Swalaah – Ufunguo wa Jannah

Uislamu ndio njia pekee inayoongoza kwenye mapenzi ya Allah Ta’ala na inaongoza kwenye Jannah. Kupitia Uislamu, mtu atapata radhi za Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) na kupata mafanikio ya milele.

Katika faradhi zote za Uislamu, faradhi ya Swalaah ipo na daraja ya juu zaidi. Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) amesema: “Swalah ni ufunguo wa Jannah.”

Katika Hadith nyingine, Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) amesema: “Swala ni nuru.” Kwa hivyo, ikiwa mtu anataka kumulika maisha yake, basi aangazie maisha yake na Swalaah.

Hivi sasa, nchi nyingi kote ulimwenguni zinakabiliwa na shida na pia uchumi mdogo. Katika kukabiliana na msukosuko huu wa kimataifa, mipango na mifumo mbalimbali inapitishwa ili kukuza uchumi.

Lakini, katika Quraan Takatifu na Hadith, Allah Ta’ala na Mtume Wake (sallallahu ‘alaihi wasallam) wameunganisha baraka za riziki na Swalaah.

Ndani ya Qur-aan Takatifu, Allah Ta’ala Anasema:

وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلَاةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا ۖ لَا نَسْأَلُكَ رِزْقًا ۖ نَّحْنُ نَرْزُقُكَ ۗ وَالْعَاقِبَةُ لِلتَّقْوَىٰ ‎﴿١٣٢﴾‏

Waamrishe familia yako kuswali na uwe na msimamo juu yake (wewe mwenyewe). Hatukuombi riziki wewe – sisi ndo tunakuruzuku.

Abdullah bin Salaam (radhiyallahu ‘anhu) anasimulia kwamba wakati wowote nyumba ya Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) ilipokuwa ikikumbwa na matatizo ya kifedha, Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alikuwa akiwahimiza kukimbilia kwenye Swalah na pia kuwasomea aya iliyotajwa hapo juu.

Nguzo ya Kituo cha Dini

Wakati mtu akisilimu, basi miongoni mwa mambo ya kwanza Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) angemfundisha ni Swalaah.

Maisha yote ya Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) yaliwekwa kwa ajili ya kusimamisha Swalah katika ummah. Alipokuja Quba na Madinah Munawwarah, kipaumbele chake cha kwanza kabisa kilikuwa ni kusimamisha msikiti na kuwaunganisha kwa ajili ya swalah.

Mbali na hayo, Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) aliamuru kwamba msikiti ujengwe katika kila eneo ili kuwaunganisha watu juu ya swalah.

Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) amesema: “Swala ni nguzo ya katikati ya Dini.” Kwa maneno mengine, kwa kulinda nguzo hii ya katikati, Dini nzima ya mtu italindwa, na kwa kuharibu nguzo hii ya katikati, muundo mzima wa Dini yake utaanguka.

Aaishah (radhiyallahu ‘anha) alielezea mwenendo wa Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) na umuhimu aliouonyesha wa kuswali msikitini. Anaripoti, “Ndani ya nyumba, Rasulullah daima alikuwa akisaidia kazi za nyumbani. Lakini mara tu aliposikia adhaan, alitoka nyumbani kwenda msikitini.”

Wakati mmoja, ujumbe wa Thaqief ulikuja kwa Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) kwa nia ya kusilimu. Hata hivyo, waliomba rukhsa kutokwenda jihaad, kutokulipa ushr (kutoa asilimia kumi ya mazao) kwa mtoza zakaat na kutokuswali.

Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alikubali maombi yao mawili ya mwanzo, lakini akakataa kuwapa kibali cha kuacha kuswali. Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) amesema: “Hakuna kheri katika Dini ambayo haina Swalaah.

Umuhimu Wa Swalaah Ndani Ya Maisha Ya Umar (radhiyallahu ‘anhu)

Umuhimu wa Swalaah ulikuwa umeingia sana katika nyoyo za Maswahaba (radhiyallahu ‘anhum) kiasi kwamba hata walipokuwa kwenye kitanda chao cha kufa, walihakikisha kwamba wanaisimamisha nguzo ya Swalaah.

Asubuhi ambayo Umar (radhiyallahu ‘anhu) alichomwa kisu, Miswar bin Makhramah (radhiyallahu ‘anhu) aliingia kwake. Alipoingia, alimkuta Umar (radhiyallahu ‘anhu) amepoteza fahamu.

Miswar (radhiyallahu ‘anhu) akawauliza wale waliokuwepo Umar (radhiyallahu ‘anhu) alikuwa tayari ameswali. Walijibu kuwa bado hajapata fahamu, na kwa hivyo hajaswali.

Miswar (radhiyallahu ‘anhu) alijua bidii ya Umar (radhiyallahu ‘anhu) katika Swalaah ndani ya maisha yake yote. Kwa hiyo, Miswar (radhiyallahu ‘anhu) akawausia kumwamsha kwa kumtajia kuwa ni wakati wa Swalaah. Kwa hiyo, wakasema: “Ewe Amirul-Mu’minin, Swalaah yako!

Mara tu Umar (radhiyallahu ‘anhu) aliposikia neno ‘Swalaah’, aliamka na kusema, “Ndiyo! Wallahi! Hakuna fungu katika Uislamu kwa yule anayepuuza Swalah yake!” Umar (radhiyallahu ‘anhu) baada ya hapo akaswali.

Umar (radhiyallahu ‘anhu) pia aliuliza, “Je, watu waliswali Alfajiri?” Aliambiwa kwamba watu waliswali. Hapo tu ndipo Umar (radhiyallahu ‘anhu) alihisi kutosheka.

Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) atujaalie tuwe na uwezo wa kuiga kila Sunnah ya Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) katika kila nyanja ya maisha yetu.

About admin

Check Also

Kutimiza Amaanah Tunayodaiwa kwa Allah Ta’ala na Viumbe

Katika zama za kabla ya Uislamu na baada ya Uislamu kufika, Uthmaan bin Talhah alikuwa …