أَرَأَيْتَ الَّذِي يُكَذِّبُ بِالدِّينِ ﴿١﴾ فَذَٰلِكَ الَّذِي يَدُعُّ الْيَتِيمَ ﴿٢﴾ وَلَا يَحُضُّ عَلَىٰ طَعَامِ الْمِسْكِينِ ﴿٣﴾ فَوَيْلٌ لِّلْمُصَلِّينَ ﴿٤﴾ الَّذِينَ هُمْ عَن صَلَاتِهِمْ سَاهُونَ ﴿٥﴾ الَّذِينَ هُمْ يُرَاءُونَ ﴿٦﴾ وَيَمْنَعُونَ الْمَاعُونَ ﴿٧﴾
Je! Umemwona mwenye kuikataa Hukumu? Kisha yeye ndiye anaye msukuma yatima, na wala hahimizi kulisha masikini. Basi ole wao wanaoswali, ambao wanapuuza Swalah zao. Na wale ambao (wanafanya wema tu) kujionyesha, na wanakataa kutoa (au kukopesha watu) hata vitu vya msingi, vidogo (ambavyo watu wanavihitaji).
أَرَأَيْتَ الَّذِي يُكَذِّبُ بِالدِّينِ ﴿١﴾ فَذَٰلِكَ الَّذِي يَدُعُّ الْيَتِيمَ ﴿٢﴾ وَلَا يَحُضُّ عَلَىٰ طَعَامِ الْمِسْكِينِ ﴿٣﴾
Je! Umemwona mwenye kuikataa Hukumu? Kisha yeye ndiye anaye msukuma yatima, na wala hahimizi kulisha masikini.
Neno ‘Deen’ lina maana tofauti. Maana moja ni Dini ya Uislamu. Maana ya pili ni hukumu. Kwa hivyo, Aayah hii inaweza kurejea kwa kafiri anayeikataa Dini ya Uislamu au Siku ya kuhukumiwa. Kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, aya hizi za mwanzo ziliteremshwa kuhusu kafiri mmoja ‘Aas bin Waa’il ambaye alijulikana kwa ubakhili wake. Vile vile, surah hii ujumbe wake sio tuu kwake bali ujumbe wa surah ni wa watu wote kiujumla na pia unawahusu Waislamu. Kwa hiyo, Waumini wanapaswa pia kupata somo kutokana na surah hii na wajiepushe na vitendo kama vile kuwachukiza mayatima au kuacha kuwalisha masikini.
Utofauti mkubwa kati ya Muumini na Kafiri ni kuamini Siku ya qiyaama na khofu ya kuhukumiwa huko Akhera. Kafiri haamini Siku ya Hukumu, na hivyo haogopi kuhukumiwa Akhera. Kwa hiyo, kuhusu Muumini wa kweli, basi kila wakati anatambua kuwa Allah Ta’ala anamuona na kwamba anatakiwa kutoa hesabu ya matendo yake yote, yawe madogo au makubwa, Siku ya Qiyaamah.
Kwa vile makafiri hamwamini Allah Ta’ala na wala haogopi hisabu Siku ya Qiyaamah, anajiona yuko katika hali ya nguvu. Hamjali yatima wala masikini na anaendelea kujishughulikisha na mali na uwezo alionao, na kusahau kuwa hali zinaweza kubadilika siku zinaofuata, na Allah Taala anaweza kuwa bariki na mali na kuwanyang’anya mali vile vile. Kwa kifupi, tajiri wa leo anaweza kuwa masikini wa kesho, na maskini wa leo anaweza kuwa tajiri wa kesho.
Kwa hiyo, katika Aya hizi, Allah Ta’ala anatuonya na matendo haya mabaya ya kuikadhibisha Siku ya qiyama, kumkimbia yatima na kuacha kuwalisha masikini, na anawahimiza waumini kuwafanyia wema mayatima na masikini.
فَوَيْلٌ لِّلْمُصَلِّينَ ﴿٤﴾ الَّذِينَ هُمْ عَن صَلَاتِهِمْ سَاهُونَ ﴿٥﴾ الَّذِينَ هُمْ يُرَاءُونَ ﴿٦﴾ وَيَمْنَعُونَ الْمَاعُونَ ﴿٧﴾
Basi ole wao wanaoswali, ambao wanapuuza Swalah zao. Na wale ambao (wanafanya wema tu) kujionyesha, na wanakataa kutoa (au kukopesha watu) hata vitu vya msingi, vidogo (ambavyo watu wanavihitaji).
