Tafseer Ya Surah Nasr

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

إِذَا جَاءَ نَصْرُ اللَّهِ والْفَتْحُ ‎﴿١﴾‏ وَرَأَيْتَ النَّاسَ يَدْخُلُونَ فِي دِينِ اللَّهِ أَفْوَاجًا ‎﴿٢﴾‏ فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَاسْتَغْفِرْهُ ۚ إِنَّهُ كَانَ تَوَّابًا ‎﴿٣﴾‏

(Ewe Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam)) Itakapokuja nusura ya Allah Ta’ala na ushindi (utekaji wa Makka Mukarramah) na ukawaona watu wanaingia katika Dini ya Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) kwa wingi, basi mtakase Mola wako na umuombe msamaha, hakika Yeye ndiye mwingi wa kusamehe.

Katika maisha yote ya Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam), makafiri walijitahidi kumpinga na kukatisha kazi yake. Usiku na mchana walikua wakipanga njama za kuwadhuru Waislamu na kuuondoa Uislamu katika uso wa dunia hii.

Kabla ya hijra kuelekea Madinah Munawwarah, Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) na Maswahabah (Radhiya Allaahu ‘anhum) walipitia mateso makali kutoka kwa makafiri.

Baada ya hijra kwenda Madinah Munawwarah pia, juhudi zao hazikupungua, bali ziliendelea kuongezeka mpaka vita vingi vikatokea baina ya Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) na Maquraishi.

Kisha ukaja wakati ambapo Allah Ta‘ala alimpa Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) ushindi na Fath-ul-Makkah (ushinda wa utekaji wa Makka Mukarramah) kulifanyika.

Ushindi wakuteka Makkah Mukarramah ulikuwa kama kilele cha juhudi za maisha ya Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam). Ilikuwa ni wakati ambapo Allah Ta’ala alimuonyesha Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) na maswahaabah wake (Radhiya Allaahu ‘anhum) matunda ya juhudi zao yanadhihirika na utukufu wa Uislamu unadhihirika duniani.

Kwa mujibu wa mufassireen, surah hii iliteremshwa katika mwaka wa 8 wa hijra muda mfupi kabla ya Fath-ul-Makkah (ushindi wa utekaji wa Makka Mukarramah), takriban miaka miwili na nusu kabla ya Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) kuondoka duniani.

Katika surah hii, Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alipewa bashara kwamba hivi karibuni Makka Mukarramah itatekwa na kwamba makabila mengi yatasilimu.

Surah Faatihah ilikuwa surah ya kwanza kamili kuteremshwa ndani ya Qur’an Takatifu, ingawa kulikuwa na aya fulani ambazo ziliteremshwa kabla yake (k.m. Aya za mwanzo za Surah ‘Alaq na aya za mwanzo za Surah Muddathir).

Alafu Sura hii (Surah Nasr), ilikuwa ni surah ya mwisho kamili ya Qur’an Takatifu kuteremshwa, ingawa kulikuwa na Aya fulani zilizoteremshwa baada yake.

Mufasirin (wanazuoni wa tafseer) wanaeleza kuwa miongoni mwa aya zilizoteremshwa baada ya Sura hii ni Aya zifuatazo:

1) Aya (الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ) “Leo nimekukamilishieni Dini yenu”.

Aayah hii iliteremshwa kwa Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam ) kwenye uwanja wa Arafaat, siku ya Jumuah, tarehe 9 Dhul Hijjah, takriban siku themanini kabla ya kufariki kwa Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam).

2) Aya ya kalaalah iliyohusu urithi. Aya hii iliteremka takriban siku hamsini kabla ya Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) kuondoka hapa duniani.

3) Aya ya pili ya mwisho kuteremka ni Aya ya mwisho ya Sura Taubah yaani (لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ) “Amekujieni Rasul kutoka miongoni mwenu”.

Aya hii iliteremka takriban siku thelathini na tano kabla ya Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) kuondoka duniani.

4) Aya ya mwisho kuteremshwa ilikuwa) (وَاتَّقُوا يَوْمًا تُرْجَعُونَ فِيهِ إِلَى اللَّـهِ) “ogopeni siku ambayo mtarudishwa kwa Allah Ta’ala. (Sura Baqarah: 281)

Aya hii iliteremka takriban siku ishirini na moja (na kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, siku saba) kabla ya Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) kuondoka hapa duniani.

وَرَأَيْتَ النَّاسَ يَدْخُلُونَ فِي دِينِ اللَّهِ أَفْوَاجًا ‎﴿٢﴾

Na utawaona watu wanaingia katika Dini ya Mwenyezi Mungu(subhaanahu wata’aala) kwa wingi.

