binary comment

Tafseer Ya Surah Kaafiroon

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ ‎﴿١﴾‏ لَا أَعْبُدُ مَا تَعْبُدُونَ ‎﴿٢﴾‏ وَلَا أَنتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ ‎﴿٣﴾‏ وَلَا أَنَا عَابِدٌ مَّا عَبَدتُّمْ ‎﴿٤﴾‏ وَلَا أَنتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ ‎﴿٥﴾‏ لَكُمْ دِينُكُمْ وَلِيَ دِينِ ‎﴿٦﴾‏

Sema: “Enyi makafiri, mimi siabudu (masanamu) mnayoyaabudu, wala nyie hamumuabudu ninayemuabudu (Allah Ta’ala). Na wala sitaabudu (masanamu) mnayoyaabudu, wala nyinyi hamtamwabudu ninayemuabudu (Allah Ta‘ala). Nyinyi mna Dini yenu na mimi nina Dini yangu.”

Sura mbili, Surah Kaafiroon na Surah Ikhlaas, zina umuhimu mkubwa na wema. Nabi (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alikuwa akizisoma Sura hizi mbili katika sunna za Alfajiri na Maghrib. Vile vile amenasihi kuwa Surah Kaafiruon isomwe kila usiku kabla ya kulala, kwa sababu ni tamko la kujitenga na shirki na ukafiri.

Wakati mmoja, Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alin’gatwa na nge. Kisha akasoma Surah Kaafiroon, pamoja na Surah Falaq na Surah Naas, na kwa hayo akapaka maji ya chumvi kwenye eneo alilon’gatwa. Kwa baraka za surah hizi, alipewa shifa.

Sababu ya surah hii kuteremshwa, kama ilivyoripotiwa na ibnu Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma), ni kwamba kuna wakati fulani kundi la Maquraish lilimjia Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) na kumuomba yafuatayo. Wakasema: “Tutakupa mali nyingi na utakuwa tajiri mkubwa zaidi wa Makka Mukarramah, tutakupa mwanamke umtakaye katika ndoa na tutakufuata na kukutii wewe kama kiongozi wetu asiyepingwa, kwa sharti ufanye haya- usiwaseme vibaya mungu zetu (masanamu). Ikiwa aukubaliani na hili, basi tukubaliane kwamba umuabudu mungu wetu kwa mwaka mmoja, na sisi tutamuabudu Mungu wako mwaka ujao.”

Juu ya hili, Jibraeel (‘alayhis salaam) alishuka pamoja na Surah Kaafiroon.

Kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, imetajwa kwamba baadhi ya wapagani wa Makkah Mukarramah walimuomba Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) wafanye suluhu kwa kuabudu mungu wao. Lakini, Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) alikataa. Hapo wakasema, “Ewe Muhammad (Sallallahu ‘alaihi wasallam), ikiwa hutaki kuabudu mungu wetu, basi uguse baadhi ya mungu zetu. Ukiwagusa basi tutakuamini wewe.” Hapo ndipo ilipoteremshwa surah hii.

Kimsingi, makafiri walikuwa wametoa mapendekezo matatu kwa Rasulullah (Sallallahu’alaihi wasallam).

Pendekezo la kwanza lilikuwa kwamba Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) asiwasemi vibaya masanamu yao.

Ikiwa hayupo tayari kwa hili, basi pendekezo la pili ilikuwa kwamba yeye akubali kujumuika ibada yake pamoja na ibada zao na Dini yake pamoja na Dini yao kwa yeye kuabudu mungu wao kwa muda wa mwaka mmoja na wao kumuabudu Allah Ta‘ala kwa mwaka mmoja.

Pendekezo la tatu waliloliweka mbele yake ilikuwa kwamba Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) angalau basi ayaguse masanamu yao ili kuonyesha aina fulani ya heshima kwao. Kwa hiyo, Allah Ta’ala aliteremsha surah hii ili kumkataza Mtume (Sallallahu’alaihi wasallam) kupokea mapendekezo yao yoyote.

Tangazo la wazi la surah hii

Sura hii ni tamko la wazi kwamba Uislamu hauwezi kuunganishwa au kuchanganywa na dini ya makafiri. Katika surah hii, Allah Ta’ala analaani vitendo vya makafiri kwa uwazi na anawausia Waislamu kumwabudu Allah Ta’ala peke yake kwa namna ambayo hakuna shirki na aina yoyote ya ukafiri.

Sababu ya Allah Ta’ala kumharamishia Rasulullah (Sallallahu’alaihi wasallam) na ummah kukubali mapendekezo ya makafiri ni kwamba Dini ya Uislamu ni Dini safi, na Dini kamilifu kiasi kwamba imeegemezwa kwenye misingi wa Tawhid (umoja wa Allah Taala) na utiifu kwa amri za Allah Ta’ala pekee.

