Siku Ambayo Ina Muda Maalum wa Kukubalika
Anas bin Maalik (radhiyallahu anhu) anaripoti: Siku ya Jumu’ah iliwasilishwa kwa Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam). Jibreel (alaihis salaam) alikuja kwa Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam). Katika kiganja chake kulikuwa na kitu kinachofanana na kioo cheupe, na katikati ya kioo kulikuwa na doa jeusi. Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) alimuuliza Jibreel (alaihis salaam), “Ni nini hiki ewe Jibreel” Jibreel (alaihis salaam) akajibu, “Kioo hiki cheupe kinaashiria Siku ya Jumu’ah ambayo umeletewa na Mola wako ili iwe Idi kwako na Ummah wako baada yako. Kuna kheri nyingi kwako ndani yake. Kwa sababu ya wewe kupokea Siku ya kwanza (yaani kuanzia Ijumaa, Jumamosi na Jumapili), mtakuwa wa kwanza (kuingia Jannah na wafuasi wenu), na Mayahudi na Wakristo (waliosilimu katika zama zao kwa nabii wao) wote watakuwa nyuma yako. Katika siku ya Juma’ah, kuna wakati maalum wa kukubalika. Mtu yoyote atakaemuomba Mola wake katika wakati huo kwa ajili ya kheri yoyote aliyoandikiwa, Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) atamjalia, na mtu yoyote anayetaka kinga kujiepusha na maovu, Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) Atamwondolea shari kubwa zaidi kutoka kwake. Huko Akhera tutaiita siku hii “Siku ya Kuongezeka” (kwa watu wa Jannah watakaopewa ewezo wa kumuona Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) na neema kuongezeka katika siku hii).”
Kumbuka: Doa jeusi liliashiria siku ya Juma’ah ambayo itakuwa siku ya mwisho ya dunia. Katika Hadith ya Musnad Abi Ya’laa,
Imepokewa kwamba Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) alisema: “Siku zilionyeshwa kwangu, na miongoni mwao nilionyeshwa Ijumaa. Ilifanana na kioo kinachong’aa, katikati yake palikuwa na doa jeusi. Nilimuuliza Jibreel (alaihis salaam) lile doa jeusi lilimaanisha nini. Alisema, ‘Ni saa ya mwisho (yaani Qiyaamah kitakachotokea siku ya Jumu’ah).’”
Siku ya Msamaha
Imepokewa kutoka kwa Anas (Radhiyallahu anhu) kwamba Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) amesema: “Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) hamwachi muislamu yoyote siku ya Jumu’ah bila ya kumsamehe (yaani wale wanaoshikilia haki za Allah na waja wake).”
Kufariki katika Mchana au Usiku wa Jumu’ah
Imepokewa kutoka kwa Abdullah bin Amr (Radhiyallahu anhuma) kwamba Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) amesema: “Hakuna Muislamu anayeaga dunia mchana au usiku wa Jumu’ah isipokuwa Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) atamuokoa na adhabu ya kaburi.”