Tafseer Ya Surah Feel

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِأَصْحَابِ الْفِيلِ ‎﴿١﴾‏ أَلَمْ يَجْعَلْ كَيْدَهُمْ فِي تَضْلِيلٍ ‎﴿٢﴾‏ وَأَرْسَلَ عَلَيْهِمْ طَيْرًا أَبَابِيلَ ‎﴿٣﴾‏ تَرْمِيهِم بِحِجَارَةٍ مِّن سِجِّيلٍ ‎﴿٤﴾‏ فَجَعَلَهُمْ كَعَصْفٍ مَّأْكُولٍ ‎﴿٥﴾‏

Je, Hukuona jinsi Mola wako alivyowafanyia watu wa tembo? Je! Hakufanya mipango yao ya khiana kuharibika? Na akawapelekea ndege kwa makundi, Wakiwapiga na mawe ya udongo wa Motoni, Na hivyo akawafanya kama majani yaliyoliwa.

Tukio la watu wa tembo lilitokea takriban siku hamsini na tano kabla ya kuzaliwa kwa Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam). Surah nzima ya Qur-aan Takatifu imetolewa kwa ajili ya tukio hili, ambayo maelezo yake yameandikwa katika vitabu vya Tafsiir, Hadith na Seerah.

Tukio la watu wa tembo kwa hakika lilikuwa ni tamko la Allah Ta’ala na ishara ya busara inayoashiria ujio wa karibu wa muhuri wa Mitume, Mtume wa Mwisho, Muhammad (Sallallahu ‘alaihi wasallam). Ulinzi ambao ulipanuliwa kwa Maquraishi ulitokana kwa sababu mjumbe wa mwisho, ambaye alikuwa karibu kukanyaga ardhi hii, angetoka katika kabila hili hili (Maquraishi). Vinginevyo kama upande wa imani, Wa Falme wa Abyssinia na Yemen walikuwa bora kuliko Maquraishi wa Makka Mukarramah, kwa sababu wao walikuwa watu wa kitabu wakati Maquraishi walikuwa wakiabudu masanamu.

Mu’jizah na Irhaas

Kitendo cha muujiza kinachodhihirika mikononi mwa Mtume baada ya kupewa utume kinaitwa Mu’jizah. Na pia tukio la ajabu linalotokea mikononi mwa Mtume kabla ya utume linajulikana kama Irhaas. Vile vile, alama inayodhihirisha kuja kwa Nabii pia inajulikana kama irhaas. Kiuhalisi, neno irhaas maana yake ni msingi. Kwa hiyo, matukio hayo ya ajabu yaliunda msingi wa kutangaza ujio wa utume.

Abraha alianzisha mashambulizi kwa watu wa Makkah Mukarramah na maangamizi yake yaliyofuata yalitokea katika mwezi wa Muharram kabla ya kuzaliwa kwa Nabii (Sallallahu ‘alaihi wasallam).

Maelezo mafupi ya tukio la watu wa tembo

Abraha alikuwa mkuu wa mkoa wa Yemen aliyechaguliwa na Najaashi (Negus). Alipowaona Waarabu wakisafiri kutoka sehemu mbali mbali kwenda Makka Mukarramah kufanya Tawaaf ya Baitullah, Abraha akaingizwa na chuki na wivu. Kwa hiyo, aliamua kusimamisha kanisa la kipekee na tukufu kwa jina la Ukristo. Lengo lake lilikuwa kulifanya kanisa lake kuwa kitovu cha hija badala ya Ka’bah. Hivyo, aliendelea na kazi yake na akasimamisha kanisa zuri huko San’aa, mji mkuu wa Yemen. Kisha akaanza kuwazuia watu wa Yemen kuzuru Makka Mukarramah na akawaamuru wachukue kanisa lake kama mbadala wa Ka’bah sahili. Haafidh Ibnu Kathir (rahimahullah) aliripoti kwamba Abraha alipata mengi ya mapambo ya thamani ili kupamba kanisa kutoka kwenye kasri la Bilqis.

Habari za kanisa lililojengwa upya zilipowafikia Waarabu, walikasirika. Mtu wa kabila la Kinaanah, akiongozwa na hisia na jazba, alitoka kwa nia ya kumfedhehesha Abraha. Alikuja karibu na kanisa la Abraha na kujisaidia katika maeneo ya karibu yake. Baadhi ya riwaya zinataja kwamba vijana wachache wa Kiarabu waliwasha moto karibu na kanisa. Upepo mkali ulipeperusha makaa ya moto hadi kwenye muundo wa mbao na kusababisha kuwashwa. Sio mbali na hili tukio Abraha alipata habari ya hili, na kwa hasira, aliapa kuibomoa Ka’aba Tukufu na kuisambaratisha chini.

Kwa nia hii ovu, alisonga mbele kuelekea Makka Mukarramah akiwa na jeshi lenye nguvu na la kutisha la watu elfu sitini wenye nguvu. Jeshi la Abraha pia liliambatana na kundi la tembo waliotumwa na Negus. Wakiwa njiani kuelekea Makka, yale makabila ambayo yalijaribu kuweka upinzani walishindwa na nguvu za upanga wa Abraha. Wakati jeshi la Abraha lilipofika Mughammas, mahali karibu na Makka Mukarramah, Abraha alituma kikosi cha wapanda farasi chini ya uongozi wa Aswad Ibn Maqsud kwenda kupora mifugo ya watu wa Makka. Miongoni mwa wanyama hao walikuwa ngamia mia mbili za Abdul-Muttalib, babu yake Rasulullah (Sallallahu’alaihi wasallam). Abdul Muttalib alikuwa kiongozi wa Maquraish na mlinzi wa Ka’ba tukufu. Alipopata taarifa za nia mbaya za Abraha, Abdul Muttalib aliwakusanya Maquraishi na kuwahakikishia kwamba hapakuwa na haja ya wao kuogopa. Aliwakumbusha kwamba Ka’aba Tukufu ni nyumba tukufu ya Allah Ta’ala na kwamba hakika Allah Ta’ala atailinda nyumba yake. Hapo hapo akatoa maelekezo wa mji mtakatifu wa Makka kuhamishwa.

Kabla ya kuondoka, akifuatana na wanawe na viongozi wachache wa Maquraishi, Abdul Muttalib alitoka kwenda kukutana na Abraha. Mara tu macho ya Abraha yalipoangukia kwa Abdul Muttalib, alishuka kutoka kwenye kiti chake cha ufalme na kumkaribisha Abdul Muttalib kwa ukarimu na mapokezi ya heshima. Abdul Muttalib alijaliwa na uzuri wa ajabu, umashuhuri wa kipekee, utisho wa kushangaza na hadhi ya kuvutia. Mtu yoyote ambaye alikutana naye kwa mara ya kwanza alibaki akishangaa na kufurahishwa na ukufu wake. Abraha alitambua vivyo hivyo kwenye mkutano wao wa kwanza.

Wakati wa mazungumzo yao, Abdul Muttalib alimwomba Abraha aachie ngamia zake ambazo zilikuwa zimetekwa na jeshi la Abraha. Abraha alishangazwa na ombi hili, akasema, “Inashangaza kuona kwamba hukutaja neno lolote kuhusu Ka’ba, ambayo ni kitovu cha Dini yako na Dini ya baba zako, lakini umeomba tu kurudishwa wa ngamia zako.” Abdul Muttalib akajibu kwa utulivu, “Mimi ndiye mwenye ngamia hivyo nimekuja kutafuta mali yangu. Ka’ba ina mmiliki ambaye hakika atailinda.” Abraha akajibu, “Inawezaje kuwa salama kutoka kwangu?” Abdul Muttalib akasema: “Hili ni jambo baina ya wewe na Yeye (Allah Ta’ala).” Muda wa ukimya ulifuata na Abraha alivutiwa na maneno mazito ya Abdul Muttalib. Kisha Abraha akaamuru kuachiliwa kwa ngamia mia mbili.

Baada ya kuwarudisha ngamia zake, Abdul Muttalib alirudi kwa watu wake na akawaamuru waondoke mara moja Makka. Kisha akaweka kiapo kutoa kafara ngamia mia mbili ili Ka’ba ibakie kulindwa. Kabla ya kuelekea milimani, Abdul-Muttalib alishikilia mlango wa Al-Ka’bah na akamuomba Allah Ta’ala kwa maneno yafuatayo:

لاهُمّ أن المرء يمــنع … رحله فامنع رحالك

“Ewe Mwenyezi Mungu! Mtu huitunza nyumba yake, Wewe utunze nyumba Yako.

وانصر على آل الصليــب … وعابديه اليوم آلك

Na uwasaidie watu wako kutoka na watu wa msalaba na waabudu wake.

لا يغلبن صليبهم … ومحالهم أبدًا محالك

Msalaba wao na vitimbi vyao kamwe haviwezi kushinda ulichopanga.

جروا جميع بلادهم … والفيل كي يسبوا عيالك

Waliburuta (na kuleta) majeshi yao yote na tembo zao ili kuwakamata wategemezi Wako.

عمدوا حماك بكيدهم … جهلًا وما رقبوا جلالك

Kwa kutojua, wamepanga njama ya kuharibu haram Yako, na wakashindwa kuzingatia ukuu Wako.”

Alipomaliza Du’a yake ya dhati, Abdul Muttalib, pamoja na masahaba zake, walipanda mlima, wakiiacha Makka tupu bila watu.

Asubuhi iliyofuata, Abraha alitayarisha askari wake na akamweka tembo wake Mahmood (kiongozi wa tembo) tayari kwa mashambulizi. Walipokuwa wakimuelekeza Mahmood kuelekea Makka Mukarramah, mtu mmoja kwa jina la Nufail bin Habib alimnong’oneza sikioni, “kaa chini Mahmood! Rudi kule ulikokuwa umetoka. Wewe uko katika nchi takatifu!” akalifungua sikio lake. Mara moja tembo alijisalimisha na kupiga magoti huku Nufail akiharakisha kwenda milimani. Watu walianza kumpiga tembo kwa fimbo za chuma lakini hakuweza kusonga. Ikiwa imeelekezwa Yemen au upande wowote ule, basi ilifanya haraka na kusonga mbele, lakini mara ilipogeuzwa kuelekea Makka, ilipiga magoti na kukataa kusogea.

Aliposonga mbele kuvunja Ka’ba, ghafla makundi makubwa ya ndege wadogo yalitokea kutoka ufukweni mwa bahari, kila mmoja akiwa amebeba kokoto tatu. Ukubwa wa kila kokoto ulifanana na saizi ya mbegu za mbaazi au dengu. Kila ndege alibeba kokoto mbili kwenye makucha yake na moja kwenye mdomo wake. Ndege kisha wakamimina kokoto hizi juu ya Abraha na jeshi lake, na mtu yoyote mnyonge ambaye kokoto hizi zingempiga hangeweza kuishi. Juu ya kila kokoto liliandikwa jina la yule ambaye iliamriwa kupigwa pamoja na jina la baba yake. Kwa uwezo wa Allah Ta’ala, kokoto hizi zilinyesha kwa haraka juu ya jeshi la Abraha kama maporomoko ya risasi za kuua. Kijiwe kingepiga kichwa kwa nguvu sana hadi kingeweza kutokea kutoka upande wa nyuma. Askari na tembo walianza kukimbia, kwa hofu, na wengi wao walikufa hapo hapo na wengine walikufa wakati wa kurudi. Kwa njia hii, jeshi ‘hodari’ la Abraha liliangamizwa kabisa na kufutiliwa mbali kutoka katika uso wa dunia.

