Wakati mmoja, Talhah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipokea dirham laki saba kutoka Hadhramawt. Usiku ule, alipopumzika ili alale, hakutulia, akigeuka huku na huko.
Mke wake kuona wasiwasi wake, aliuliza, “Ni nini kinakusumbua?” Akajibu, “Mtu atawezaje kumfikiria Mola wake wakati ana mali nyingi nyumbani kwake? (yaani nahofia kuwa mali hii itasababisha nighafilike na kumsahahu Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) na kuto kumkumbuka)”
Mke wake mheshimiwa alipendekeza azigawe fedha hizo miongoni mwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ‘anhum) wa Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam). Kusikia hivyo, Talhah (Radhiyallahu ‘anhu) alifarijika na akasema, “Mwenyezi Mungu akurehemu! Hakika wewe ni mwanamke mwema, mwongofu, na binti wa mtu mwema, mwongofu.” Alikuwa Ummu Kulthum, binti wa Abu Bakr (Radhiyallahu ‘anhu).
Asubuhi iliyofuata, aligawa mali kati ya Maswahabah Muhajirina na Ansar (Radhiyallahu ‘anhum). Miongoni mwa Maswahaba aliowapelekea mali hii ni Ali (Radhiya Allaahu ‘anhu).
Mke wake alipomuona akitumia mali yote kwa maswahaabah (Radhiya Allaahu ‘anhum), alimwambia: “Je kuna mali yoyote iliobaki ya kwetu (ili tutekeleze mahitaji zetu)? Akamwambia mke wake kuhifadhi mali iliyobaki, ambayo ilikuwa takriban dirham elfu moja. (Siyaru A’alamin Nubala 3/24)