Nyumba ya Faatimah (radhiyallahu ‘anha) ilikuwa mbali na nyumba ya Rasulullah (sallallahu alaihi wasallam) Rasulullah (sallallahu alaihi wasallam) siku moja alimwambia: “Ni matamanio yangu kwamba uishi karibu nami.” Faatimah (radhiyallahu ‘anha) akajibu, “Nyumba ya Haarithah iko karibu na nyumba yako. Ukimwomba abadilishe nyumba yake na yangu, atakubali kwa furaha.” Rasulullah (sallallahu alaihi wasallam) akajibu, “Tayari amebadilisha mara moja kwa ombi langu. Ninaona aibu kumwomba kwa mara ya pili.”
Basi, Haarithah (radhiyallahu ‘anhu) kwa namna fulani alikuja kujua kwamba Rasulullah (sallallahu alaihi wasallam) alikuwa akitamani Faatimah (radhiyallahu ‘anha) aishi karibu naye. Hapo hapo akamwendea Rasulullah (sallallahu alaihi wasallam) na akasema, “Ewe Rasulullah (sallallahu alaihi wasallam), nimepata kujua kwamba unatamani Faatimah (radhiyallahu ‘anha) aishi karibu nawe. Hizi ndo nyumba zangu. Hakuna nyumba nyingine iliyo karibu na yako zaidi ya hizi nyumba zangu. Faatimah (radhiyallahu ‘anha) anaweza kubadilisha nyumba yake na nyumba yangu yoyote. Ewe Rasulullah (sallallahu alaihi wasallam) unachokikubali kwangu ni kipenzi zaidi kwangu kuliko unachoniachia.”
Rasulullah (sallallahu alaihi wasallam) alikubali ombi hilo akisema, “Najua kwamba wewe ni mkweli na una ikhlaas katika hayo unayoyasema”, na Rasulullah akamuombea dua.