Allah Ta’ala – Anaye Ruzuku Viumbe Vyote

Wakati mmoja, kipindi cha Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam), kundi la Maswahabah (radhiyallahu anhum) kutoka kabila la Banu Al-Ash’ar walisafiri kutoka Yemen hadi Madinah Munawwarah kwa ajili ya hijrah.

Walipofika kwenye mji uliobarikiwa wa Madinah Munawwarah, walikuta kwamba chakula chao walichokuja nacho kilikuwa kimekwisha. Hivyo, waliamua kumtuma mmoja wa masahaba kwa Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) kumwomba awafanyie mpango wa chakula.

Basi, mwenzao alipofika kwenye mlango wa nyumba uliobarikiwa wa Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam), alimsikia Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) akisoma aya ifuatayo ya Qur-aan.

 وَمَا مِن دَابَّةٍ فِي الْأَرْضِ إِلَّا عَلَى اللَّهِ رِزْقُهَا وَيَعْلَمُ مُسْتَقَرَّهَا وَمُسْتَوْدَعَهَا ۚ كُلٌّ فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ ‎﴿٦﴾

Hakuna kiumbe duniani ambaye rizki yake haitolewi na Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala). Anajua mahali pake ya milele na mahali pake pa kupita. Kila kitu kimo katika kitabu kinacho dhihirisha.

Aliposikia Aya hii ya Qur-aan Takatifu, yule sahabi alijifikiria, “Kuna haja gani ya kuwasilisha ombi letu kwa Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) wakati Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) Mwenyewe amechukua jukumu la kutoa rizki kwa viumbe vyote?”

Akajiambiya kwamba, “Sisi, watu wa Banu Al-Ash’ar, si watu wa chini kuliko wanyama mbele ya Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala). (Basi Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala), Mwingi wa Rehma na Mwenye kurehemu, ataturuzuku.)”

Akiwa na wazo hili akilini mwake, hakuwasilisha ombi la watu wake kwa Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam). Badala yake, hapo hapo aligeuka kutoka kwenye mlango wa Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) na kurudi kwa watu wake.

Aliporudi kwa watu wake, akawahutubia akisema: “Ewe Marafiki zangu! Furahini, kwani nusra ya Allah Ta’ala itakujieni hivi karibuni!”
Watu wake wa Ash’ari walielewa kauli yake kuwa ina maana kwamba alikuwa amefikisha ujumbe wao kwa Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam), na kwamba Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) atafanya mipango ya chakula chao hivi karibuni.

Baadaye wakaona watu wawili wakiwajia wakiwa wamebeba sinia kubwa iliyojaa nyama na mikate. Wale watu wawili waliwapa kile chakula na kuondoka. Kisha Maswahaba wale wa Ash’ari wakakaa chini na kufurahia chakula hicho, wakila hadi kushiba.

Walipomaliza chakula hicho, walikuta chakula kingi cha kutosha kilibaki kwenye sinia, na hivyo wakaona ni bora kumrudisha chakula kilichobakia kwa Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) ili akitumie apendavyo. Kwa hivyo, waliwaamuru watu wawili kupeleka chakula kwa Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam)

Baadaye, wote walipojiwasilisha kwa Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam), walimshukuru kwa chakula hicho na kumwambia kwamba hawajawahi kula chakula kitamu kama chakula alichowapelekea. Aliposikia hivyo, Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) alishangaa sana na akawaambia, “Sikuwaletea chakula chochote.”

Kisha wakamweleza Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) kwamba walikuwa wamemtuma mmoja katika maswahaba kumwomba awaandalie chakula, na aliporudi akawapa bashara ya kwamba nusra ya Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) itakuja karibuni. Hili liliwafanya waamini kwamba chakula walichokuwa wamekipokea kilitumwa na Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) mwenyewe.

Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) akamwita yule sahaabi ambaye alikuwa ametumwa na ombi hilo na akamuuliza kwa nini hakuwasilisha ombi lao. Kisha akamjulisha Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) kuhusu yaliyotokea.

Aliposikia tukio lote, Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) akawafahamisha kwamba chakula walichopokea hakikutumwa na yeye, bali kilitumwa na Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala), ambaye amechukua jukumu la kuwaruzuku viumbe vyote.”

About admin

Check Also

Rizki Ipo Mikononi Wa Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) Peke Yake

Kila kiumbe anahitaji rizki kwa ajili ya kuendelea kwake na kuishi kwake, na rizki iko …