Nafasi ya juu ya Sa’eed bin Zaid (Radhiyallahu ‘Anhu) kati ya watu wa Madinah Munawwarah

Katika kipindi cha khilaafah yake, Mu’aawiyah (Radhiyallahu ‘Anhu) aliandika barua kwa Marwaan bin Hakam – waziri wake aliemchagua juu ya Madinah Munawwarah – ambaye yeye alimwagiza achukue Bay’ah (ahadi ya utii) kutoka kwa watu wa Madinah Munawwarah kwa niaba ya mtoto wake, Yazeed bin Mu’aawiyah, ambaye alikuwa Khalifah baada yake. Mu’aawiyah (Radhiyallahu ‘Anhu) hakuwa na ufahamu wa vitendo vibaya vya mtoto wake Yazeed, na kwa hivyo alitaka kumchagua kama mrithi wake kwa Khilaafah.

Lakini, Marwaan hakuyatekeleza maagizo haya mara moja. Mtu wa Syria ambaye alikuwa huko Madinah Munawwarah wakati huo alimuuliza Marwaan sababu ya kuchelewesha kutekeleza maagizo ya Mu’aawiyah (Radhiyallahu ‘Anhu). Marwaan alijibu akisema, “Namsubiri Sa’eed bin Zaid (Radhiyallahu ‘Anhu) ili aje na achukuwe bay’ah, kwani anachukuliwa kama kiongozi wa watu na mtu mashuhuri kati ya watu wa Madinah Munawwarah. Ikiwa atachukuwa bay’ah kwa Yazeed, basi watu wengine watamfuata.”

Mtu wa Syria huyo kisha akasema, “Kwa nini siendi na kumleta kwako ili aweze kufanya bay’ah?” Alienda nyumbani kwa Saeed bin Zaid (Radhiyallahu ‘Anhu) na akamwagiza aje kwa Marwaan na afanye bay’ah kwa Yazeed.

Sa’eed bin Zaid (Radhiyallahu ‘Anhu) akajibu, “Unaweza kurudi; nitakuja na kufanya bay’ah (ikiwa ninataka). ”

Mtu wa Syria alikasirika akisema, “Unapaswa kwenda sasa na kuchukuwa bay’ah, au sivyo nitakukata kichwa! ”

Sa’eed bin Zaid (Radhiyallahu ‘Anhu) akajibu, “Unaniita nichukuwe bay’ah kwa wale ambao tulipigana nao kwa sababu ya Uislamu.” Na maneno haya ulionyesha kwamba yeye alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza wa Rasulullah (Sallallahu ‘Alaihi Wasallam), kwa sababu hio alielewa kwamba mtu gani anayestahili kuchukuwa bay’ah kwake na mtu gani hafai, na bila shaka, Yazeed hakustahili kutimiza.

Mtu huyo wa Syria kisha akarudi kwa Marwaan na kumweleza kile kilichotokea, ambacho Marwaan alimshauri abaki kimya na asiwafahamishe watu juu ya kile kilichopitishwa.

Sa’eed (Radhiyallahu ‘Anhu) kwa hivyo alikataa kuja kuchukuwa bay’ah kwa Yazeed, na kwa hivyo Marwaan alimuacha nje na kuanza kuchukua bay’ah, kwa niaba ya Yazeed, kutoka kwa Watu wa Madinah Munawwarah.

Baadaye, mke anayeheshimiwa wa Rasulullah (Sallallahu ‘Alaihi Wasallam), Ummu Salamah (Radhiyallahu’ Anha) alifariki. Alikuwa ametoa wasiyya kwamba swala ya Janaazah yake ifanyike na Sa’eed bin Zaid (Radhiyallahu ‘Anhu). Kwa sababu ya upendeleo wake, Marwaan hakuenda mbele kuswalisha Swala ya janazah.

Pindi alipomsubiria Sa’eed bin Zaid, mtu huyo wa Syria alimuuliza Marwaan, “Kwanini hukwenda mbele kuongoza Janaazah? ” Marwaan akajibu, “Ninamgojea mtu ambaye ulikuwa umekusudia kumtoa kichwa (wakati hakutaka kuja mbele kuchukuwa bay’ah kwa Yazeed),” Marwaan alisema haya kwa kumzingatia Sa’eed bin Zaid (Radhiyallahu ‘Anhu).

Kusikia hili, mtu huyo wa Syria aligundua nafasi ya juu wa Sa’eed na hapo hapo akafanya istighfaar, akiomba msamaha wa Allah Ta’ala kwa makosa aliyoyafanya kwa sa’eed. (Tareekh Ibnu Asaakir 21/88, Mustadrak #5853 na al-Mu’jamul Kabeer #345)

About admin