Mahdi (Radhiya Allaahu ‘anhu)

Kuja kwa Mahdi (Radhiya Allaahu ‘anhu) ni dalili ya kwanza kati ya alama kuu zitakazojitokeza kabla ya Qiyaamah. Katika hadith nyingi, Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) alikuwa amebashiri kuja kwa Mahdi (Radhiya Allaahu ‘anhu) ndani ya ummah huu.

Allaamah Suyooti (Rahimahullah) ametaja kuwa hadithi zinazohusu kuja kwa Mahdi (Radhiya Allaahu ‘anhu) ni nyingi sana kiasi kwamba yamefikia kiwango cha twaatur (yaani idadi kubwa ya wapokezi wameisimulia kwa kufuatana, katika kila zama). Kwa hiyo, Maulamaa wanakubaliana kwa pamoja kwamba kuamini kuja kwa Mahdi (Radhiya Allaahu ‘anhu) ni miongoni mwa imani za kimsingi za Ahlus Sunnah wal Jamaa’ah.

Kabla ya Qiyaamah, ummah wa Kiislamu utakuwa ukipitia dhulma mikononi mwa makafiri katika sehemu nyingi duniani. Itakuwa wakati huo ambapo Allah Ta‘ala atamtuma Mahdi (Radhiyallahu ‘anhu) kwa ummah ili kuwanusuru na kuhuisha dini duniani. Imepokewa kwamba Mahdi (Radhiya Allaahu ‘anhu) atakuja kabla ya Dajjaal kudhihirika duniani.

Uhakika Wa Mahdi Kuja

Kuhusiana na uhakika wa kuja kwa Mahdi (Radhiya Allaahu ‘anhu), Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) ametaja: “Lau ingebakia siku moja tu duniani, Allah Ta’ala angeirefusha mpaka amlete mtu kutoka Ahl-ul-Bayt ambaye jina lake litalingana na jina langu, na jina la baba yake litalingana na jina la baba yangu.” (Sunan Abu Dawood #4282 & 4284)

Mahdi (Radhiya Allaahu ‘anhu) Ni Katika Kizazi Cha Faatimah (Radhiya Allaahu ‘anha)

Mahdi (Radhiya Allaahu ‘anhu) atatoka katika kizazi cha Hasan (Radhiyallahu ‘anhu), mtoto wa Faatimah (Radhiyallahu ‘anha). Jina lake litakuwa Muhammad na jina la baba yake litakuwa Abdullah.

Imepokewa kwamba katika tukio moja, Ali (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimtazama mwanawe Hasan (Radhiya Allaahu ‘anhu) na akasema, “Hakika huyu mwanangu ni kiongozi, kama jinsi Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) alivyotaja kuhusiana naye. Atatokea mtu kutoka kizazi chake ambaye ataitwa jina sawa na Nabii wako. Atafanana na Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) kwa tabia lakini hatofanana naye kimwili na maumbile.” (Sunan Abu Dawood #4290)

Maelezo Ya Mahdi (Radhiya Allaahu ‘anhu) Kimaumbile

Mahdi (Radhiya Allaahu ‘anhu) atakuwa na paji la uso kubwa na kutakuwa na mwanya kati ya meno yake mawili ya mbele. Pua lake litakuwa lirefu, yenye ncha kali na kuwa juu kidogo. Atakuwa na doa leusi kwenye shavu lake la kulia. Atakuwa na rangi ya Waarabu.  (Manaarul Muneef #335, Zakheeratul Huffaaz #4645, Sunan Abu Dawood #4287 na Aqdud Durar 100-102)

Pindi atakapotokea kutakuwa na utafauti baina ya ummah na matetemeko ya ardhi yatakuwepo kwa wingi.  Atakuwa na umri wa miaka arobaini wakati wa kuonekana kwake. Wakati wa kujitokeza kwake katika Ummah kama Mahdi, atakuwa amevaa kilemba.  (Majma’uz Zawaa’id #12393, Fitan li-Nu’aim bin Hammaad #1067 na Zakheeratul Huffaaz #6506)

Allah Ta’ala Akimtayarisha Mahdi (Radhiya Allaahu ‘anhu) na Kujenga Kipaji Cha Kuongoza Ndani Yake.

Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) amesema: “Mahdi (Radhiya Allaahu ‘anhu) ni miongoni mwetu, Ahl-ul-Bayt. Allah Ta’ala Atamtayarisha ndani ya usiku mmoja (yaani Allah Ta’ala Ataumba uwezo wa kuongoza ndani yake ndani ya usiku mmoja). (Musnad Ahmed #645)

Kuna hadith nyingi zilizoripotiwa kuhusiana na uadilifu ambao Mahdi (Radhiya Allaahu ‘anhu) atatawala nao, na baraka tele zitakazokuwepo katika umma wakati wa utawala wake. Inshaallah baadhi ya hadithi hizi zitatajwa katika sehemu zinazokuja.

About admin

Check Also

Sifa kumi za mwili, za kibinadamu za Dajjaal

Katika hadith, Rasulullah (Sallallahu ‘Alaihi Wasallam) ameelezea Ummah sifa za kibinadamu za Dajjaal. Rasulullah (Sallallahu …