Siku moja, kundi la maQurraa (wale waliokuwa wataalamu wa kusoma Qur-aan Majeed) kutoka Basrah walimjia Abdullah bin Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) na kumwambia, “Kuna mchamungu mmoja anaishi katika eneo letu, ambaye mara nyingi hufunga na kutekeleza Swalah nyingi za Tahajjud. Yeye ni mchamungu sana kiasi kwamba kila mmoja wetu anatamani kufanana naye katika ibaadah. Amemwoza bintiye kwa mpwa wake, lakini kwa sababu ya umaskini, hawezi kumpa binti yake vitu atakavyohitaji kwa ajili ya nikaah yake.”
Abdullah bin Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) akawapeleka nyumbani kwake, na akachukua mifuko sita ya dinari (sarafu za dhahabu) kutoka kwenye sanduku, akawakabidhi, akiwaomba wampelekee yule mchamungu.
Walikuwa karibu kuondoka, pale Ibnu Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliposema, “Sidhani kama ni njia ya haki ya kumsaidia. Ikiwa tutampa pesa, atakuwa na shida sana katika kupanga vitu vyote vya nikaah ya binti yake, na wakati wake mwingi wa thamani utapotea katika kununua vitu. Ratiba yake ya ibaadah itavurugwa. Utajiri wa dunia hauna thamani ya kuweza kuvuruga mazingatio ya Muislamu mchamungu. Sio chini ya utu wetu sisi kumtumikia ndugu Muislamu. Tufanye mipango ya ndoa, tununue vitu vya nikaah na tumpe jirani yetu.”
MaQurraa walikubali hili, wakanunua vitu vyote vilivyohitajika, na wakamkabidhi yule mchamungu vitu hivyo. (Fazaa’il-ul-Sadaqaat [Kiingereza] 731,
Alislaam Juhudi za Kuleta uislam ndani ya maisha yetu