Wakati mmoja, Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) alikuwa hana chakula na kuhisi njaa. Wakati Ali (radhiya allaahu ‘anhu) alipopata habari kwamba Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) alikuwa akipatwa na njaa, mara moja moyo wake ulijaa na wasiwasi. Hayo yalikuwa mapenzi yake kwa Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) kiasi kwamba hakuweza kupumzika huku akijua kwamba Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) alikuwa katika shida na dhiki. Hata hivyo, Ali (radhiya allaahu ‘anhu) mwenyewe hakuwa na chakula chochote cha kumgawia Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam).
Kwa hiyo, Ali (radhiya allaahu ‘anhu) alitoka nyumbani kwake kwenda kutafuta kazi ili aweze kupata hela kununua chakula kwa ajili ya Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam). Wakati Ali (radhiya allaahu ‘anhu) alizunguka kutafuta kazi, alifika kwenye bustani ya Myahudi fulani. Ali (radhiya allaahu ‘anhu) alijitolea kumtekea maji myahudi kisimani, kwa sharti kwamba kwa kila ndoo ya maji anayochota, Myahudi amlipe tende moja.
Myahudi akakubali na Ali (radhiya allaahu ‘anhu) akachota ndoo kumi na saba za maji kutoka kisimani. Wakati wa malipo ulipofika, Myahudi alimpa hiyari Ali (radhiya allaahu ‘anhu) kuchukua aina yoyote ya tende aliotaka kutoka kwenye bustani yake. Hivyo, Ali (radhiya allaahu ‘anhu) alichukua tende kumi na saba za aina ya ‘Ajwah, kisha akampelekea na kuumpa Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam).
Alipomfikishia hizo tende kwa Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam), Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) akamwita kwa kunia lake na akamuuliza, “Ewe Abul Hasan! Umezipata wapi hizi tende?” Ali (radhiya allaahu ‘anhu) akajibu, “Ewe Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam)! Nilisikia kuhusu njaa uliyo nayo, nikatoka kutafuta kazi ili nipate chakula cha kukuletea!”
Aliposikia hivyo, Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) akamuuliza: “Je, ulifanya hivi kwa sababu ya upendo wa Allah Ta’ala na Mtume Wake (sallallahu ‘alaihi wasallam) tu?” Ali (radhiya allaahu ‘anhu) akajibu, “Ndiyo, Ewe Nabii wa Allah (sallallahu ‘alaihi wasallam)!”
Kisha Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) akasema: “Hakuna mja ambaye ana mapenzi ya kweli kwa Allaah Ta’ala na Mtume Wake (sallallahu ‘alaihi wasallam) isipokuwa atajaribiwa kwa ufukara. Hivyo basi, yule ambaye ana mapenzi ya kweli kwa Allah Ta’ala na Mtume Wake (sallallahu ‘alaihi wasallam) lazima awe tayari kukabiliana na mtihani wa Sabr.” (Sunan Kubra lil-Bayhaqi #11649 na Sunan Ibnu Maajah #2446)