Abu ‘Uthmaan (Rahimahullah) anasimulia kwamba Sa’d (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema:
Aya ifuatayo ya Qur’an tukufu iliteremshwa kunihusu mimi:
وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حُسْنًا ۖ وَإِن جَاهَدَاكَ لِتُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا
Tumemuusia mwanaadamu kuwafanyia wema wazazi wawili. Na wakikulazimisha (wazazi wako makafiri) kunishirikisha (katika ibada yangu) yale ambayo una ilimu nayo, basi usiwatii.
Nilikuwa mtoto mtiifu sana kwa mama yangu. Hata hivyo, nilipoukubali Uislamu, aliniambia, “Ewe Sa’d! Je, ni dini gani hii mpya ambayo umeizua? Ninakuamrisha uiache dini hii ama sivyo sitaongea na wewe kamwe wala sitakula wala kunywa chochote mpaka nife. Ndipo utalazimika kubeba lawama ya kifo changu kwa sababu watu watakuita ‘mtu aliyemuua mama yake mzazi’.” Nikajibu, “Ewe mama yangu! Usifanye hivyo kwa sababu siko tayari kuiacha dini yangu hii kwa lolote duniani!”
Kisha mama yangu alishinda na njaa kwa siku tatu mchana na usiku hadi alipodhoofika sana. Pindi nilimuona katika hali hii, nilimuambia, “Ewe mama yangu! Napenda kukufahamisha kwamba, Wallahi, kama mngekuwa na maisha mia moja na ukapoteza yote mmoja baada ya nyingine, kwa sababu ya kujaribu kunishawishi niuache Uislamu, sitoiacha dini yangu kamwe. Kwa hiyo ukipenda unaweza kula na ukipenda unaweza kubaki na njaa.” Mama yake Sa’d (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipoona dhamira yake isiyoyumba na kujitolea kwake kwa Uislamu, alitambua kwamba kamwe hatauacha Uislamu kwa chochote na hivyo akavunja kiapo chake na kuanza kula. (Siyar A’laam min Nubalaa juzuu ya 3 safa 69, Sahih Muslim #1748)