Wakati wa vita vya Uhud, Rasulullah (sallallahu alaihi wasallam) aliuliza, “Sa’d bin Rabee yuko wapi? Sijui hali yake.” Baada ya hapo, mmoja wa Maswahaba (radhiyallahu ‘anhum) alitumwa kumtafuta. Alikwenda hadi mahali ambapo miili ya mashahidi zilikuwepo.
Alipaza sauti kwa jina la Sa’d (radhiyallahu ‘anhu) kuona kama yupo hai. Mahali fulani alipokuwa akitangaza kwamba alitumwa na Rasulullah (sallallahu alaihi wasallam) ili kuuliza kuhusu Sa’d bin Rabee, alisikia sauti dhaifu ikitoka upande mmoja. Aligeukia upande ule na kugundua kuwa Sa’d (radhiyallahu ‘anhu) alikuwa amelala kati ya mashahidi na alikuwa karibu kupumua pumzi lake la mwisho.
Sa’d (radhiyallahu ‘anhu) alisikika akisema: “Nifikishie salaamu zangu kwa Rasulullah (sallallahu alaihi wasallam) na ujumbe ufuatao, ‘Ewe Rasulullah (sallallahu alaihi wasallam), Allah ta’ala akupe ujira kwa niaba yangu, uliotukuka na mzuri kuliko malipo yoyote anayotoa Allah ta’ala zaidi kuliko mitume wake wowote.”
Baada ya hapo, akamwambia yule aliyetumwa kumtafuta. “Wafahamishe ndugu zangu Waislamu kwamba hakuna kitakachowaondolea lawama siku ya Qiyaamah kama adui atafanikiwa kumfikia Rasulullah (sallallahu alaihi wasallam) na kumuua kabla ya watu wote kufa.” Kwa maneno haya, Sa’d (radhiyallahu ‘anhu) alipumua mwisho wake na akaondoka duniani.
Maswahaba wametoa uthibitisho wa kweli wa kujitolea kwao kwa Rasulullah (sallallahu alaihi wasallam) Wakati wao waliteswa na jeraha baada ya jeraha na walikuwa kwenye pumzi yao ya mwisho, hawakuwa na malalamiko wala hamu kwenye midomo yao na hawakuweza kufikiria kitu kingine chochote isipokuwa usalama na ustawi wa Rasulullah (sallallahu alaihi wasallam) Allah subhaana wata’ala atubariki na chembe ya upendo wa kweli ambao Maswahabah (radhiyallahu ‘anhum) walikua nao kwa Rasulullah (sallallahu alaihi wasallam).