Talhah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alioa wake wanne. Kila mmoja katika wake zake wanne alikuwa dada wa mmoja katika wake wa Mtume wanaoheshimika (Sallallahu alaihi wasallam). Kwa sababu ya hili ndio maana Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) alimwambia, “(Wewe ni) shemeji yangu hapa duniani na Akhera (yaani utakuwa shemeji yangu katika Jannah).” (Al-Ahaadithul Mukhtaarah #847)
Allah Ta’ala alikuwa amewachagua wake zake wote wanaoheshimika wa Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) kuwa wake zake hapa duniani, na Allah Ta’ala pia alikuwa ameamrisha kuwa watakuwa wake zake huko Akhera (katika Jannah). Kwa hiyo, katika Hadith hii, Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) ameashiria kwamba Wake wa Talhah (Radhiya Allaahu ‘anhu) pia watakuwa wake zake Akhera, na hivyo kumfanya Talha (Radhiya Allaahu ‘anhu) shemeji wa Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) duniani na katika Jannah.
Talha (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa ameoa wake wanne wafuatao ambao walikuwa dada wa wake wanne wa Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) Azwaaj-e-Mutahharaat:
1. Ummu Kulthum binti Abi Bakr al Siddiq, ambaye alikuwa dada yake Aaishah (Radhiyallahu anhuma)
2. Hamna binti Jahsh, ambaye alikuwa dada yake Zainab binti Jahsh (radhiyallahu ‘anhuma)
3. Fari’ah binti Abi Sufyan, ambaye alikuwa dada yake Umm Habibah binti Abi Sufyan (radhiyallahu ‘anhuma)
4. Ruqayyah binti Abi Umayyah, ambaye alikuwa dada yake Ummu Salamah binti Abi Umayyah (radhiyallahu ‘anhuma). (Al-Isabah 3/432)