Nabi Isa (alaihis salaam)

Isa (‘alayhis salaam) ni Mtume wa Allah Ta‘ala na anahesabiwa miongoni mwa manabii wa daraja la juu. Allah Ta’ala alimteremshia Injili (Biblia) na akamjalia na Shari’ah. Yeye ndiye Nabii aliyetumwa duniani kabla ya Mtume (Sallallahu alaihi wasallam).

Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) amesema: “Manabii wote ni kama ndugu wa baba mmoja, mama zao wanatofautiana, na Dini yao ni moja (yaani wote wanaamini tauheed – umoja wa Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’ala), ingawa Shari’ah zao ni tofauti). Mimi ndiye mtu wa karibu sana wa Nabii Isa bin Maryam (‘alayhis salaam), kwa sababu hakuna Nabii baina yetu. Hakika Nabii Isa (‘alayhis salaam) atashuka.” (Musnad Ahmed #9270)

Allah Ta’ala alimtuma Nabii Isa (‘Alayhis Salaam) kwa Bani Israa’il, lakini hawakumuamini na wakamkataa. Walijaribu hata kumuua, lakini Allah Ta’ala akamlinda na akamnyanyua mbinguni akiwa hai. Hivi sasa, Nabii Isa (‘Alayhis Salaam) yupo hai mbinguni, na kabla ya Qiyaamah, Allah Ta’ala atamrudisha duniani.

Katika Hadith, Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) amesema, “Naapa kwa Yule ambaye maisha yangu yapo mkononi mwake! Nabii Isa (‘alayhis salaam)) atashuka kutoka mbinguni, na atatawala miongoni mwenu kama mtawala mwadilifu. Atauvunja msalaba na kuua nguruwe…” (Sahih Muslim #155)

Kushuka kwa Nabii Isa (‘alaihis salaam) – Dalili Kubwa ya Qiyaamah

Kuteremka kwa Nabii Isa (‘alayhis salaam) kutoka mbinguni kuja duniani inahesabiwa miongoni mwa alama kuu za Qiyaamah.

Katika Qur-aan Majeed, Allah Ta‘ala Anasema, “Na hakika yeye (Nabii Isa [alayhis salaam]) ni chanzo cha kupata elimu ya Saa ya Mwisho (yaani kushuka kwake ni dalili ya Qiyaamah), basi usiwe na shaka juu yake (Saa ya Mwisho ya Qiyaamah kutokea)… (Sura Zukhruf aya 61)

Katika Hadith moja, Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) ametaja, “Hakika Qiyaamah hakitotokea mpaka muone kabla yake ishara kuu kumi. Moshi (aina ya ukungu au moshi utakaoshuka duniani kutoka mbinguni kabla ya Qiyaamah ambapo Waislamu watapata homa na makafiri watapoteza fahamu), kutokea kwa Dajjaal, mnyama kujitokeza, kuchomoza kwa jua kutoka magharibi, kushuka kwa Nabii Isa (‘alaihis salaam), Ya’juuj na Ma’juuj kutokea, sehemu tatu kuu duniani kuzama; kuzama mashariki, kuzama magharibi na kuzama katika Bara la Arabu. Alama ya mwisho ni moto utakaotokea Yemen na kuwapeleka watu kwenye uwanja wa kufufuliwa (Syria). (Sahih Muslim #2901)

Imani ya Ahlus Sunnah wal Jamaa’ah kuhusiana na Nabi Isa (‘alaihis salaam) kumuua Dajjaal.

Moja ya sababu kuu za Nabii Isa (‘alayhis salaam) kurudishwa duniani kabla ya Qiyaamah itakuwa ni kumuua Dajjaal. Nabii Isa (‘alaihis salaam) kumuua Dajjaal ni miongoni mwa imani za kimsingi za Ahlus Sunnah wal Jamaa’ah.

Allaamah Qadhi Iyaadh (rahimahullah) ametaja kuwa Nabii Isa (‘alaihis salaam) kurejea duniani kumuua Dajjaal ni miongoni mwa imani za kimsingi za Ahlus Sunnah wal Jamaa’ah. Muhadditheen, Fuqahaa na Ulamaa wa Aqaa’id wote wanakubali imani hii.

About admin

Check Also

Mahdi (Radhiya Allaahu ‘anhu)

Kuja kwa Mahdi (Radhiya Allaahu ‘anhu) ni dalili ya kwanza kati ya alama kuu zitakazojitokeza …