Dhul Hijjah – Mwezi wa Hajj na Kuchinja

Dhul Hijjah ni mwezi wa mwisho wa kalenda ya Kiislamu. Ingawa mwezi mzima wa Dhul Hijjah ni mtukufu na wenye baraka, siku kumi za kwanza za Dhul Hijjah zina utukufu na fadhila kubwa zaidi.

Kuhusiana na siku kumi za mwanzo za Dhul-Hijjah, Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alisema: “Siku bora zaidi duniani ni siku kumi (za dhul Hijjah).” (At-Targheeb #1785)

Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) ametaja kwamba maswahaabah (Radhiya Allaahu ‘anhum) walikuwa wakisema kwamba kila siku kumi za mwanzo za Dhul Hijjah ni sawa na siku elfu moja katika fadhila, na tarehe 9 (Siku ya ‘Arafa) ni sawa na siku elfu kumi kwa wema. (Lataaiful Ma’arif pg 460)

Kuhusu siku kumi za mwanzo za Dhul-Hijjah, basi ukubwa na wema wake unaweza kuthibitishwa kwamba ndani ya Qur’an Takatifu, Allah Ta’ala aliotoa qasm (kiapo) juu ya hizi siku kumi. Allah Ta’ala anasema:

وَالۡفَجۡرِ ۙ﴿۱﴾ وَلَیَالٍ عَشۡرٍ ۙ﴿۲﴾

(Nakula kiapo) kwa mapambazuko ya Alfajiri na kwa masiku kumi (ya Dhul Hijjah)

Sunna na Aadaab za Siku Kumi za Kwanza za Dhul Hijjah

1. Kufunga siku kumi za mwanzo za Dhul Hijjah ni sawa na kufunga mwaka mzima, na kusimama katika swalah usiku ni sawa na kuswali Laylatul Qadr, na thawabu za wema huzidishwa mara mia saba. (Jaami’ Tirmidhi #758)

2. Ibaadah inayotekelezwa katika siku hizi inapata malipo zaidi kuliko ibaadah inayofanywa wakati mwingine wowote. (Sahih Bukhaari #969)

3. Kufunga siku ya tisa ya Dhul Hijjah (Siku ya ‘Arafa) unafuta madhambi za miaka miwili. (Sahih Ibnu Hibbaan #3631)

4. Mwenye kukesha ndani ya usiku wa tarehe 8, 9 na 10 Dhul Hijjah na ibaadah, Jannah ni wajibu kwake. (At-Targheeb #1656)

5. Mwenye kukesha usiku wa Idi kwa ́ibaadah, moyo wake utalindwa na fitnah. (Sunan Ibnu Majah #1782)

6. Soma dhikr zifuatazo kwa wingi katika mchana na usiku huu:

سُبْحَانَ اللهِ اَلْحَمْدُ لِلّٰهِ لَا إِلٰهَ إِلَّا اللهُ اَللهُ أَكْبَرْ

7. Siku ya Arafa ni siku bora zaidi ndani ya mwaka. Siku hii, shiriki katika dua na soma dhikr zifuatazo kwa wingi:

لَا إِلٰهَ إِلَّا اللهُ وَحْدَهُ لَا شَرِيْكَ لَهُ لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ بِيَدِهِ الْخَيْرُ وَهُوَ عَلٰى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيْرٌ

8. Soma Takbeer-ut-Tashreeq kuanzia Alfajiri ya tarehe 9 Dhul Hijjah mpaka Alasiri tarehe 13 Dhul Hijjah (Swala 23 za fardh). Wanaume wataisoma kwa sauti huku wanawake wakiisoma kwa sauti ya chini baada ya kila swala ya fardh.

Takbira-ut-Tashreeq ni ifuatavyo:

اَللهُ أَكْبَرْ اَللهُ أَكْبَرْ لَا إِلٰهَ إِلَّا اللهُ اَللهُ أَكْبَرْ اَللهُ أَكْبَرْ وَللهِ الْحَمْدْ

9. Ikiwa kuchinja ni waajib juu ya mtu, basi ni lazima ahakikishe anaitimiza ibaada hio ya kuchinja.

10. Ni mustahab kwa wale wanaokusudia kuchinja kuacha kukata kucha na kupunguza nywele zao kuanzia mwanzo wa mwezi wa Dhul Hijjah mpaka mnyama wao wachinjwe. (Sahih Muslim #1977)

About admin