Tafseer Ya Surah Humazah

وَيْلٌ لِّكُلِّ هُمَزَةٍ لُّمَزَةٍ ‎﴿١﴾‏ الَّذِى جَمَعَ مَالًا وَعَدَّدَهُۥ ‎﴿٢﴾‏ يَحْسَبُ أَنَّ مَالَهُ اَخْلَدَهُ ‎﴿٣﴾‏ كَلَّا لَيُنْبَذَنَّ فِى الْحُطَمَةِ ‎﴿٤﴾‏ وَمَآ اَدْرٰىكَ مَا الْحُطَمَةُ ‎﴿٥﴾‏ نَارُ اللّٰهِ ٱلْمُوقَدَةُ ‎﴿٦﴾‏ الَّتِى تَطَّلِعُ عَلَى الْأَفْـِٔدَةِ ‎﴿٧﴾‏ اِنَّهَا عَلَيْهِم مُّؤْصَدَةٌ ‎﴿٨﴾‏ فِى عَمَدٍ مُّمَدَّدَةٍ ‎﴿٩﴾‏

Ole wake kila msengenyaji, mdhihaki, aliye kusanya mali na kuendelea kuzihesabu! Anadhani kuwa mali yake itamfanya abakie milele. Kamwe! Hakika atatupwa katika ‘Hutamah’ (moto unaosaga). Na nini kinaweza kukujulisha ni nini ‘Hutamah’? Ni Moto wa Allah Ta’ala ulio washwa, unao panda nyoyoni. Hakika (Moto huo) utafungwa nao, kwa nguzo zilizonyoshwa (zilizopanuliwa).

وَيْلٌ لِّكُلِّ هُمَزَةٍ لُّمَزَةٍ ‎﴿١﴾

Ole wake kila msengenyaji, mdhihaki,

Surah hii inaonya juu ya adhabu kali ya kufanya madhambi makubwa matatu kisha ikaeleza na kubainisha asili ya adhabu hiyo kali. Dhambi hizo tatu ni kusengenya, kudhihaki na kujilimbikizia mali kwa ubinafsi.

Makafiri wengi wa Makka Mukarramah walikuwa wakifanya maovu ya kusengenya, kukashifu, kutupiana matusi na kumkejeli Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam). Wale waliokuwa wakifanya maovu hayo wanalaaniwa katika Aya hizi kwa namna ambayo pia inawatahadharisha Waislamu ya kutokufanya maovu hayo wao kwa wao.

Katika surah hii, maovu mawili ya kwanza yanayozungumziwa ni: Humazah na Lumazah.

Wafasiri wengi wanakubali kwamba neno “Humazah”, ambalo limetoolewa kutoka kwenye neno “Hamz”, linamaanisha mtu anayesengenya, yaani kusema vibaya juu ya mtu nyuma ya mgongo wake. Kwa hivyo, wafasiri wengi wanakubali kwamba neno “Lumazah” ambalo linatokana na neno “Lamz”, linamrejelea mtu anayemfanyia mtu mzaha yaani kumsema vibaya mtu usoni mwake.

Dhambi hizi zote mbili ni mbaya kimaadili na kijamii. Qur-aan Takatifu na Sunnah zimetoa maonyo makali kwa madhambi haya. Lakini, inapotazamwa kwa mtazamo mmoja, kusengenya ni mbaya zaidi kuliko kumfanyia mtu mzaha. Sababu ya kusengenya ni mbaya zaidi ni kwamba mabaya ya mtu yanapozungumzwa nyuma ya mgongo wake, basi aliyefanyiwa hivyo hayupo kujitetea na pia awezi kumwachusha huyo mtu kumfanyia mzaha. Hivyo, dhambi inaendelea kutendwa zaidi na zaidi.

Mzaha, kwa upande mwingine, ingawa ni dhambi mbaya yenyewe, lakini ni ndogo kwa kiwango kuliko kusengenya. Sababu ni kwamba mwathirika yupo kujitetea na anauwezo wa kutokumruhusu mtu huyo kuendelea kumfanyia mzaha. Hata hivyo, inapozingatiwa kwa mtazamo mwingine, basi mzaha pia inawezakuwa mbaya zaidi kuliko kusengenya, Kwa sababu kumsema vibaya mtu usoni mwake ni sawa na kumtukana na kumdhalilisha. Jambo hili lina madhara zaidi kiadili na kijamii na kuumiza zaidi (ukilinganisha na kusengenya jambo ambalo halimuumizi mtu kwa vile hana ujuzi nalo), na kwa hiyo adhabu yake ni kali zaidi.

Kwa kujadili matatizo au changamoto za watu, sisi tunafikiri kwamba tunafanya kitu kizuri na chenye faida, na tunasaidia jamii. Lakini, ukweli wa mambo ni kwamba mara nyingi, majadiliano yanapakana na gheebah (kusengenya). Kwa hiyo, tunafanya dhambi bila hata kuichukulia kuwa ni kosa.

Mtu anapofikishia watu habari za wengine, basi hatambui na kuelewa kuwa anasababisha mgawanyiko kati ya watu. Watu wanaoshiriki kuwa marafiki na wale ambao mioyo zao zipo na umoja – kwa kufikishia habari za mtu fulani kwa fulani, mioyo yao inasambaratika na uhusiano wa muda mrefu huvunjika.

Katika Hadith, Nabi (Sallallahu ‘alaihi wasallam) ameripotiwa kusema:

وشرار عباد الله المشاؤون بالنميمة والمفرقون بين الأحبة الباغون البرآء العنت

Waja wabaya zaidi wa Allah Ta’ala ni wale wanao zulia watu, na kujenga uadui baina ya marafiki na kutafuta makosa ya watu maasumu.

Hadith hii inataja kwamba watu wabaya zaidi ni wale watu wanaofikishia habari za watu kwa wengine na kuanza fitnah.

Nia ya watu wengi ni mbaya na wanatafuta njia za kuwatukana watu wasio na hatia, kuwashusha wacha Mungu au kukashifu wale ambao hawana lawama. Kwa hivyo, lengo lao si chochote ila kuleta sifa mbaya kwa watu. Wanajionyesha kuwa ni wenye kuitakia wema, wakiangalia wema wa Dini, ili watu wawaone kuwa ni wachamungu na wanyofu. Jinsi wanavyowaangusha watu ni kushambulia uadilifu wao nyuma ya migongo yao kwa kufanya gheebah kuhusu wao. Mtazamo wao huu ni kwamba wanakutana na hali ya heshima sana, wakionekana kuwa wacha Mungu ili watu wasiwaangalie kama wanavunja uhusiano .Wakati huo huo, matokeo ya matendo yao ni kuvunja familia na kusababisha mifarakano katika jamii.

الَّذِى جَمَعَ مَالًا وَعَدَّدَهُۥ ‎﴿٢﴾

aliye kusanya mali na kuendelea kuzihesabu! 

Kosa la tatu lililotajwa katika Aayah ni kuhusu mtu anayekusanya mali na kuendelea kuzihesabu. Mapenzi ya kupita kiasi na tamaa ya mali humzuia kutumia mali katika njia zilizoamrishwa na Allah Ta’ala. Mtu anayejirundikia mali na kuendelea kuzihesabu atajishughulisha daima na kuongeza mali yake.

Onyo hili linatumika kwa yule tajiri ambaye muda wote anahusika katika kukusanya mali yake bila ya kutekeleza wajibu wake kwa masikini au kwa Allah Ta‘ala.

يَحْسَبُ أَنَّ مَالَهُ اَخْلَدَهُ ‎﴿٣﴾‏ كَلَّا لَيُنْبَذَنَّ فِى الْحُطَمَةِ ‎﴿٤﴾‏ وَمَآ اَدْرٰىكَ مَا الْحُطَمَةُ ‎﴿٥﴾‏ نَارُ اللّٰهِ ٱلْمُوقَدَةُ ‎﴿٦﴾‏ الَّتِى تَطَّلِعُ عَلَى الْأَفْـِٔدَةِ ‎﴿٧﴾‏

Anadhani kuwa mali yake itamfanya abakie milele. Kamwe! Hakika atatupwa katika ‘Hutamah’ (moto unaosaga). Na nini kinaweza kukujulisha ni nini ‘Hutamah’? Ni Moto wa Allah Ta’ala ulio washwa, unao panda nyoyoni. 

Kwa kawaida, mtu anapochomwa, kwanza anahisi maumivu katika viungo vyake vya nje, na hatimaye, anahisi maumivu katika viungo vyake vya ndani na moyo wake. Hata hivyo, moto wa Jahannum ni mkali sana na mkali kiasi kwamba unapanda mara moja kwenye moyo. Kwa hiyo, wakati moyo ambao ni kiti cha hisia zote huanza kuwaka, basi mtu anaweza kufikiria vizuri maumivu makali ambayo mtu atapata wakati huo.

اِنَّهَا عَلَيْهِم مُّؤْصَدَةٌ ‎﴿٨﴾‏ فِى عَمَدٍ مُّمَدَّدَةٍ ‎﴿٩﴾‏

Hakika (Moto huo) utafungwa nao, kwa nguzo zilizonyoshwa (zilizopanuliwa).

Katika Aayah hii, Allah Ta‘ala anaeleza kwamba moto katika Jahannam utatanda juu yao kwa nguzo zilizonyoshwa. Kwa hivyo watazungukiwa na moto na kufungiwa humo kwa namna ambayo hawataweza kuuepuka.

About admin

Check Also

Tafseer Ya Surah Ikhlaas

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ ‎﴿١﴾‏ اللَّهُ الصَّمَدُ ‎﴿٢﴾‏ لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ ‎﴿٣﴾‏ وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا …