Dalili Za Qiyaamah 2

Makusudio ya Kubainisha Alama za Qiyaamah kwa Ummah

Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) ameufahamisha Ummah dalili nyingi ndogo ndogo na kubwa zitakazojitokeza kabla ya Qiyaamah. Dalili nyingi ndogo tayari zimeshuhudiwa katika karne zilizopita, na pia dalili nyingi hizi zikishuhudiwa leo.

Aalim na Muhaddiyth mkubwa, ‘Allaamah Qurtubi (Rahimahullah), ametaja sababu mbili za Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) kueleza dalili za Qiyaamah kwa ummah:

(1)Umma utakapoona dalili yoyote, itakuwa ni ukumbusho kwao kuamka kutoka katika usingizi na ughafili na uzembe wao na kuja kwenye Dini.

(2)Wataweza kujiokoa na fitna za wakati huo kwa kurejea kwa Allah Ta‘ala kwa kufanya toba na kujiandaa kwa ajili ya Akhera. (Ta’leeq-us-Sabiyh 7/176)

Miongoni mwa dalili ndogo ambazo tayari zimetokea katika karne zilizopita ni zifuatazo:

1. Kupasuliwa kwa mwezi kwa ishara iliyobarikiwa ya Mtume (Sallallahu alaihi wasallam).

2. Kufariki kwa Mtume (Sallallahu alaihi wasallam).

3. Umar (Radhiyallahu ‘anhu), Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) na Ali (Radhiyallahu ‘anhu) kuuwawa kishahidi.

4. Tauni ya Amwaas, wakati wa utawala wa Umar (radhiyallahu ‘anhu), ambapo maelfu ya watu walifariki duniani.

5. Baytul Muqaddas kutekwa na ufalme wa Kirumi na faarsi (persia) kuanguka ambao ulitokea wakati wa utawala wa Umar (radhiyallahu ‘anhu).

6. Husein (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuuwawa huko Karbalaa wakati wa utawala wa Yazid bin Muawiyah.

7. Mauaji yaliyotokea huko Harrah (sehemu nje ya Madinah Munawwarah) ambapo maelfu ya watu, miongoni mwao wakiwa ni maswahaabah (Radhiya Allaahu ‘anhum) na Taabi’een (rahimahumullah), waliuawa kikatili wakati wa utawala wa Yaziyd bin Mu’aawiyah.

8. Ufalme wa Umar bin Abdul Aziz (rahimahullah) na uadilifu ulitawala duniani wakati huo.

9. Uvamizi wa Tartars katika karne ya saba ya Uislamu.

10. Istanbul kutekwa mikononi mwa Muhammad Al-Faatih (rahimahullah) wakati wa karne ya tisa ya Uislamu.

Kila moja ya dalili ndogo zilizotajwa hapo juu imebashiriwa na Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) na ilitokea sawa sawa na vile alivyoitaja katika Hadithi.

Katika Hadith ifuatayo, Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) alitaja dalili nyingine ndogo za Qiyaamah. Ikiwa tutachunguza hali ya ummah leo, tutakuta kwamba nyingi ya dalili hizi kwa sasa zinashuhudiwa kote ulimwenguni. Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) amesema:

“Wakati ngawira za vita zitachukuliwa kama mali ya kibinafsi ya watu ili kugawanywa kati yao, wakati amana itachukuliwa kuwa ngawira (yaani. kama mali ya umma), wakati zakaah itazingatiwa kama ushuru, wakati elimu ya Dini itapatikana kwa nia zisizokuwa za Dini, wakati mwanamume atamtii mkewe na kumuasi mama yake, na kumweka rafiki yake karibu naye na kumweka baba yake mbali, na sauti zitapazwa ndani ya msikiti, na mtenda madhambikatika kabila atakuwa kiongozi wao, na mtu wa chini kabisa wa watu atakuwa mwakilishi wao, na mtu ataheshimiwa kwa kuogopa uovu na ukali wake, na wasichana wa kuimba na vyombo vya muziki vita tamba na kuenea sehemu zote. Pombe itatumiwa (wazi wazi hadharani), na Watu wa Ummah huu watawalaani watu wa zamani wa Ummah huu, (zitakapodhihiri dalili hizi) basi watu wangoje vimbunga, mitetemeko ya ardhi, watu kuzama ardhini, kuharibika kwa uso, mawe kunyesha kutoka mbinguni na dalili nyingine zinazofanana na hizo zitakazofuata kwa mfululizo wa haraka, kama vilelulu katika uzi huanguka kwa kufuatana kwa uwepesi unapokatwa uzi.” (Sunan Tirmizi #2211)

Ikumbukwe kwamba Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) alitumwa kama kiongozi wa wanadamu hadi mwisho wa zama. Pia alikuwa kiongozi wa Manabii na Marasul wote (‘alaihimus salaam) wa zamani. Hivyo, alipotabiri kutokea kwa dalili hizi, lengo lilikuwa ni kuwaonya ummah juu ya mitihani huu, na kuwaonyesha njia ya wokovu mbele ya mitihani na changamoto hizo.

Allah Ta’ala auepushe ummah na madhambi na maovu yote na atuweke imara juu ya Uislamu.

About admin