Ndani ya hadith Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) alikuwa ametabiri matukio yatakayotokea kabla ya Qiyaamah. Aliutahadharisha ummah juu ya mitihani na misukosuko mbalimbali ambayo itawakumba katika sehemu tofauti na nyakati tofauti duniani. Pia aliwaonyesha njia ya uongofu na wokovu kupitia fitnah hizi.
Huu ndio uzuri na ubora wa Dini ya Uislamu, kwamba Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) hakumtuma Mtume Wake (Sallallahu alaihi wasallam) tu kama chanzo cha mwongozo kwa umma, bali amembariki na elimu ya matukio ambayo yatafumuka duniani kabla ya Qiyaamah ili uwongozo wake utakuwepo katika changamoto zote za wakati wote.
Kwa hivyo, tunapata maelezo mazuri kabisa yameandikwa ndani ya hadith za Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam), ambayo inaelezea changamoto za karibu na za mbali ambazo ummah utakutana nazo baada ya kufariki kwa Mtume (Sallallahu alaihi wasallam). Miongoni mwa fitnah hizi ni dalili ndogo na kubwa za Qiyaamah.
Amr bin Akhtab (Radhiya Allaahu ‘anhu) anasimulia, “Wakati mmoja, Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) alisimama msikitini na akaanza kutufahamisha matukio yatakayotokea kabla ya Qiyaamah. Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) alipanda mimbar baada ya Swalah ya Alfajiri na akazungumza mpaka wakati wa Swalah ya Adhuhuri. Baada ya kuswali Swalah ya Adhuhuri, alipanda tena kwenye mimbar na akaendelea kuzungumza mpaka kwenye Swalah ya Asr. Baada ya kumaliza Swalah ya Asr, alipanda tena kwenye mimbar na akazungumza mpaka jua lilipozama. Katika mkusanyiko huo siku hiyo, alitufahamisha yale yatakayojiri katika ummah mpaka siku ya Qiyaamah. Kwa hivyo, miongoni mwetu waliokumbuka zaidi ndio wajuzi zaidi miongoni mwetu kuhusu dalili za Qiyaamah. (Sahih Muslim #2892)
Hadithi zinazozungumzia dalili za Qiyaamah ni nyingi. Kuna Dalili ambazo zimeelezewa kwa uwazi kwa undani sana, na dalili zingine zimeelezewa kwa ufupi. Kwa hiyo, wakati dalili yoyote ambayo Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) aliieleza kwa kina ilipodhihirika mbele ya Maswahabah (Radhiya Allaahu ‘anhum), ilikuwa ni kama maneno ya Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) yametimia mbele ya macho yao.
Maulamaa wamebainisha dalili za Qiyaamah katika makundi mawili; dalili ndogo za Qiyaamah na dalili kubwa za Qiyaamah. Kutokana na dalili ndogo, dalili ya kwanza kabisa kuonekana ilikuwa ni kufariki kwa Mtume (Sallallahu alaihi wasallam), wakati dalili kubwa ya kwanza kutokea itakuwa ni kuja kwake Mahdi (Radhiya Allaahu ‘anhu) duniani.
Inshaa Allah, katika sehemu zitakazofuata, tutakuwa tunazijadili dalili ndogo na kubwa za Qiyaamah ambazo zimeelezwa katika hadith, pamoja na kueleza maana za hizo hadith popote inapohitajika.