Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akimwomba Abdullah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) amsomee Quraan Majeed.

Wakati mmoja, Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) alikuja kwa kabila la Bani Zafar (kabila la Answaar). Akiwa amekaa juu ya mimbar akiwahutubia, alimwambia Abdullah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu), “Nisomee Qur-aan.”

Kwa unyenyekevu mkubwa, Abdullah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimwambia Mtume (Sallallahu alaihi wasallam), “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, nikusomee wewe Qur’an Majeed wakati Qur’an imeshushwa kwako?”

Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akasema: “Natamani kusikia ikisomwa na yoyote kasoro mimi.”

Abdullah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) kisha akaanza kusoma Sura Nisaa, huku Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akisikiliza kwa makini kisomo chake. Alipofika aya ya arobaini na moja ya Sura Nisaa:

فَكَيْفَ إِذَا جِئْنَا مِن كُلِّ أُمَّةٍ بِشَهِيدٍ وَجِئْنَا بِكَ عَلَىٰ هَٰؤُلَاءِ شَهِيدًا ‎﴿٤١﴾‏

“Basi itakuwaje tutakapowatoa katika kila umma shahidi, na tukakuleta wewe (ewe Muhammad) kuwa shahidi juu ya watu hawa?”

Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akamwambia: “Unaweza kuacha kusoma sasa.”

Wakati Abdullah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipotazama juu ya uso wa baraka wa Mtume (Sallallahu alaihi wasallam), alikuta macho ya Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) yamejazwa na machozi (kutokana na utukufu uliotukuka na nafasi ya juu ambayo Mwenyezi Mungu atamjaalia Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) siku ya Qiyaamah, kama ilivyotajwa katika aya hapo juu). (Sahih Bukhaari #5055, Fathul Baari 99/9)

About admin