Katika Aya hizi, Allah Ta’ala anazungumza kuhusu wale Waumini wanaopuuza Swalah zao na kuwafanyia watu ubakhili. Wanaposimama kuswali, hawaswali kwa ikhlasi. Bali wanaswali kwa ajili ya kujionyesha tu na ili watu wawachukulie kuwa ni Waislamu wachamungu. Kwa hivyo, wanapokuwa hawako mbele ya watu, basi ima hawaswali Swalah zao, au wanaswali baada ya wakati kupita na kuwa qadhaa, au hawatimizi swala zao jinsi inavyopaswa kutekelezwa, yaani kwa misimamo sahihi, katika wakati sahihi, na kuswali na jamaa msikitini n.k. Kwa hakika, hawana mapenzi ya kweli na kujali Swalah katika nyoyo zao.
Vile vile, hao watu niwa bakhili na wanakataa kuwapa watu hata vitu vya msingi, vidogo ambavyo watu wanavihitaji. Neno halisi lililotumika katika aya hii ni “maa’un”, ambalo maana yake halisi ni ‘vitu vidogo na vya bei nafuu’, kama vile vyombo vya udongo, chumvi, sukari, n.k. Ikiwa mtu anahitaji vitu kama hivyo, basi yule mwenye anavyo anapaswa kumkopesha na kumsaidia mwenye hana.
Neno maa’un pia linaweza kumaanisha zakaah. Kwa maneno mengine, watu hawa wanakataa kutoa zakaah yao ya faradhi. Hii imepokewa kutoka kwa Ali (Radhiya Allaahu anhu) ambaye ametaja kwamba neno maa’uon katika Aya hii linahusu zakaah, kwa sababu zakaah inalipwa kwa kiwango kidogo kulinganisha na mali yote ya mtu.
Kimsingi Aya hizi zinaeleza viwango ambavyo mtu huhukumiwa mbele ya Allah Ta’ala. Mtu wakati wote anatakiwa kuwa na wasiwasi juu ya uhusiano wake na Allah Ta’ala na wasiwasi pia kama anatimiza maamrisho za dini ya Allah Ta’ala kama vile kusimamisha Swalaah katika maisha yake, kutoa zakaah, n.k.
Vile vile, anapaswa kujishughulisha na kutimiza haki anazodaiwa na watu na kuwafanyia wema familia yake, majirani, marafiki, mayatima na masikini. Ikiwa mtu atakuwa bakhili, basi hatatimiza haki ya Allah Taala katika mali yake kwa kutoa zakaah, wala hatatimiza haki anazowapa waja wa Allah Taala kwa kutimiza haki anazodaiwa na masikini, ndugu, majirani na wenginevyo.
Wakati mmoja, Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam ) alikuwa safarini alipotoa amri kwamba wale ambao wana usafiri wa ziada wawasaidie wale ambao hawana usafiri.
Imepokewa kutoka kwa Abu Sa’eed (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa: “Siku moja tulikuwa safarini pamoja na Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam ) ghafla, mtu aliyekuwa amepanda usafiri wake, kaja mbele ya Mtume (Sallallahu ‘alahi wasallam ). Mtu huyo alikuwa katika shida na tabu na alikuwa akitazama kulia na kushoto ili kuona kama kuna yoyote angeweza kumsaidia katika kumtimizia mahitaji yake. Katika tukio hilo, Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) aliwausia Maswahabah (Radhiya Allaahu ‘anhum) akisema, “Mwenye usafiri wa ziada amsaidie yule ambaye hana usafiri. Yule aliye na rizki za ziada awasaidie wenye hawana rizki.” Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam ) akaendelea kutaja aina mbalimbali za mali (ambazo mtu anatakiwa kuzitumia katika sadaqah), akiwahimiza na kuwausia Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) kuzitumia kiasi kwamba tulihisi kama yule aliye na kitu chochote kinachozidi mahitaji yake hana haki ya kukizuia na kubaki nacho (badala, awagawie wenye haja). (Saheeh Muslim #1728)
Kutokana na Hadithi hii, tunaelewa kwamba hali ya Muumini ni kwamba asiwe mbinafsi na mwenye majivuno, na anajali tu maendeleo ya kidunia ya nafsi yake na familia yake wa karibu. Badala, muumini wa kweli anawajali Waislamu kwa ujumla na anatafuta fursa za kuwasaidia watu. Kwa hivyo, mtu kama huyo yuko tayari kusaidia watu walio karibu naye na huonyesha huruma kwa watu wote, iwe ni familia, majirani, marafiki au hata maskini mwenye mahitaji.