Tafseer Ya Surah Kauthar

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ ‎﴿١﴾‏ فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ ‎﴿٢﴾‏ إِنَّ شَانِئَكَ هُوَ الْأَبْتَرُ ‎﴿٣﴾‏

Hakika Sisi tumekuruzuku (na tukakubariki kwa) kheri nyingi. Basi sali kwa Mola wako, na uchinje. Hakika, anayekuchukia atakatiliwa mbali.

Katika sura hii, Allah Ta’ala anazungumza na Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam ) akisema: “Hakika sisi tumekuruzuku (na tumekubariki kwa) kheri nyingi.”

Mema na kheri nyingi aliyobarikiwa nazo Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam ) katika dunia hii yanaonekana kupitia jina lake la baraka na heshima yake kuinuliwa, Dini yake kuendelea kustawi na kuimarika zaidi, na idadi ya watu wanaoingia katika Dini ya Allah Ta’ala unaongezeka siku kwa siku.

Imekuwa zaidi ya miaka 1400 tangu zama za nubuwwah, na bado kwa kupita kila siku, idadi ya Uislamu unazidi kwa kasi. Haya yote ni miongoni mwa kheri nyingi ambazo Allah Ta’ala amempa Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) hapa duniani.

Zaidi ya hayo, huko Akhera, Allah Ta’ala amembariki Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) kwa wingi wa kheri kwa njia ambayo Ummah wake utakuwa mkubwa zaidi kuliko umma wote. Kwa hakika, Ummah wake utazidi umma wote kwa pamoja.

Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam ) ametaja kuwa watu wa Jannah watakuwa katika safa 120, na miongoni mwa safa 120, safa 80 watatoka katika umma wa Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam). Kwa maneno mengine, umma wa Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam ) utakuwa thuluthi mbili ya watu wote wa Jannah.

Mbali na heshima hii, Allah Ta’ala pia atambariki Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam ) kwa nafasi ya juu ya Maqaam-ul-Mahmood.

Maqaam-ul-Mahmood ni nafasi ambayo Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) atapewa pekee ambapo atabarikiwa na heshima ya kumuomba Allah Ta’ala shafaa’a kwa niaba ya wanadamu wote ili Allah Ta’ala aanze hesabu Siku ya Qiyaamah.

Vile vile Allah Ta‘ala amempa Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) heshima ya kuwa kiongozi wa Manabii na Mitume wote. Kwa hivyo, Siku ya Qiyaamah, Manabii na Mitume wote watakuwa nyuma ya bendera ya Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) wakati Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) atakapo waombea wanadamu wote kwa Allah Ta’ala.

Kuhusiana na hilo, Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) amesema: “Mimi ni kiongozi wa kizazi cha Nabii Aadam ( ́alayhis-Salaam), na Siku ya Qiyaamah itakuwa mkononi mwangu bendera ya sifa zote, na nyuma yangu atakuwepo Nabi Aadam (alayhis salaam) na kizazi chake chote.”

Pia katika wingi wa wema ambao Allah Ta’ala amembariki nao Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) ni chemchemi ya Kauthar huko Akhera. Rasulullah (sallallahu’alaihi wasallam) ataunywesha ummah wake maji kutoka kwenye chemchemi yake ya Kauthar.

Katika aya hii, Allah Ta’ala anasema: “Hakika sisi tumekuruzuku (na tumekubariki na) Kauthar (mema nyingi).” Neno ‘Kauthar’ kihalisi linamaanisha ‘mema nyingi’. Kwa hiyo, chemchemi hii ya Kauthar pia ni miongoni mwa wema ambao Allah Ta’ala amembariki nao Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam).

