Madai Ya Baadhi Ya Watu Wa Kufah:

Katika mwaka wa 21 A.H., baadhi ya watu wa Kufah walikuja kwa ‘Umar (Radhiyallahu ‘anhu) na kumlalamikia Sa’d (Radhiyallahu ‘anhu) kwamba hakuswali sawa sawa. Wakati huo, Sa’d (Radhiya Allahu ‘anhu) alichaguliwa na Umar (radhiyallahu ‘anhu) kama gavana wa Kufah.

Hivyo basi ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamwita Sa’d (Radhiya Allaahu ‘anhu) na alipofika, akazungumza naye kwa heshima kubwa akisema, “Ewe Abu Ishaaq (hii ilikuwa cheo chake)! Baadhi ya watu wa Kufah wanadai kuwa hauswali sawa sawa.

Sa’d (Radhiya Allaahu ‘anhu) akajibu, “Wallahi! Ninawatimizia swalah ambayo Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) aliifanya, bila kuacha kipengele chochote.” Sa’d (Radhiya Allaahu ‘anhu) kisha akaeleza namna ya kuswali akisema, “Ninapowaongoza katika Swalaah ya isha, huwa narefusha zile mbili za mwanzo na ninafupisha rakaa mbili za pili (kwa namna ambayo Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) aliswali.” ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akajibu kwa kusema: “Ewe Abu Ishaaq! Haya yalikuwa maoni kamili niliyokuwa nayo kuhusu wewe mwenyewe.

‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) baada ya hapo alimrudisha Sa’d (Radhiya Allaahu ‘anhu) kurudi Kufah pamoja na watu wachache ili kuchunguza tuhuma dhidi yake. Watu ambao Umar radhiyallahu anhu aliwatuma walikwenda kwenye kila msikiti wa Kufah ili kuwauliza watu kuhusu Sa’d radhiyallahu anhu. Watu walipoulizwa, hawakuwa na la kusema juu yake ila maneno ya kumsifu kwa kila jambo alilofanya.

Mwisho, walifika kwenye msikiti katika wilaya ya kabila la Banu ‘Abs. Hapa, kulikuwa na mtu kwa jina Usaamah bin Qataadah, ambaye alisimama na kusema, “Kwa vile umeniuliza kuhusu Sa’d (Radhiya Allaahu ‘anhu), basi kuna malalamiko matatu ambayo ninayo dhidi yake (1) Hatokagi Jihaad pamoja na jeshi. (2) Hagawi mali kwa uadilifu na usawa, (3) Hana uadilifu katika maamuzi yake.”

Aliposikia madai hayo ya uongo, Sa’d (Radhiya Allaahu ‘anhu) alijibu, “Wallahi! Nitakufanyieni laana tatu ikiwa mnasema uwongo – Ewe Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala)! Iwapo mja wenu huyu anasema uwongo, na amesimama tu kwa ajili ya umaarufu na kujulikana, basi (1) mrefushe maisha yake, (2) ongeza umasikini wake, (3) na mshirikishe katika fitnah.”

Baadaye, Usaamah bin Qataadah alipoulizwa na watu kuhusu hali yake, alikuwa akijibu, “Nimefikia uzee na nimenaswa na fitnah na yote haya ni kwa ajili ya laana ya Sa’d (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambayo yamenitesa.”

Mmoja wa wapokezi wa tukio hili, ‘Abdul Malik, anataja, “Nilimuona (Usaamah bin Qataadah) baadae akiwa katika uzee. Nyusi zake zilikuwa zimeinama kwenye macho yake kutokana na uzee, na alikuwa akiwachokoza wasichana watumwa mitaani na kuwasumbua.”
(Sahih Bukhari #755)

About admin

Check Also

Damu Ya Kwanza iliyomwagika kwa ajili ya Uislamu

Muhammad bin Ishaaq (rahimahullah) anasimulia: Mwanzoni katika Uislamu, Maswahaabah wa Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) walikuwa …