Miongoni mwa neema kubwa za Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aalah) juu ya mtu ni neema ya wazazi. Neema ya wazazi ni neema yenye thamani sana na isiyoweza kubadilishwa hadi kwamba inapewa kwa mtu mara moja tu katika maisha yake.
Kama vile neema za zingine za maisha inatolewa mara moja tu kwa mtu, na itakapoisha, haitarudi tena, hivyo ndivyo neema ya wazazi pia ipo, ikichukuliwa, haiwezi kupatikana tena.
Kila neema ambayo mtu anafurahia ina haki fulani zinazohusiana nayo. Iwapo fadhila za wazazi ni miongoni mwa neema kubwa, basi haki zinazoambatanishwa nayo ni miongoni mwa haki muhimu sana katika dini.
Ndani ya Quran Majeed na Hadith za mtume (sallallahu alaihi wasallam) zimejaa maamrisho kuhusu umuhimu mkubwa wa
kutimiza haki za wazazi na kuwatendea wema wa hali ya juu.
Katika Qur’aan Majeed, Allah Ta’ala Anasema:
وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۚ إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا ﴿٢٣﴾
Mola wako amefaradhisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na muwatendee wema wazazi wawili. Ikiwa mmoja wao au wote wawili watafikia uzee, usimwambie “Uff (neno au maneno ya hasira au maneno ya kukera)” na usiwakemee, na uongee nao kwa maneno ya heshima.
Imepokewa katika Hadith kwamba radhi za Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) ziko katika radhi za wazazi, na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) iko katika kuwachukiza wazazi.
Wazazi Wako Ni Pepo Au Jahannum Yako
Wakati fulani, Sahaabi alimuuliza Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) kuhusu haki za wazazi. Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) akasema: “Hao (wazazi) ni Pepo yako au Jahannamu yako.”
Kwa maneno mengine, ikiwa mtu ni mpole, mwenye huruma na upendo kwa wazazi wake na kuwatii katika mambo yote yanayoruhusiwa, atabarikiwa na Jannah. Kinyume chake, ikiwa atawaasi na akawa mkali na mkorofi kwao, basi matendo yake mabaya yatakuwa sababu ya yeye kuingia katika moto wa Jahannamu.
Milango Miwili Ya Jannah Ikibaki wazi
Katika Hadith nyingine, Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) amesema: “Muislamu yoyote atakaepitisha siku yake katika hali ya kuwa wazazi wake wameridhika naye (yaani anamtii Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) katika kutekeleza haki za wazazi wake), basi milango miwili ya Jannah itafunguliwa kwa ajili yake. Ikiwa ana mzazi mmoja tu aliye hai, basi mlango mmoja tu utakuwa wazi kwa ajili yake.
“Muislamu yoyote anayepitisha siku yake katika hali ya kuwa wazazi wake wamemkasirikia (yaani kumuasi Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) katika kutekeleza haki za wazazi wake), basi milango miwili ya Jahannam yatafunguliwa kwa ajili yake. Ikiwa ana mzazi mmoja tu aliye hai, basi mlango mmoja tu utakuwa wazi kwa ajili yake.”
Tukio La Mwanaume Kumbeba Mama Yake Wakati Wa Kufanya Thawaaf
Imepokewa kwamba katika tukio moja, Abdullah bin Umar (radhiyallahu anhuma) alikuwa akifanya thawaaf alipomuona mtu kutoka Yemen akiwa amembeba mama yake mgongoni huku akifanya thawaaf.
Mwanaume huyo akiwa amembeba, alikuwa akitamka maneno yafuatayo kama mashairi:
Mimi ni ngamia wake mtiifu. Usafiri mwingine wowote ambao anaweza kupanda unaweza kumuogopesha, lakini kamwe sitamsababishia hofu yoyote (yaani, sitamsababishia usumbufu wowote). Sasa nimembeba mgongoni, lakini kipindi alichonibeba tumboni mwake kilikuwa kirefu zaidi.
Baada ya kumaliza thawaaf, mtu huyo alimuuliza Ibnu Umar (radhiyallahu anhuma), “Je, nimetimiza haki ya mama yangu kwa kumbeba wakati wa thawaaf?”
Ibnu Umar (radhiyallahu anhuma) akajibu, “Hapana! Kwa kweli, hujamlipa hata dakika moja ya maumivu aliyopata wakati wa kukuzaa wewe.”
Utiifu na huduma kwa wazazi ni njia inayoelekea Jannah. Kuona faraja ya wazazi, kuwatimizia haja zao na kuwaonyesha upendo na heshima wanayostahiki ni ibaadah kubwa inayompa mtu thawabu kubwa katika dunia hii na ijayo.