Siku ya Qiyaamah watu wa Ummah wake watakuja mbele yake na atawanywesha maji ya Kauthar ambayo yatakuwa meupe kuliko maziwa na matamu kuliko asali. Imepokewa katika Hadithi kwamba vyombo vya chemchemi yake ya Kauthar vitakuwa vingi kama idadi ya nyota angani. Wale ambao watabarikiwa kunywa maji kutoka katika mikono yake ya baraka kwenye chemchemi yake ya Kauthar hawatapata kiu baada ya hapo kamwe. (Saheeh Muslim #2300)

Kwa hio, kutakuwa na baadhi ya watu ambao Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) aliwachukulia kuwa ni katika Ummah wake, lakini Siku ya Qiyaamah, Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam ) atawakuta Malaika wanawaepusha na chemchem yake. na kuwanyima heshima yakunywa kutoka kwa mikono yake iliyobarikiwa.

Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) atawaambia Malaika: “Kwa nini mnawazuia wasije kwangu na hali wao ni miongoni wa Ummah wangu?” Malaika watajibu wakisema, “Hujui walilofanya baada ya wewe kuondoka duniani. Watu hawa walikuwa wameasi na kujitenga na Uislamu.”

Kwa maneno mengine, wakati wa uhai wa Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam), walikuwa wameonyesha kujitolea kwa Uislamu, lakini baadaye, walikuwa wamejitenga na Uislamu.

Allah Ta’ala atulinde sote tusiwe na kundi hili la watu!

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ ‎﴿٢﴾

Basi mswalie Mola wako, na uchinje.

Katika aya hiyo hapo juu, Allah Ta’ala anamfahamisha Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) kuhusu neema na fadhila nyingi ambazo Allah Ta’ala amemruzuku.

Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) alipewa fadhila kubwa na nyingi sana ambazo hakuna mwanadamu yoyote aliyebarikiwa nazo. Hivyo, katika aya hii, Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) anaambiwa kwamba, kwa kumshukuru Mola wake, anapaswa kurejea kwa Allah Ta’ala katika Swalaah na pia kujitolea.

Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) jinsi kajaaliwa neema hizi kubwa, basi sisi, kama umma wake, tutafurahia wema na baraka za neema hizi, kwa sababu wema na baraka za Nabii (sallallahu ‘alaihi wasallam) hutiririka kwa umma wake. Kwa hiyo, tukiwa miongoni wa Ummah wake, tunatakiwa pia kuonyesha shukurani kwa Allah Ta‘ala kwa kuswali na kujitolea.

Aina moja ya kujitolea ni kujitolea kwa kuchinja (idi kubwa) jinsi tunavyo jua; lakini vile vile kuna aina nyingi za kujitolea ambazo tunapaswa pia kutoa yenye kuhusiana na maisha yetu, mali na matendo yetu.

Aina zingine za kujitolea pia huingia chini ya juhudi za ujumla ambazo umma unahitaji kuzifanya kwa ajili ya Allah Ta’ala.

إِنَّ شَانِئَكَ هُوَ الْأَبْتَرُ ‎﴿٣﴾‏

Hakika, anayekuchukia atakatiliwa mbali.

Neno ‘Abtar’ lililotajwa katika aya hii linamaanisha yule ambaye kizazi chake na nasaba yake imekatwa.

Wakati watoto wa kiume wa Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam), Qaasim na Ibrahim (Radhiya Allaahu anhuma), walipofariki, maadui waliona nafasi ya kumdhihaki na kumchokoza. Walisema kwamba yeye si mtu wa kuwa na wasiwasi naye au kumjali, kwa sababu kizazi chake kimekatwa. Kama vile uzazi wake umekatiliwa mbali, hivi karibuni maono na kazi yake pia itakatizwa kwa sababu kwa ujumla, ni kizazi cha mtu kinachopeleka utume wake mbele.

Kwa hiyo, katika aya hii, Allah Ta’ala anamfariji Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) na kumwambia, “Mwenye kukuchukia basi atakatiliwa mbali.” (na wewe hutakatiliwa mbali).

Kwa maneno mengine, “Jina lako, utukufu wako, utume wako na fadhila na neema zote ambazo Allah Ta’ala amekupa kwa ajili yako na ummah wako utaendelea mpaka Siku ya Qiyaamah.”