Hivyo basi, Dini hii kamwe haiwezi kuunganishwa na dini nyingine yoyote, kwa sababu kila dini nyingine kasoro Uislamu imeegemezwa juu ya ukafiri na shirki lakini dini ya Kiislamu imeegemezwa juu ya usafi, tawhid (umoja wa Allah Taala) na utii kamili kwa Allah Ta’ala peke yake.

قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ ‎﴿١﴾‏ لَا أَعْبُدُ مَا تَعْبُدُونَ ‎﴿٢﴾‏ وَلَا أَنتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ ‎﴿٣﴾‏ وَلَا أَنَا عَابِدٌ مَّا عَبَدتُّمْ ‎﴿٤﴾‏ وَلَا أَنتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ ‎﴿٥﴾

Sema: “Enyi makafiri, mimi siabudu (masanamu) mnayoyaabudu, wala nyie hamumuabudu ninayemuabudu (Allah Ta’ala). Na wala sitaabudu (masanamu) mnayoyaabudu, wala nyinyi hamtamwabudu ninayemuabudu (Allah Ta‘ala). Nyinyi mna Dini yenu na mimi nina Dini yangu.”

Ukichunguza aya hizi, zinaonekana kama zimerudiwa. Lakini, kuna tofauti kati ya aya mbili za kwanza ikilinganishwa na aya mbili za pili.

Aya mbili za kwanza zinahusu kipindi cha sasa na aya mbili za pili zinahusu kipindi cha baadaye, yaani: kwa sasa, hatuendi kuabudu mnachokiabudu na wala huko mbele hatutaabudu mnachokiabudu. Kwa hivyo, usitaraji sisi kukufuata katika yale unayoyaabudu wakati wowote. Kwa mujibu wa maelezo haya, “maa” katika aya zote nne imetafsiriwa kama “maa mausoola” yaani kitu cha kuabudiwa – tunamuabudu Allah Ta’ala na nyinyi mnaabudu masanamu yenu.

Ufafanuzi wa pili wa aya hizi ambao umetolewa na Allaamah Ibnu Katheer (rahimahullah), ni kwamba ‘maa’ katika Aya mbili za mwanzo itatafsiriwa kama “maa mausoola, na ‘maa’ katika aya mbili za pili imetafsiriwa kuwa “ maa masdariyya”. Kwa hiyo, aya hizi zitatafsiriwa kuwa “Siabudu (masanamu) mnayoyaabudu, wala nyie hamuabudu ninayemuabudu (Allah Ta‘ala). Na wala mimi siabudu kwa namna mnaabudu na wala hamuabudu kwa namna ninayo abudu.”

Kwa maneno mengine, kwa mujibu wa maelezo haya, aya mbili za kwanza zinaonyesha kwamba lengo la ibada yetu na ibada yako ni tofauti. Tunamuabudu Allah Ta’ala na nyinyi mnaabudu mungu zenu. Mistari miwili ya pili inaonyesha kwamba sisi ni tofauti katika namna ya ibada yetu yaani: njia zetu za ibada ni tofauti kabisa na ni nguzo tofauti kutoka kwa kila mmoja. Ikiwa unatamani kubaki kwenye njia yako ya uwongo, basi usitarajie mimi kuhama kutoka kwenye njia ya haq na kuendana na njia yenu mbaya za ibada, na wala sitarajii wewe kuendana na njia zangu za ibada. Hakuna upatanisho kati ya njia zetu za kuabudu kwa sababu zote mbili ni tofauti kabisa kutoka kwa kila mmoja.

Kimsingi, aya hizi zinaashiria kwamba njia ya Uislamu ni njia ya usafi na uadilifu, njia ya kuamini na kumwabudu Allah Ta‘ala pekee na kutii na kusalimu amri anazozitoa peke yake bila ya upotofu wowote. Kinyume chake, njia ya shirki na kukufuru inapingana kabisa na njia ya Uislamu kwa sababu inadai kukubali kila kitu badala ya Allah Taala. Kwa hiyo, Muislamu na asiyekuwa Muislamu wako kwenye njia mbali mbali tofauti kwa kila jambo na Mwislamu kamwe hawezi kuwafuata wasio Waislamu katika matendo yao ya ibada, desturi, kafara, mitindo, sherehe, mienendo ya biashara na mitindo ya maisha.

Sura hii inafikisha asili ya tawhiyd na kunyenyekea kwa maamrisho ya Allah Ta‘ala pekee na umuhimu kwa Muumini kuonyesha utiifu usio na shaka katika nyanja zote za maisha yake ya kidunia na dini. Muumini si kama kafiri anayeenda na wakati na kubadilika na tukio. Bali, katika hali na hali zote, Muumini hubakia kuwa mwaminifu kwa Allah Ta’ala. Haijalishi ni saa ngapi ndani ya mwaka na anaishi katika mazingira gani, kama yuko katika mji wake wa asili au nje ya mji ndani ya likizo, iwe katika maisha yake ya nyumbani, maisha ya kijamii au katika shughuli zake za kibiashara – yeye hubakia thabiti katika dini kila wakati kwa sababu ya yeye kufahamu kwamba ataulizwa mbele ya Allah Ta’ala.

