Miswar bin Makhramah (radhiya allaahu ‘anhu) anaeleza kwamba wakati Umar (radhiya allaahu ‘anhu) alichomwa kisu, akaanza kuhuzunika na akawa na wasiwasi mkubwa juu ya ummah.
Abdullah bin Abbaas (radhiya allaahu ‘anhuma) akamfariji na kusema: “Ewe Ameer-ul-Mu’mineen! Hakuna haja ya wewe kuhuzunika. Ulibakia katika kundi la Rasulullah (sallallahu’alaihi wasallam) na ukatimiza haki za uswahaba wake. Kisha Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) akaondoka kwenye dunia hii kwa hali ya kuwa amekuridhia.
“Kisha ukabaki katika kundi la Abu Bakr Siddiq (radhiya allaahu ‘anhu) na ukaheshimu uhusiano huu. Abu Bakr Siddiq (radhiya allaahu ‘anhu) baada ya hapo aliondoka duniani huku akiwa amefurahishwa na wewe.
“Kisha ukabakia miongoni mwa Waislamu (kama Amirul-Mu’minin) na ukatimiza haki za Ummah. Ukitangulia na kujitenga nao, basi hakika utakuwa umeondoka hali ya kuwa wako radhi nawe.”
Umar (radhiya allaahu ‘anhu) akajibu: “Hayo uliyoyataja kuhusiana na uswahaba wa Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam ) na kuridhika kwake nami, basi (hili si jambo la kufaulu kwangu badala yake) hii ni fadhila kubwa na neema kutoka upande wa Allah Taala ambayo amenineemesha.
“Kuhusiana na uswahaba wa Abu Bakr Siddiq (radhiya allaahu ‘anhu) na kuridhika kwake nami, basi hii pia ni fadhila kutoka upande wa Allah Ta’ala ambayo amenineemesha. Na kuhusu wasiwasi na huzuni hii ambayo unanikuta nayo, hii ni kwa sababu ya wasiwasi nilio nao juu yako na ummah wengine wa Kiislamu (kwamba hali yako itakuwaje baada ya mimi kuondoka hapa duniani).
“Nachukua kiapo kwa Allah Ta’ala, lau ningekuwa na dhahabu sawa sawa na dunia nzima, basi bila shaka ningeitumia kujikomboa na adhabu ya Allah Ta’ala kabla sijasimama mbele yake na kukutana naye.
Tazama khofu ya Umar (radhiya allaahu ‘anhu), licha ya yeye kupewa bashara ya Jannah hapa hapa duniani na Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam), hii ilikuwa ni kiwango cha kumcha Allah Ta’ala wakati wa kifo chake.