Hadi mpaka ushidi wa Makka Mukarramah, makabila mengi walikuwa wakingoja kuona majibu ya Maquraishi. Sababu ni kwamba Maquraishi walichukuliwa kama kabila lenye heshima kubwa miongoni mwa Waarabu wote. Kwa hiyo, Waarabu wengine waliosalia walisubiri kuona watakachofanya.

Hivyo, katika kutekwa kwa Makka Mukarramah, baada ya Maquraish kuukubali Uislamu, makabila mengi yalianza kuingia katika kundi la Uislamu kwa wingi.

Imepokewa kuwa wakati mmoja, watu mia saba waliingia Madinah Munawwarah kusilimu na kutangaza shahaadah zao. Watu kutoka nchi mbalimbali walituma wajumbe wao Madinah Munawwarah kusilimu na kutangaza shahaadah.

 فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَاسْتَغْفِرْهُ ۚ 

Basi mtakase Mola wako na umuombe msamaha, hakika Yeye ndiye mwingi wa kusamehe.

Katika aya hii, Allah Ta’ala anamfahamisha Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) kwamba anapowaona watu wanaingia katika Dini ya Allah Ta’ala kwa wingi, basi amtukuze Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) na amwombe maghfirah. Dhamira yake inakaribia kukamilika na wakati wake kuondoka duniani kunakaribia.

Uislamu unatufundisha kwamba maisha ambayo mtu anapewa na Allah Ta’ala si kwa ajili ya yeye kujipatia sifa, umaarufu wa kidunia au kuonyesha uwezo wake kwa watu kama inavyokuwa katika zama hizi.

Bali neema ya maisha mtu anayopewa ni kwa ajili ya kuonyesha unyenyekevu mbele ya Allah Ta‘ala huku akiishi maisha ya uchamungu na uadilifu na kuonyesha wema, huduma na huruma kwa viumbe.

Hatupaswi kuwa wabinafsi na wala hatupaswi kujihusisha na wema. Bali tunapaswa kuhusisha wema wote na kila mafanikio za neema na utukufu kwa Allah Ta’ala peke yake.

Katika tukio hili la Fath-ul-Makkah, Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alipokuwa kwenye kilele cha utukufu na uwezo, alionyesha unyenyekevu mkubwa zaidi mbele ya Allah Ta’ala na akahusisha ushindi wote kwa Allah Ta’ala pekee.

Mshairi anaeleza namna Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alivyoingia Makka Mukarramah kama kiongozi mshindi wakati wa Fath-ul-Makkah. Mshairi anasema:

Aliingia Makka Mukarramah kama kiongozi mshindi, akiwa ameinamisha kichwa chake chini na machozi yakimtoka (kwa unyenyekevu na shukurani kwa Allah Ta‘ala). Kisha alitangaza hadharani msamaha wa ujumla na usalama kamili na msamaha kwa watu wote wa Makka Mukarramah, (licha ya kuwa na hatia ya kuwatesa Waislamu kabla ya hili. Walipouona mwenendo wake tukufu) watu wa Makka Mukarramah walijuta na kuona haya (kwa sababu ya matendo yao kabla hili tukio).

Baada ya kuingia Makka Mukarramah, Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alitoa khutbah mbele ya watu wote, na ndani ya khutbah alisoma takbira mara tatu kisha akasoma sifa zifuatazo za Allah Ta’ala:

لَا إِلَهَ إِلَّا الله وَحْدَهُ، صَدَقَ وَعْدَهُ، وَنَصَرَ عَبْدَهُ، وَهَزَمَ الْأَحْزَابَ وَحْدَهُ

Amna mungu apasae kuabudiwa isipokuwa Allah Ta’ala peke yake, ambaye ametekeleza ahadi yake, na akamsaidia mja wake, na akayashinda majeshi Peke Yake.

Mtu anapaswa kujiuliza kuwa mtu anapokuwa kwenye nafasi ya madaraka atakuwa na tabia gani?

Je, atawadharau watu kwa kiburi na dharau, akijiona yeye ni bora kuliko wao, au atawaonea huruma na kuwasamehe kama Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alivyowatendea wale waliomdhulumu yeye na maswahaabah wake (Radhiyallahu ‘anhum)?

Vile vile tunaelewa kutokana na mwenendo wa Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) kwamba hakujinasibisha na ukubwa au ushindi wowote, bali aliuhusisha ukubwa na ushindi kwa Allah Ta’ala peke yake, kwa sababu alifahamu kuwa ni Allah Ta’ala peke yake alileta siku hii ya utukufu, heshima na ushindi kwake.

