Tafseer Ya Surah Dhuha

بِسْمِ ٱللَّـهِ ٱلرَّحْمَـٰنِ ٱلرَّحِيمِ

وَالضُّحٰى ﴿١﴾ وَالَّيْلِ إِذَا سَجٰى ﴿٢﴾ مَا وَدَّعَكَ رَبُّكَ وَمَا قَلٰى ﴿٣﴾ وَلَلْـاخِرَةُ خَيْرٌ لَّكَ مِنَ الْاُولٰى ﴿٤﴾ وَلَسَوْفَ يُعْطِيكَ رَبُّكَ فَتَرْضٰى ﴿٥﴾ اَلَمْ يَجِدْكَ يَتِيمًا فَـاوٰى ﴿٦﴾ وَوَجَدَكَ ضَآلًّا فَهَدٰى ﴿٧﴾ وَوَجَدَكَ عَآئِلًا فَاَغْنٰى ﴿٨﴾ فَاَمَّا الْيَتِيمَ فَلَا تَقْهَرْ ﴿٩﴾ وَاَمَّا السَّآئِلَ فَلَا تَنْهَرْ ﴿١٠﴾ وَاَمَّا بِنِعْمَةِ رَبِّكَ فَحَدِّثْ ﴿١١﴾

Naapa kwa nuru ya asubuhi, na kwa usiku unapoingia. Mola wako hakukuacha wala hakukukasirikia. Na hakika Akhera ni bora kwako zaidi kuliko ya sasa (maisha). Na hivi karibuni mola wako atakupa neema (nyingi) utakazoziridhia. Kwani hakukukuta wewe ni yatima, kisha akakupa sehemu yakuishi? Na hakukukuta Katika hali ya kutokujua, kisha akakuonyesheni njia? Na hakukukuta wewe mhitaji, kisha akakuruzuku na mali? Basi yatima usimuoneshe ukali; na kuhusu mwombaji, basi usimnyime; na ama fadhila za mola wako, basi endelea kuzitaja.

Katika siku za mwanzo za Uislamu, wakati Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) alikuwa Makkah Mukarramah, hakupokea wahi kutoka kwa Allah subhaana wata’ala kwa siku chache. Kutokana na hili, baadhi ya makafiri walianza kumdhihaki Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) wakisema: “Mola wako amekuchukia, kwa hiyo hakuletei wahi tena.”

Aina hizi za dhihaka na matamshi ya kuumiza bila shaka yatasababisha maumivu kwa mtu. Hata hivyo, Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) alikuwa na yakini kamili kwamba Allah subhaana wata’ala yupo pamoja naye na hakumuacha wala Hakumkasirikia. Kwa hivyo, kama faraja kwa Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) na kama fundisho kwa Ummah wake, Allah subhaana wata’ala aliteremsha surah hii, ambamo Anaeleza kwamba wale ambao wamejitolea kwa ajili ya Allah subhaana wata’ala na wanapitia aina fulani ya ugumu wa maisha, basi hawapaswi kuhisi hivyo kama hata dakika moja, kwamba Allah subhaana wata’ala amewaacha au kwamba Allah subhaana wata’ala amewachukia. Kwa hiyo, Allah subhaana wata’ala anaianza surah hii kwa Aya ifuatayo:

وَالضُّحٰى ﴿١﴾ وَالَّيْلِ إِذَا سَجٰى ﴿٢﴾ مَا وَدَّعَكَ رَبُّكَ وَمَا قَلٰى ﴿٣﴾

Naapa kwa nuru ya asubuhi, na kwa usiku unapoingia. Mola wako hakukuacha wala hakukasirikia.

Katika Aayah hii, Allah subhaana wata’ala anaapa kwa nuru ya asubuhi na kwa usiku unapoingia. Katika hili ni dalili kwamba mwanadamu atapitia Hali tofauti, na vile vile baada ya giza la usiku huja nuru ya mchana, vivyo hivyo, baada ya kipindi cha shida kitakuja kipindi cha urahisi.

Kwa hivyo, mtu anapopitia hali ya shida, asihisi kuwa Allah amemkasirikia au amemuacha. Bali mtu anatakiwa kurejea kwa Allah subhaana wata’ala na kubaki kuwa mtiifu kwake kila wakati.

وَلَلْـاخِرَةُ خَيْرٌ لَّكَ مِنَ الْاُولٰى

Na hakika Akhera ni bora kwako zaidi kuliko maisha ya sasa.

Maana ya Aayah hii ni kwamba maisha ya Akhera ni bora kwa Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) kuliko maisha ya dunia. Vile vile, inaweza pia kumaanisha kwamba kila dakika itakayokuja katika maisha ya Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) itakuwa bora kuliko dakika zilizotangulia.

Hii inamaanisha ya Kwamba hii ni bashara maalum kwa Nabii wa Allah (sallallahu ‘alaihi wasallam) kwamba Allah Ta’ala ataendelea kumbariki na kumzidishia elimu, utambuzi Wake maalum na kupata ukaribu zaidi kwa Allah Ta’ala. Katika hili, kuna dalili pia inayoonesha uboreshaji wa rizqi, heshima na uongozi wake.

Lakini, kama vile Aya hii inaonyesha  bashara kwa Nabii wa Allah (sallallahu ‘alaihi wasallam), pia ni njia ya kutia moyo kwa kila muumini mwadilifu kubaki na matumaini ya rehema za Allah Ta’ala.

Kama Muumini ataendelea kuwa na dhamira ya kufuata sunna mubaraka za Rasulullah (sallallaahu alaihi wasallam) katika maisha yake, na akajitahidi kupata ukaribu maalum wa Allah Ta’ala, basi kila dakika inayokuja itakuwa bora kwake kuliko muda uliyopita, Allah Ta’ala ataendelea kumpa mafanikio na maendeleo katika ufahamu wake, ujuzi, heshima na mengineyo.

Kwa hivyo, anapopatwa na dhiki au shida yoyote basi asihuzunike na kupoteza matumaini, bali anatakiwa arejee kwa Allah Ta’ala na awe na matumaini katika rehema zake.

وَ  لَسَوفَ یُعْطِيْکَ رَبُّکَ فَتَرضٰی

Na hivi karibuni mola wako atakupa neema nyingi ili uridhike.

Katika aya hii, Allah Ta’ala anamfahamisha kipenzi chake Nabii wa Allah (sallallaahu alaihi wasallam) kwamba Yeye atatimiza mahitaji yake na matamanio yake mpaka yeye (Sallallahu alaihi wasallam) atakaporidhika. Miongoni mwa matakwa na matamanio ya Mtume ( sallallaahu alaihi wasallam) ni kwamba Uislamu uendelee na kuenea duniani kote na kwamba Waislamu wapate ushindi dhidi ya maadui yao. Haya yote yamejumuishwa miongoni mwa neema maalum alizo ahidi Allah Ta’ala.

Imetajwa katika Hadith kwamba ilipoteremka Aya hii, Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) alisema:

إِذًا وَاللَّهِ لَا أَرْضَى وَوَاحِدٌ مِنْ أُمَّتِي فِي النَّارِ

‘Sitafurahi na wakati hata mtu mmoja katika ummah wangu yupo ndani mwa Moto wa Jahannum’.

Kutokana na hili, tunaweza kuona mapenzi makubwa aliyokuwa nayo Rasulullah (sallallaahu alaihi wasallam) kwa umma wake, ambapo hatapata raha na furaha kwa hata mtu mmoja katika umma wake anaungua katika Jahannum. Kwa maneno mengine, Rasulullah (Sallallaahu alaihi wasallam) ana mapenzi makubwa na ummah kiasi kwamba anatamani kumuona kila mtu wa ummah wake akiingia kwenye Jannah. Kwa hivyo, Siku ya Qiyaamah, Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) ataomba mbele ya Allah Ta‘ala ili kila mtu katika Umma wake aingie Jannah.

Rasulullah (Sallallaahu alaihi wasallam) ana mapenzi makubwa na umma wake. Upendo wa Mtume (Sallallaahu alaihi wasallam) kwa kila mtu ndani mwa ummah wake unatakiwa iwe kwamba sisi pia tuonyeshe uaminifu na utiifu wetu kwake wakati wote. Katika suala hili, mambo mawili ni muhimu sana.

Kwanza ni kwamba tushikamane na sunna mubaraka zake katika nyanja zote za maisha yetu na tujiepushe kabisa na yale yote ambayo hayampendezi na aliyotukataza nayo. Kwa namna hii, kwa kushikamana kikamilifu na sunna mubaraka zake, tutakuwa tunaonyesha shukrani zetu kamili kwake.

Pili ni kwamba tunamswalia mtume (sallallaahu alaihi wasallam) kwa wingi, hasa siku za Ijumaa. Hii italeta furaha kwenye moyo wa mubaarak wa Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam).

اَلَمْ يَجِدْكَ يَتِيمًا فَـاوٰى

Kwani hakukukuta yatima, kisha akakupa sehemu ya kuishi?

Rasulullah (Sallallaahu alaihi wasallam) alikuwa yatima tangu mwanzo wa uhai wake, kama baba yake alivyofariki kabla ya kuzaliwa kwake. Mama yake kisha alifariki akiwa na umri wa miaka sita, na baada ya hapo babu yake, Abdul Muttalib, alimtunza hadi kufikia umri wa miaka minane, na baada ya hapo, Abu Taalib alimtunza mpaka alipokaribia umri wa miaka hamsini.

Kuhusu Abu Taalib, basi alimuonyesha Rasulullah (Sallallaahu alaihi wasallam) mapenzi ambayo hata baba asingeyaonyesha. Vile vile, kila mtu aliyeingia katika maisha ya Mtume (Sallallaahu alaihi wasallam) alimuonesha mapenzi ambayo yalikuwa yanazidi sana mapenzi ya baba au ya wazazi. Basi hili lilitoka kwa Allah Ta’ala, kwamba kila aliyemuona alimpenda na akakuza mapenzi mazito kwake.

وَوَجَدَكَ ضَآلًّا فَهَدٰى

Na hakukukuta wewe katika hali ya kutokujuwa, kisha akakuonyesha njia?

Kabla ya utume, Rasulullah (Sallallaahu alaihi wasallam) alikuwa hajui undani wa njia ya Dini. Kwa hivyo, Allah Ta’ala Akambariki kwa utume, akamfundisha undani wa Dini nzima na akamuonyesha njia ambayo atawaongoza watu kwa Allah Ta’ala.

وَوَجَدَكَ عَآئِلًا فَاَغْنٰى

Na hakukukuta wewe ni muhitaji, kisha akakuruzuku na mali.

Katika Aya hii, Allah Ta’ala anazungumza na Mtume (Sallallaahu alaihi wasallam), akimkumbusha neema zake juu yake, pale alipolelewa yatima, hakuwa na mali; kisha Allah Ta’ala akambariki na mali.

فَاَمَّا الْيَتِيمَ فَلَا تَقْهَرْ

Basi yatima usimfanyie ukali.

Rasulullah (sallallahu alaihi wasallam) aliishi maisha ya kiyatima na alijua hisia na mawazo zinazopita katika akili na moyo wa yatima. Yatima ni kwamba kwa ujumla hana mtu wa kuonyeshwa upendo na wema kwake. Kwa hiyo, Allah Ta’ala ameahidi malipo makubwa kwa wale wanaomlea yatima. Hadithi inasema kuwa nyumba bora ni ile nyumba ambayo yatima anaheshimiwa na kutunzwa vizuri, na nyumba mbaya zaidi ni ile nyumba ambayo yatima anafanyiwa ukatili, kudharauliwa na kutotendewa wema. Kwa hivyo, katika Aaya hii, Allah Ta’ala anamwamuru Nabii (sallallahu ‘alaihi wasallam) na ummah kuwatendea wema na huruma mayatima na kutowafanyia ukali.

وَاَمَّا السَّائِلَ فَلَا تَنْهَرْ

Na wala muombaji basi usimzuie.

Katika aya hii, Allah Ta’ala anamwambia Nabii (Sallallahu ‘alaihi wasallam) kwamba akikujieni mwombaji, basi msimzuie. Kwa maneno mengine, unapaswa kuwa mkarimu na kumjali. Kwa njia hii, ummah wako utakuiga wewe na kuwa na mazingatio kwa masikini na mafukara.

وَاَمَّا بِنِعْمَةِ رَبِّكَ فَحَدِّثْ

Na fadhila za Mola wako, basi zidi kuzitangaza.

Katika aya hii, Allah Ta’ala anazungumza na Nabii (Sallallahu ‘alaihi wasallam) na kumwamrisha azungumze juu ya neema ambazo Allah Ta’ala amemneemesha. Kwa hiyo, kutokana na aya hii, tunapata kujua kwamba kutaja neema ambazo Allah Ta’ala amembariki nazo mtu mbele ya watu, kwa kumshukuru Allah Ta’ala, inajuzu, kwa sharti kwamba mtu asijifakhari au kuhusisha kuzipata kwake mafanikio yeye mwenyewe, lakini anayachukulia kama ni neema tupu ya Allah Ta’ala juu yake.

About admin

Check Also

Tafseer Ya Surah Ikhlaas

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ ‎﴿١﴾‏ اللَّهُ الصَّمَدُ ‎﴿٢﴾‏ لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ ‎﴿٣﴾‏ وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا …