Baada ya kusilimu, watu wa Najraan walikuja kwa Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) na wakamwomba awapelekee mtu mwaminifu (anayeweza kuwafundisha Dini).
Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) akawaambia:
لأبعثن إليكم رجلا أمينا حق أمين
“Nitawatumia mtu mwaminifu, hakika ni mwaminifu sana.”
Katika hatua hiyo, Maswahaabah (Radhiya Allaahu ‘anhum) waliokuwepo wote walitamani kuwa wapokezi wa bashara hii ya Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam). Kisha Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) akamchagua Abu Ubaidah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwenda kwa watu wa Najraan na kuwafundisha dini.
Aliposimama Abu Ubaidah (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kukaribia kuondoka, Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alisema maneno haya kuhusu yeye, “Mtu huyu ndiye muaminifu (maalum) wa Ummah huu”. (Sahih Bukhaari #3480- 3481)
Maelezo: Sifa ya uaminifu ulikuwa ni alama ya Maswahaba wote. Hata hivyo, kwa sababu ya sifa hii kuwa bora zaidi katika maisha ya Abu Ubaidah (Radhiya Allaahu ‘anhu), Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alimpa cheo hiki maalum.