Kwa maneno mengine, Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) alikuwa akionyesha unyenyekevu wake wa hali ya juu mbele ya Allah Ta’ala, akielewa kuwa sisi ni waja wa mwenyezimungu (subhaanahu wata’aala) tumejaa udhaifu na mapungufu, na ni Allah Ta’ala Pekee ndiye Aliye Mkuu zaidi, mkamilifu na wa milele. Yeye ndiye mkuu na hana dosari wala upungufu kwake.

Hivyo, ili kutangaza ukamilifu wa Allah Ta‘ala, tumeamrishwa kusoma Subhaanallah na Alhamdulillah, na kudhihirisha unyonge na upungufu wetu, tumeamrishwa kusoma istighfaar.

Kwa hivyo, kwa kumhimidi Allah Ta’ala, tunatangaza kwamba Yeye ndiye Kiumbe pekee asiye na dosari na kwamba sifa zote ni Zake peke yake.

Na kwa kusoma istighfaar, tunatangaza kwamba sisi ni waja Wake wenye dhambi, na hivyo tunamwomba msamaha kwa mapungufu na dhambi zetu.

 فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَاسْتَغْفِرْهُ

basi mtakase Mola wako na umuombe msamaha, hakika Yeye ndiye mwingi wa kusamehe.

Kwa vile surah hii inashiria kuwa kazi na lengo la Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) kufikia mwisho na pia inashiria kuwa wakati wa kifo chake kuwa karibu, Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) alielekezwa kujishughulisha na tasbihi (kutamka utakaso wa Allah Ta’ala), tahmeed (kumtakasa Allah Ta‘ala na kumshukuru) na istighfaar (kuomba msamaha kwa Allah Ta’ala).

Tumefunzwa katika Hadith ya baraka kwamba baada ya kukamilisha kazi yoyote nzuri, tunapaswa kumsifu Allah Ta’ala kwa kuikamilisha kazi hiyo, na pia tunapaswa kumuomba msamaha kwa mapungufu na makosa yoyote yaliyotokea kutoka upande wetu wakati wa kufanya kazi hiyo.

Kimsingi, surah hii inamfundisha kila Muislamu kwamba katika kilele cha kila jambo, anatakiwa arejee kwa Allah Ta‘ala kwa kusoma tasbihi, tahmid na istighfaar.

Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa akisema kwamba baada ya kuteremshwa Sura hii, Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alikuwa akisoma dhikr (sifa za Allah Ta’ala) ifuatayo mara kwa mara:

سُبحَانَ اللهِ وَبِحَمْدِهِ أَسْتَغْفِرُ اللهَ وَأَتُوْبُ إِلَيْهِ

Imepokewa katika Hadith kwamba dhikr (سُبحَانَ اللهِ وَبِحَمْدِهِ سُبحَانَ اللهِ العَظِيم) itakuwa na uzito mkubwa katika mizani Siku ya Qiyaamah.

Kwa hivyo, tunapaswa kuchukua muda fulani kila siku kusoma dhikr hii.

Vile vile Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) naye alikua akisoma dhikr ifuatayo (أَسْتَغْفِرُ اللهَ وَأَتُوْبُ إِلَيْهِ).

Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) anaripoti kwamba baada ya kuteremshwa Sura hii, Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alikuwa akisoma سُبحَانَ اللهِ وَبِحَمْدِكَ أَسْتَغِفُرُ الله katika Rukuu yake na Sajdah wakati wa kuswali.

Katika Hadith moja, Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) ametaja: “Bashara njema ziwe kwa mtu ambaye ana istighfaar nyingi katika kitabu chake cha matendo.”

Katika Hadith hii, bashara njema imetolewa kwa mtu ambaye hutubu daima na kuomba msamaha kwa Allah Ta’ala.

Kwa hiyo, badala ya mtu kujiamini kupita kiasi na kuridhika na mema anayoyafanya, basi adhihirishe upungufu na udhaifu wake mbele ya Allah Taala, na afidia udhaifu wake kwa kuendelea kuomba msamaha kwa Allah Taala.

About admin

Check Also

Tafseer Ya Surah Lahab

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ تَبَّتْ يَدَا أَبِي لَهَبٍ وَتَبَّ ‎﴿١﴾‏ مَا أَغْنَىٰ عَنْهُ مَالُهُ وَمَا كَسَبَ ‎﴿٢﴾‏ سَيَصْلَىٰ نَارًا …