Shariah na kitabu cha kila Nabii mwingine kimefutwa kwa kuja kwake Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) duniani, na ni shariah na kitabu tu cha Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) ndio kitabakia hadi mwisho wa wakati.

Kimsingi, katika aya hii, Allah Ta’ala anamhakikishia Nabii wake kipenzi (Sallallahu ‘alaihi wasallam) kwamba adui yake, ‘Aas bin Waa’il au Ka’ab bin Ashraf, au yoyote mwingine aliyekuwa anamsema vibaya Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) – hivi karibuni watakatiliwa mbali na hakutakuwa mtu hata mmoja wakuwakumbuka. Kwa hiyo, lau isingelikuwa tafsir ya aya hizi au seerah ya Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) , basi majina ya watu hawa yasingeonekana kamwe duniani. Kwa njia hii, watu hawa wamefutwa kabisa kutoka kwa kumbukumbu za wakati.

Kinyume chake, kizazi kilichobarikiwa cha Mtume (Sallallahualaihi wasallam) kinaendelea hadi leo kupitia Faatimah (Radhiya Allaahu anha) na kitaendelea hadi Siku ya Qiyaamah.

Karibu na Qiyaamah, Imaam Mahdi (Radhiyallahu ‘anhu) atawaongoza Waislamu, na atatoka katika kizazi cha Rasulullah (Sallallahualaihi wasallam) kupitia Faatimah (radhiyallahu anha).

Madhumuni ambayo mtu anataka kizazi chake kiendelee ni hasa kwa wao kuweka mbele malengo na maadili ambayo alikuwa akijitahidi kuweka juhudi katika maisha yake yote, akitumaini kwamba lengo na maadili yake yanaweza kuendelea kubaki duniani baada ya kufariki kwake. Kwa hiyo, Ummah wa Nabii (Sallallahu ‘alaihi wasallam ) ni kizazi chake cha kiroho – kwa sababu wanamuamini, kumfuata na kueneza ujumbe wake. Kizazi hiki kitaendelea kustawi na kuongezeka hadi mwisho wa nyakati.

Kwa hiyo, katika pande zote za dunia, hutakuta si mamia au maelfu, bali mamilioni ya watu wanaotaka kutoa mali zao, muda, damu na jasho kwa ajili ya ujumbe wa Nabii (Sallallahu ‘alaihi wasallam). Kwa hiyo, tunaona kwamba mtu mkubwa zaidi duniani ni Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam). Kitabu chake (Qur’an Takatifu) ni kitabu kinachosomwa zaidi ulimwenguni kote na maadui zake wote wamefutiliwa mbali kutoka kwenye uso wa dunia hii.

Somo moja muhimu tunalojifunza kutokana na surah hii ni kwamba tunapokuta kazi yoyote nzuri inafanyika, tunapaswa kuwa na moyo wa kuikumbatia, kuiunga mkono na kuikuza kwa kila njia. Tukifanya hivyo, tutapewa sehemu ya wema katika kazi hio njema.

Kinyume chake, tukiikosoa na kukemea kazi nzuri, basi tutakuwa kama Aas bin Waa’il, adui wa Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam), ambaye alimkosoa Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) kwa kueneza Dini.

Vile vile kama vile alivyokatwa, kupoteza jina lake, sifa na kila kitu kingine, ikiwa tutafuata njia yake, basi pia tutafanyiwa hiyo hiyo.

Kwa hivyo, tukifuata njia ya sunna na kuunga mkono Sunna kwa kila njia, basi Allah Ta’ala atasababisha jina letu na wema wetu kustawi duniani, hata baada ya sisi kuondoka duniani.

About admin

Check Also

Tafseer Ya Surah Lahab

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ تَبَّتْ يَدَا أَبِي لَهَبٍ وَتَبَّ ‎﴿١﴾‏ مَا أَغْنَىٰ عَنْهُ مَالُهُ وَمَا كَسَبَ ‎﴿٢﴾‏ سَيَصْلَىٰ نَارًا …