Yeye hayumbishwi na mila na desturi za makafiri wakati wowote, bali hutangaza maadili ya kweli ya Uislamu popote anapokwenda na yoyote anayekutana naye. Hali hii ndiyo iliyopatikana miongoni mwa Maswahaba ndiyo iliyowafanya kufanikiwa popote pale walipokwenda duniani na kuzifanya nyoyo za watu kuvutiwa na Uislamu kwa kukutana nao tu.

 لَكُمْ دِينُكُمْ وَلِيَ دِينِ ‎﴿٦﴾‏

Nyinyi mna dini yenu na mimi nina dini yangu.

Deen inaweza kutafsiriwa kwa njia tofauti. Tafsiri moja ya “Dini” ni dini – kama alivyopendelea Imamu Bukhaari (rahimahullah). Kwa hiyo, tafsiri ya aya hiyo ni, “Nyinyi mna dini yenu na mimi nina dini yangu.”

Tafsiri nyingine ya dini ni ‘njia’. Kwa hiyo, tafsiri ya aya hiyo ni, “Nyinyi mna njia yenu na mimi nina njia yangu”.

Kwa maneno mengine, itabidi ubebe matokeo ya matendo yako na nitafurahia matokeo ya matendo yangu.

Kuwa Na Marafiki Makafiri

Funzo moja muhimu tunalopata kutoka surah hii ni kwamba Muumini hatakiwi kupinda kanuni zozote za Dini ili kuwaridhisha makafiri. Ni kwa sababu hii kwamba Aya nyingi za Qur’an Takatifu, Allah Ta‘ala ametukataza kuwafanya makafiri marafiki.

Allah Ta’ala Anasema katika Qur’an Takatifu:

يَا أَيُّهَا الَّذِيْنَ آمَنُوْا لَا تَتَّخِذُوْا الْكٰفِرِينَ أَوْلِيَاءَ مِنْ دُوْنِ الْمُؤْمِنِيْنَ أَتُرِيْدُوْنَ أَنْ تَجْعَلُوْا للهِ عَلَيْكُمْ سُلْطَانًا مُّبِيْنًا

Enyi mlio amini! Msiwafanye makafiri kuwa ni marafiki badala ya Waumini. (Sura Nisaa aya 144)

Katika aya nyingine, Allah Ta’ala Anasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِيْنَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوْا الْيَهُوْدَ وَالنَّصٰرٰى أَوْلِيَاءَ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ وَمَنْ يَتَوَلَّهُم مِّنكُمْ فَإِنَّهُ مِنْهُمْ إِنَّ اللهَ لَا يَهْدِيْ الْقَوْمَ الظّٰلِمِينَ

Enyi mlio amini! Msiwafanye Mayahudi na Wakristo kuwa marafiki! Ni marafiki wao kwa wao. Na atakaye wafanya urafiki nao miongoni mwenu, basi atakuwa miongoni mwao. Hakika Allah Ta’ala hawaongoi watu madhalimu kwenye njia iliyonyooka. (Surah Maa’idah aya 51)

Kutokana na aya hizi mbili, tunaelewa kwamba kuwachukua makafiri kama marafiki kumekatazwa sana katika Uislamu. Vile vile, katika Hadith, Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) ameamrisha kwa uthabiti kwamba waumini washirikiane na waumini tu.

Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) aliwaambia maswahaabah:

لا تصاحب إلا مؤمنا

Usimfanye mtu yoyote kuwa rafiki isipokuwa muumin. (Sunan Abu Dawood #4832)

Sababu ya Shari’ah kuwakataza waumini kufanya urafiki na makafiri ni kwamba mara tu waumini watakapowafanya makafiri kuwa marafiki, mara kwa mara wataanza kuwaiga katika njia zao, mavazi, mtazamo, utamaduni na maadili.

Haya mwishoni yatasababisha kughafilika au kuregea kwenye wajibu wao ambao wanadaiwa na Allah Ta’ala na waumini wengine.

Mara tu waumini wanapokuwa na mwelekeo kama yao na utamaduni wao, basi wataanza kuishi kama wao na kudhania maadili yao, na mwishoni hadi wataacha utamaduni na maadili yao ya Kiislamu.

Ikumbukwe kwamba ingawa tumekatazwa kuwafanya makafiri kuwa marafiki, tumeamrishwa kuwa wapole na wenye kujali kwao. Vile vile, tunaruhusiwa kushughulika nao katika biashara, nk. kwa sharti tusiwe karibu nao na kuamiliana kwetu nao kubaki ndani ya vigezo vya Shari‘ah.

Kimsingi, hatutawabania haki zao, lakini wakati huo huo, hatutaathiriwa na njia na utamaduni wao na kuanza kupindisha dini yetu.

About admin

Check Also

Tafseer Ya Surah Ikhlaas

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ ‎﴿١﴾‏ اللَّهُ الصَّمَدُ ‎﴿٢﴾‏ لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ ‎﴿٣﴾‏ وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا …