Tafseer Ya Surah Quraish

لِإِيلفِ قُرَيْشٍ ‎﴿١﴾‏ اِلٰفِهِمْ رِحْلَةَ الشِّتَآءِ وَالصَّيْفِ ‎﴿٢﴾‏ فَلْيَعْبُدُوا۟ رَبَّ هٰذَا الْبَيْتِ ‎﴿٣﴾‏ الَّذِىٓ أَطْعَمَهُم مِّن جُوْعٍ وَاٰمَنَهُمْ مِّنْ خَوْفِۭ ‎﴿٤﴾‏

Kwa ajili ya usalama ya Maquraishi, usalama wanaoufurahia katika safari zao katika miezi ya za baridi na miezi za joto. Wamuabudu Mola wa Nyumba Takatifu (Ka’aba), ambaye amewaruzuku chakula wasipate njaa na anawalinda na khofu.

Katika zama za kabla ya Uislamu, ujambazi, mauaji na vita vya ndani vilikuwa vya kawaida na vimejaa miongoni mwa makabila katika ardhi ya wa arabu. Kwa hiyo, walipokuwa wakisafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine, watu walikuwa na hofu ya mara kwa mara ya kushambuliwa na adui zao au kutekwa njiani na majambazi.

Lakini ilipokuja kwenye kabila la Maquraish, walipewa heshima kubwa zaidi kutoka makabila yote yaliyokuwa yanaishi warabuni kwa sababu ya nafasi yao ya juu ya kuwa walinzi wa Ka’bah Takatifu. Watu waliiheshimu Ka’bah Takatifu na walezi wa Ka’bah. Kwa hiyo, watu hawakuingilia misafara ya biashara ya Maquraishi na wakawaruhusu wapite kwa uhuru na usalama katika wakati ambapo misafara mingine ilikuwa ikitekwa, kuibiwa. Kwa hivyo, misafara yao ilikuwa ikienda kwa uhuru kwenda Yemen wakati wa majira ya baridi kali, na kuelekea Shaam wakati wa joto, bila ya kupata khofu yoyote, wakirudi na aina zote za mazao, chakula na mahitaji mengine ambayo watu wa Makka Mukarramah walihitaji.

Kimsingi, Ka’bah Takatifu ilikuwa sababu kuu ya usalama wa Maquraish na ustawi wao wa kiuchumi.

اِلٰفِهِمْ رِحْلَةَ الشِّتَآءِ وَالصَّيْفِ ‎﴿٢﴾

Kwa ajili ya usalama ya Maquraishi, usalama wanaoufurahia katika safari zao katika miezi za baridi na miezi za joto

Katika surah hii, Allah Ta‘ala anawakumbusha Maquraish juu ya neema hizi mbili maalum za Allah Ta’ala juu yao; fadhila ya usalama na fadhila ya ustawi. Baada ya kuwafahamisha juu ya fadhila hizi mbili, Allah Ta’ala anawaamrisha kuwa wamtii Yeye pekee na wasimwabudu yoyote mwengine.

Kutokana na hili, tunaelewa pia kwamba Maquraishi wamebarikiwa na heshima ya ziada kutoka kwa Allah Ta’ala ikilinganishwa na wengine. Imepokewa katika Hadith kwamba Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) amesema: “Kutoka katika watoto wa Ismaa’eel (‘alaihis salaam), Allah Ta’ala amewachagua Banu Kinaanah, na katika Banu Kinaanah, Allah Ta’ala Amewachagua. Maquraishi, na katika Maquraishi, Allah Ta’ala aliwachagua Banu Haashim, na katika Banu Haashim, Allah Ta’ala alinichagua mimi.”

Hivyo, Maquraishi wamepewa heshima kubwa na Allah Ta’ala Mwenyewe. Kwa ujumla, heshima hii hupatikana kupitia uamuzi wa Mwenyezi Mungu subhaanahu wata’aala. Mtu hawezi kuuliza swali, “Kwa nini Maquraishi walipewa nafasi ya juu zaidi ikilinganishwa na wengine?” Kwa sababu hii ni fadhila ya Allah Ta’ala, na humpa fadhila zake amtakaye yeye.

Vile vile, sababu ya wazi ya Maquraishi kupewa nafasi hii ya juu ikilinganishwa na wengine ni kwamba walikuwa na sifa nyingi kubwa na utukufu kama vile uaminifu, kuonyesha shukrani, kuwachunga watu na kuwasaidia wanyonge na wanaodhulumiwa. Sifa hizi tukufu na maadili ya kusifiwa yalikuwa ya kawaida miongoni mwa Maquraishi. Kwa hivyo, Allah Ta’ala alikuwa amewachagua kuwa walinzi wa nyumba Yake.

فَلْيَعْبُدُوا۟ رَبَّ هٰذَا الْبَيْتِ ‎﴿٣﴾ الَّذِىٓ أَطْعَمَهُم مِّن جُوْعٍ وَاٰمَنَهُمْ مِّنْ خَوْفِۭ ‎﴿٤﴾‏

Wamuabudu Mola wa Nyumba Takatifu (Ka’aba), ambaye amewaruzuku chakula wasipate njaa na anawalinda na khofu.

Katika surah hii, Allah Ta’ala anaonyesha umma wa Nabi (Sallallahu ‘alaihi wasallam) njia ya kupata neema yake maalum.

Njia ya kupata neema maalum ya Allah Ta’ala ni kuonyesha utiifu kwa Allah Ta’ala na kumshukuru. Mtu anapokuwa mtiifu kwa Allah Ta‘ala na akaonyesha shukurani, Allah Ta’ala humbariki kwa neema mbili kubwa.

Neema ya kwanza ni kwamba Allah Ta’ala humneemesha na rizki za halali na humkinga na njaa. Vile vile Allah Ta’ala atamruzuku kwa wingi katika mali na rizki yake.

Neema ya pili ni kwamba Allah Ta’ala atamjalia usalama katika maisha yake na mali yake.

Katika aya nyingine ya Qur-aan Takatifu, Allah Ta’ala anataja mfano ambapo umma ulibarikiwa na kila aina ya neema kutoka upande wake.

وَضَرَبَ اللَّهُ مَثَلًا قَرْيَةً كَانَتْ آمِنَةً مُّطْمَئِنَّةً يَأْتِيهَا رِزْقُهَا رَغَدًا مِّن كُلِّ مَكَانٍ

Na Allah Ta’ala anatoa mfano: Mji uliokuwa na usalama, na rizki yake inaufikia kwa wingi kutoka kwa kila mahali.

Walibarikiwa na usalama, mali, n.k, lakini pale walipovunja uaminifu wao na Allah Ta’ala na kukosa shukurani kwa neema zake, Allah Ta’ala alibadilisha hali zao za dunia kutoka kwenye maendeleo na kuwa kwenye ufukara na kutoka kwenye hali ya usalama kufikia kwenye hali ya hofu na hatari.

فَكَفَرَتْ بِأَنْعُمِ اللَّهِ فَأَذَاقَهَا اللَّهُ لِبَاسَ الْجُوعِ وَالْخَوْفِ بِمَا كَانُوا يَصْنَعُونَ

Lakini (watu wa mji) walizikanusha neema za Allah Ta’ala. Basi Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) akaionjesha na njaa na hofu (ilioifunika) kama nguo, kuwa ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyatenda.

“Njaa na hofu iliyowafunika kama nguo” iliyotajwa katika aya hii ina maana kwamba njaa na uwoga ulikuwa mkubwa sana kiasi kwamba ilikuwa kama vile imewavisha na kuwafunika kuanzia kichwani hadi miguuni.

Kwa hivyo, tunaelewa kwamba njia ya kufurahia neema za Allah Taala na njia ya kuziweka neema za Allah Ta’ala salama na kuzilinda zisipokonywe ni kuwa mtiifu kwa Allah Taala na kuonyesha shukurani na uaminifu kwa Allah Taala kwa fadhila zake kila wakati.

Imaam Jazaree (rahimahullah), imaam mashuhuri wa qiraa’ah, anasema kwamba wakati wa hofu, inapendekezwa kusoma Sura ya Quraish.

Katika Tafseer ya Mazhari, Qaari Thanaaullah (rahimahullah) anasema, “Sheikh wangu, Mirza Mazhar Sahib (rahimahullah), alikuwa ameniusia kwamba pindi mtu anapoingiliwa na hofu na uwoga, basi asome surah hii.” Qaari Thanaaullah (rahimahullah) anaendelea kusema, “Nilifanya zoezi hili na nikaona kuwa ni lenye faida nyingi.”

About admin

Check Also

Tafseer Ya Surah Lahab

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ تَبَّتْ يَدَا أَبِي لَهَبٍ وَتَبَّ ‎﴿١﴾‏ مَا أَغْنَىٰ عَنْهُ مَالُهُ وَمَا كَسَبَ ‎﴿٢﴾‏ سَيَصْلَىٰ نَارًا …