Tafseer ya Surah Qadr

بِسمِ اللّٰـهِ الرَّحمٰنِ الرَّحيمِ

اِنَّا أَنزَلنٰهُ فى لَيْلَةِ القَدْرِ ﴿١﴾ وَما أَدرىٰكَ ما لَيلَةُ القَدرِ ﴿٢﴾ لَيلَةُ القَدرِ خَيرٌ مِن أَلفِ شَهرٍ ﴿٣﴾ تَنَزَّلُ المَلـٰئِكَةُ وَالرّوحُ فيها بِإِذنِ رَبِّهِم مِن كُلِّ أَمرٍ ﴿٤﴾ سَلـٰمٌ هِىَ حَتّىٰ مَطلَعِ الفَجرِ ﴿٥﴾

Hakika Sisi tuliiteremsha (Qur’an) katika usiku wa Qadar (usiku wenye heshma kubwa). Na jambo gani  litakalokujulisha ni nini usiku wa Qadar? Usiku wa Qadar ni bora kuliko miezi elfu. Malaika na Jibraeel (‘alayhis salaam) huteremka humo kwa idhini ya Mola wao kwa kila amri. Ni (usiku huu) ni Amani; (na) ni mpaka mapambazuko ya alfajiri.

Wafasiri wa Qur-aan Takatifu wanaeleza kwamba sababu ya kuteremshwa Sura hii ni kwamba katika tukio moja, Rasulullah sallallahu  alaihi  wasallam aliwafahamisha maswahaabah (Radhiya Allaahu ‘anhum) kuhusu mujaahid fulani miongoni mwa Bani Israaeel ambaye alipigana katika Jihaad kwa miezi elfu. Maswahabah (Radhiya Allaahu ‘anhum) waliposikia kuhusu jitihada ya mtu huyu, walishangaa na kuonyesha tamani juu ya hili.

Hapo Allah ta’ala akateremsha surah hii kama zawadi na fadhila kwa umma huu. Fadhila makhsusi iliyotajwa katika surah hii ni kwamba mtu yoyote katika ummah huu atakayemuabudu Allah Taala katika usiku huu wa Qadr, atajipatia ujira wa kumuabudu Allah Taala kwa zaidi ya miezi elfu moja na miezi elfu ni sawa sawa na miaka thamanini na tatu!

اِنَّا أَنزَلنٰهُ فى لَيْلَةِ القَدْرِ ﴿١﴾

Hakika Sisi tuliiteremsha (Qur-aan) katika usiku wa Qadar (usiku wa heshma kubwa).

Katika aya hii, Allah Ta‘ala anaeleza kwamba Aliiteremsha Qur-aan takatifu katika usiku wa Qadr. Hadithi zingine zinaeleza kwamba Qur-aan  iliteremshwa kwa Rasulullah sallallahu  alaihi  wasallam kwa muda wa miaka ishirini na tatu.

Wafasiri wa Qur-aan Takatifu wanaeleza kwamba Qur-aan iliteremshwa mara ya kwanza kutoka Lowh-ul-Mahfoudh hadi mbingu ya kwanza katika mwezi wa Ramadhaan katika usiku wa Qadr. Baada ya hapo, Quraan yote iliteremshwa kutoka mbingu ya kwanza juu ya Nabii wa Allah sallallahu  alaihi  wasallam kwa muda wa miaka ishirini na tatu.

وَما أَدرىٰكَ ما لَيلَةُ القَدرِ ﴿٢﴾ لَيلَةُ القَدرِ خَيرٌ مِن أَلفِ شَهرٍ ﴿٣﴾

Na jambo gani litakalokujulisha ni nini usiku wa Qadar? Usiku wa Qadar ni bora kuliko miezi elfu.

Usiku huu unajulikana kama usiku wa Qadr. Maana moja ya ‘Qadr’ ni heshima na. Sababu ya usiku huu kupewa cheo hiki ni kuwa ni sababu ya Ummah huu kupata heshima mbele ya Allah Ta‘ala. Kwa hiyo, kila mtu anapaswa kujitahidi kumuabudu Allah Ta’ala katika usiku huu na kupata baraka kubwa za usiku huu. Hata kama mtu ni faasiq mkubwa na amejidhalilisha kwa kufanya madhambi, usiku huu unampa fursa ya dhahabu ya kujirudisha kwenye nafasi ya heshima na utukufu kwa kuomba msamaha kwa Allah Taala kwa makosa yake pamoja na kujishughulisha na ibada ya Allah Ta’ala katika usiku huu uliobarikiwa.

