Zubair bin Awwaam (radhiyallahu ‘anhu) anaripoti kwamba katika tukio la Uhud, Rasulullah (sallallaahu ‘alaihi wasallam) alikuwa amevaa silaha mbili.
Wakati wa vita, Rasulullah (Sallallaahu ‘alaihi wasallam) alikusudia kupanda juu ya jabali lakini kutokana na uzito wa zile silaha mbili, hakuweza kufanya hivyo. Kwa hiyo alimwomba Talhah (radhiyallahu ‘anhu) kukaa chini ili apate msaada kutoka kwake na kupanda juu ya mwamba. Talhah (radhiyallahu ‘anhu) hapo hapo aliketi chini na kumsaidia Rasulullah (sallallaahu ‘alaihi wasallam) kupanda juu ya jabali.
Zubair (radhiyallahu ‘anhu) anasema kwamba alimsikia Rasulullah (sallallaahu ‘alaihi wasallam) akisema wakati huo, kuwa waajib kwa Talhah (yaani Jannah imekuwa waajib kwa Talhah).
Katika vita vya Uhud, Talhah (radhiyallahu ‘anhu) kwa ushujaa alifuatana na Rasulullah (sallallaahu ‘alaihi wasallam) na akamlinda. Wakati wowote Maswahaabah (radhiyallahu ‘anhum) walipojadili vita vya Uhud, walikuwa wakisema kwamba siku hii (siku ya Uhud) ilikuwa ya Talhah(radhiyallahu ‘anhu). Talhah (radhiyallahu ‘anhu) alikuwa amemkinga Rasulullah (sallallaahu ‘alaihi wasallam) na mwili wake. Alipata majeraha zaidi ya themanini mwilini mwake, lakini hakuondoka na kumuacha Rasulullah (sallallaahu ‘alaihi wasallam), ijapokuwa mkono wake ulikuwa umepooza kutokana na majeraha makali.