1. Anza kuomba dua yako kwa kumtukuza Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) kisha umswalia Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam). Baada ya hapo, katika hali ya unyenyekevu na heshima zote, taja haja zako mbele ya Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala)
Fadhaalah bin Ubaid (radhiyallahu ‘anhu) anaripoti kwamba katika tukio moja, Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) alikuwa amekaa msikitini wakati mtu alipoingia msikitini na kuswali. Kisha akaomba dua: “Ewe Mwenyezi Mungu, nisamehe na unirehemu.” Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) akamwambia: “Ewe Musalli, umeharakisha (katika dua yako). Baada ya kuswali, unapokaa (kushiriki kwenye dua), basi (kwanza) mtukuze Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) kwa sifa zinazostahiki utukufu Wake. Baada ya hapo uniswalie, kisha muombe Allah Ta’ala, na muulize haja zako.” Baadaye, Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) akamuona mtu mwingine akiswali. Baada ya kuswali, alijishughulisha na dua. Kwanza alimhimidi Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) na baada ya hapo akamswalia Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam). Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) akamuambia “Ewe Musalli, muombe Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala), na muulize haja zako, dua yako itajibiwa (kwa sababu ulitimiza adabu za dua).
Abdullah bin Mas’uud (radhiyallahu ‘anhu) ametaja, “Wakati wowote ukitaka kuomba dua mbele ya Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala), basi aanze kwa kumtukuza Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) na kumsifu kwa sifa zinazolingana na utukufu na wake. Baada ya hapo, amswalie Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam), na baada ya hapo anatakiwa sasa kumuomba Allah Ta’ala chochote anachotaka. Kwa hakika (kwa kutimiza adabu za dua) kwa njia hii, kunamatumaini kwamba mtu atafaulu (kujibiwa dua yake).”