وَما أَدرىٰكَ ما لَيلَةُ القَدرِ ﴿٢﴾ لَيلَةُ القَدرِ خَيرٌ مِن أَلفِ شَهرٍ ﴿٣﴾

Na jambo gani litakalokujulisha ni nini usiku wa Qadar? Usiku wa Qadar ni bora kuliko miezi elfu.

Wafasiri wa Qur-aan Takatifu wanaeleza kwamba maana nyingine ya ‘Qadr’ ni Taqdir (kudra na amri ya Allah Ta’ala). Usiku huu pia unaitwa usiku wa Qadr (usiku wa kudra na amri) kwa sababu ni katika usiku huu ambapo huteremshwa amri ya Allah Ta’ala kuhusu Taqdir ya viumbe kwa Malaika. Malaika wanafahamishwa ni nani atakayezaliwa na nani atafariki katika mwaka huo pamoja na vipimo vya rizqi ambazo Allah Ta‘ala atamteremshia kila mtu.

Ijapokuwa kuna riwaya mbili kuhusiana na taqdir ya viumbe;

Riwaya moja inaeleza kwamba Taqdir yanateremshwa kwa Malaika katika Laylatul Baraa’ah, usiku wa 15 wa Sha’baan, na riwaya ya pili inaeleza kwamba majaaliwa yanateremshwa kwa Malaika kwenye usiku ya Laylatul Qadr – riwaya hizi zote mbili ziko sahihi.

Maulamaa wameafikiana baina ya riwaya zote mbili kwa kueleza kwamba katika usiku wa 15 wa Sha’baan, unaojulikana kwa jina la Laylatul Baraa’ah, Malaika wanafahamishwa kuhusiana na mambo mbalimbali ambayo yameandikwa kufanyika mwaka unaofuata. Kwa mfano, amri imepitishwa kuhusu nani ataishi na nani atakufa, ni rizqi ngapi itatolewa kwa kila mtu, ni mtu gani atabarikiwa na fursa ya Hijja na Umra n.k. Vile vile, maelezo mengine yote yanayohusiana na wanadamu yameandikwa na kukadiriwa katika usiku huu wa Baraa’ah na Malaika wanajulishwa kuhusiana na maamuzi haya.

Baada ya hapo, katika usiku wa Qadr, maamuzi yote ambayo yameandikwa kufanyika katika usiku wa Baraa’ah basi hufikishwa kwa Malaika ili watekeleze maamrisho ya Allah Ta‘ala.

 تَنَزَّلُ المَلـٰئِكَةُ وَالرّوحُ فيها بِإِذنِ رَبِّهِم مِن كُلِّ أَمرٍ ﴿٤﴾ سَلـٰمٌ هِىَ حَتّىٰ مَطلَعِ الفَجرِ ﴿٥﴾

Malaika na Jibraeel (‘alaihis salaam) huteremka humo kwa idhini ya Mola wao kwa kila amri. Ni (usiku huu) ni Amani; (na) ni mpaka mapambazuko ya alfajiri.

Katika usiku huu, neema ya ziada na baraka za Allah Ta‘ala ni kwamba Jibraeel (‘Alaihis Salaam) anashuka kutoka Sidratul Muntaha pamoja na Malaika wote. Sidratul Muntaha inaelezeka kuwa ni kituo cha mwisho ambacho Malaika wanaweza kupaa mbinguni. Anaposhuka Jibraeel (‘Alaihis Salaam) na Malaika wengine katika ardhi usiku huu, wanamsalimu kila Muislamu, mwanaume na mwanamke.

Imepokewa kutoka kwa Abullah bin Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasulullah… amesema kwamba Malaika wote walioko Sidratul Muntaha wanateremka kutoka mbinguni kwenda ardhini pamoja na Jibraeel (‘Alaihis Salaam) na wanamsalimu kila Muumini wa kiume na wakike. Lakini, wamalaika huwa hawasalimu wale wanaokunywa pombe au kula nguruwe.

Wale wanaosimama katika ibaada katika usiku huu hakika wamebarikiwa na ni wenye bahati Sana. Malaika wanaoshuka kutoka mbinguni wanakuwa wanawaombea du’aa kwa Allah Ta’ala awamiminie neema na rehema zake makhsusi. Zaidi ya hayo, Allah Ta’ala anawasamehe madhambi yao zote madogo yaliyotangulia. Abu Hurairah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ameripoti kuwa Rasulullah… amesema: “Mwenye kusimama katika ibada ya usiku wa Qadr kwa Imaani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake zote yaliyopita.”

Riwaya nyingine inataja kuwa ulipoanza mwezi wa Ramadhaan, Rasulullah… aliwahutubia maSwahaabah (Radhiya Allaahu ‘anhum) akisema: “Hakika mwezi huu (wa Ramadhaan) umewakujieni, na ndani yake mna usiku mkubwa zaidi na bora kuliko miezi elfu moja. Mwenye kunyimwa usiku huu hakika amenyimwa kheri zote, na ni wale walionyimwa kwa hakika ndio watakaonyimwa kheri ya usiku huu.”

Hivyo basi, katika usiku huu wa baraka mtu ahakikishe anajishughulisha na ibaada na kujiepusha na aina zote za madhambi. Mtu anatakiwa pia kujishughulisha na du‘aa nyingi na kumuomba Allah Ta’ala amsamehe madhambi zake na ambariki kwa rehema zake maalum.

 

 تَنَزَّلُ المَلـٰئِكَةُ وَالرّوحُ فيها بِإِذنِ رَبِّهِم مِن كُلِّ أَمرٍ ﴿٤﴾ سَلـٰمٌ هِىَ حَتّىٰ مَطلَعِ الفَجرِ ﴿٥﴾

Malaika na Jibraeel (‘alaihis salaam) huteremka humo kwa idhini ya Mola wao kwa kila amri. Ni (usiku huu) ni Amani; (na) ni mpaka mapambazuko ya alfajiri.

Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliwahi kumwambia Rasulullah (radhiyallahu ‘anha), “Ewe Rasulullah (sallahu ‘alaihi wasallam) ! Nikiupata usiku huu wa Qadr basi niombe du’aa gani?” Rasulullah (sallahu ‘alaihi wasallam) akajibu kwa kutaja du’aa:

اَللّٰهُمَّ إِنَّكَ عَفُوٌّ تُحِبُّ الْعَفْوَ فَاعْف عَنِّيْ

Ewe Allah! Wewe ni mwingi wa kusamehe, na unapenda kusamehe, basi nisamehe!

Kupitia du’aa hii, Rasulullah (sallahu ‘alaihi wasallam) aliufundisha ummah daima kurejea kwa Allah Ta’ala kwa kutubia dhambi zao, na kwa vyovyote vile wasijisikie kuwa wao hawana dhambi na hawana makosa.

Ijapokuwa tarehe kamili ya Laylatul Qadr haijafafanuliwa kwa Ummah, Rasulullah (sallahu ‘alaihi wasallam) aliuusia ummah watafute Laylatul Qadr katika mwezi wa Ramadhaan. Katika baadhi ya Hadithi, imeandikwa kwamba Rasulullah (sallahu ‘alaihi wasallam) alisema, “Tafuteni Laylatul Qadr katika kumi la mwisho la Ramadhaan,” na katika hadithi zingine, Rasulullah (sallahu ‘alaihi wasallam) amesema: “Tafuteni Laylatul Qadr katika siku zenye hazigawaniki kwenye kumi la mwisho wa Ramadhaan.” Maulamaa wanaeleza kwamba Laylatul Qadr inaweza kutokea katika siku yoyote ya mwezi wa Ramadhani.

Hata hivyo, mara nyingi hutokea katika usiku kumi za mwisho za mwezi wa Ramadhani katika usiku usio gawanika.

About admin

Check Also

Tafseer Ya Surah Lahab

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ تَبَّتْ يَدَا أَبِي لَهَبٍ وَتَبَّ ‎﴿١﴾‏ مَا أَغْنَىٰ عَنْهُ مَالُهُ وَمَا كَسَبَ ‎﴿٢﴾‏ سَيَصْلَىٰ نَارًا …