
Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kisha akaleta jiwe lenye shimo kwa Mtume (Sallallahu alaihi wasallam), kisha akakamua maziwa ndani yake kwa kutumia lile jiwe kama chombo. Baada ya kumaliza kukamua maziwa, Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam), Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) na Abdullah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) wote walikunywa maziwa hayo.
Baada ya hapo, Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akaamuru chuchu za mbuzi huyo kurudi katika hali yake ya awali ya kutokuwa na maziwa yoyote, na mara moja ikarudi katika hali yake ya awali.
Baada ya kuushuhudia muujiza huu mbele ya macho yake, moyo wa Abdullah bin Mas’uud ulikuwa umezidiwa na mapenzi ya Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam). Baada ya siku chache, alikuja kwa Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) na akasilimu.
Wakati wa kusilimu, alimwambia Mtume (Sallallahu alaihi wasallam), “Nifundishe yale maneno uliyoyasoma wakati ulipomkamua mnyama ambaye hakuwa na maziwa kwenye chuchu zake.” Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) kisha akapitisha mkono wake uliobarikiwa juu ya kichwa chake na kusema:
يرحمك الله فإنك غليم معلم
“Allah Ta‘ala akurehemu. Wewe ni kijana ambaye utakuwa na kipaji kizuri baadaye katika uwanja wa elimu.” (Musnad Ahmad #3598)
Katika riwaya moja, imetajwa pia kwamba Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) alimuombea dua kwa Allah Ta‘ala ili amjaalie na baraka maalum. (Sahih Ibnu Hibbaan #6504, Munsnad Ahmad #4412, 3598 na Musnad Abu Ya’laa #5096)
Alislaam Juhudi za Kuleta uislam ndani ya maisha yetu