Siku ambayo Abu Bakr Siddeeq (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliposilimu, alianza kuwalingania watu kwenye Uislamu. Allah Ta’ala alimfanya kuwa sababu ya Maswahaabah (Radhiya Allaahu ‘anhum) wengi kuingia katika Uislamu. Miongoni mwa maswahaabah waliosilimu kupitia kwa Abu Bakr Siddiq (Radhiya Allaahu ‘anhu) ni Talhah bin Ubaidillah (Radhiyallahu ‘anhu).
Talhah (Radhiya Allaahu ‘anhu) anaeleza:
Siku moja, nilisafiri hadi Busraa kwa madhumuni ya biashara. Siku moja, nilikuwa sokoni Busraa wakati Nilimsikia mtawa akiita kutoka nyumbani kwake, “Je kuna kuna mtu yoyote hapa ambaye anatoka sehemu ya Haram ya Makka Mukarramah.” Nikajibu, “Mimi ni mkazi wa Haram ya Makka Mukarramah.”
Mtawa akauliza, “Je, Ahmad (Sallallahu alaihi wasallam) bado ametokea?” Nilimuuliza yule mtawa kwa ufafanuzi zaidi nikisema, “Unamaanisha nani (kwa jina Ahmad)?” Mtawa akajibu, “Mtoto wa ‘Abdullah bin ‘Abdil Muttalib. Huu ndio mwezi ambao atatokea. Atatokea katika Haram ya Makka Mukarramah na kuhamia ardhi ya mawe (eneo la milima) ambayo ina mitende tele. Yeye ndiye wa mwisho miongoni mwa Manabii (‘alaihimus salaam) na Nabii wa mwisho. Usichelewe kumfuata.”
Mazungumzo na yule mtawa yalikuwa na athari kubwa moyoni mwangu. Mara moja nilirudi Makka Mukarramah na kuwauliza watu kama kuna jambo lolote jipya limetokea wakati sikuwepo, nilipokuwa safarini. Wakajibu, “Ndio, Muhammad (Sallallahu alaihi wasallam), muaminifu amedai utume, na mtoto wa Abu Quhaafah (Abu Bakr [Radhiya Allaahu ‘anhu]) amejiunga naye.”
Bila kuchelewa nilikwenda kwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye alinipeleka kwa Mtume (Sallallahu alaihi wasallam). Nilipofika mbele ya Mtume (Sallallahu alaihi wasallam), nilisilimu na pia nikampa maelezo ya kina ya kile kilichotokea kati yangu na yule mtawa wa Busraa. (Al-Isabah 3/430-431)