Abraha baada ya kupigwa alikumbwa na ugonjwa hatari ambao ulieneza sumu mwilini mwake. Walipokuwa wakimbeba, mwili mzima ulimtoka ndui iliyotoka usaha na damu. Moja baada ya nyingine, viungo vyake vya mwili vilianza kugawanyika na kuanguka chini. Hatimaye, alipofika San’aa, kifua chake kilipasuka, na kumfanya afe kifo kibaya.

Allah Ta’ala anaeleza tukio zima katika aya zifuatazo za Qur’an:

أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِأَصْحَابِ الْفِيلِ ‎﴿١﴾‏ أَلَمْ يَجْعَلْ كَيْدَهُمْ فِي تَضْلِيلٍ ‎﴿٢﴾‏ وَأَرْسَلَ عَلَيْهِمْ طَيْرًا أَبَابِيلَ ‎﴿٣﴾‏ تَرْمِيهِم بِحِجَارَةٍ مِّن سِجِّيلٍ ‎﴿٤﴾‏ فَجَعَلَهُمْ كَعَصْفٍ مَّأْكُولٍ ‎﴿٥﴾‏

Mafunzo:

1) Wivu na husda ni ugonjwa wa uharibifu. Inasababisha ugomvi na mabishano. Mtu ambaye amemezwa na wivu huwa katika hali ya hasira mara kwa mara na hutafuta njia za kumshinda mtu mwingine. Ulikuwa ni wivu wa Abraha uliompelekea kujenga “Ka’bah mpinzani”, na hii ndiyo iliyopelekea kuangamizwa kwake.

2) Hasira humfanya mtu kupoteza fahamu, na kwa hasira hufanya maamuzi ambayo atajutia baadaye. Hivyo, tunaona kwamba uamuzi wa Abraha wa kuiharibu Ka’bah ulileta kushindwa kwake na kupelekea mwisho wake wa kusikitisha.

3) Ikiwa kiburi haijaondolewa, mtu ataanguka katika matatizo makubwa. Kama Abraha angekandamiza ubinafsi wake, hangekuwa na wivu na kujenga muundo wa mpinzani. Ingemuokoa na matatizo mengi.

4) Nguvu na uwezo wote ni wa Allah Ta’ala. Allah Ta’ala ndiye pekee mwenye uwezo mkuu. Kila kitu kiko katika udhibiti Wake. Akipenda atawaangamiza tembo wakubwa kwa kokoto. Kwa hiyo, mtu hatakiwi kutishwa na nguvu za ulimwengu. Ikiwa Allah Ta’ala atamlinda mtu, hakuna anayeweza kumdhuru hata kidogo, licha ya nguvu na uwezo wao.

5) Allah Ta’ala hutuma msaada wake kwa wale wanaojisalimisha Kwake kwa moyo wote.

6) Mlinzi wa Dini ni Allah Ta’ala. Atamtumia yoyote na chochote Anachotaka kama njia ya kuilinda Dini. Kwa hiyo, katika kuitumikia Dini, mtu asigeukie njia yoyote isiyoruhusiwa na ambayo itapata ghadhabu ya Allah Ta’ala.

7) Daima tunapaswa kukumbuka kwamba Allah Ta’ala hategemei juhudi zetu za kuulinda Uislamu. Kwa hiyo, tunapaswa kufuata njia halali ambazo Allah Ta’ala ameamuru kuzifuata na baada ya hapo kumtegemea Allah Ta’ala kuleta matokeo mazuri.

About admin

Check Also

Tafseer Ya Surah Ikhlaas

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ ‎﴿١﴾‏ اللَّهُ الصَّمَدُ ‎﴿٢﴾‏ لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ ‎﴿٣﴾‏ وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا …