Tafseer Ya Surah Al-Qaar’iah

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمٰنِ الرَّحِيْمِ

الْقَارِعَةُ ‎﴿١﴾‏ مَا الْقَارِعَةُ ‎﴿٢﴾‏ وَمَآ اَدْرٰىكَ مَا الْقَارِعَةُ ‎﴿٣﴾‏ يَوْمَ يَكُونُ النَّاسُ كَالْفَرَاشِ الْمَبْثُوثِ ‎﴿٤﴾‏ وَتَكُونُ الْجِبَالُ كَالْعِهْنِ الْمَنفُوشِ ‎﴿٥﴾ فَاَمَّا مَن ثَقُلَتْ مَوَازِيْنُهُۥ ‎﴿٦﴾‏ فَهُوَ فِى عِيشَةٍ رَّاضِيَةٍ ‎﴿٧﴾‏ وَاَمَّا مَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُۥ ‎﴿٨﴾‏ فَاُمُّهُۥ هَاوِيَةٌ ‎﴿٩﴾‏ وَمَآ اَدْرٰىكَ مَا هِيَهْ ‎﴿١٠﴾‏ نَارٌ حَامِيَةٌ ‎﴿١١﴾‏

Siku ya tukio la Mpigiko; na ni siku gani ya tukio la Mpigiko? Na nini kitakujulisha kuhusiana na tukio la Mpigiko? Siku ambayo watu watakuwa kama nondo walio tawanyika; na milima itakuwa kama sufi zilizo chambuliwa. Basi ambaye mizani yake (ya amali) ni nzito, atakuwa katika maisha ya furaha. Na ama yule ambaye mizani yake ni nyepesi, makazi yake yatakuwa “Haawiyah” (shimo la Jahannam). Na nini kitacho kujulisha nini hiyo? (Ni) moto mkali.

 يَوْمَ يَكُونُ النَّاسُ كَالْفَرَاشِ الْمَبْثُوثِ ‎﴿٤﴾

Siku ambayo watu watakuwa kama nondo walio tawanyika;

Katika surah hii, Allah Ta’ala anaelezea hali ya kusikitisha ya watu siku ya Qiyaamah. Siku hiyo, watu watakimbia huku na huko kwa kuchanganyikiwa na kufadhaika kutokana na kuzidiwa na woga wa uwajibikaji na hesabu. Allah Ta’ala anaelezea tukio hilo katika Aya nyingine ya Quraan Takatifu akisema: Siku hiyo mtu atamkimbia ndugu yake mwenyewe, na mama yake na baba yake, na mke wake na watoto zake. Kila mmoja wao, Siku hiyo, atakuwa na wasiwasi wa kutosha kiasi cha kumfanya asijali wengine. (Sura Abas: 34-37)

Katika Aya hii, Allah Ta’ala anaeleza hali ya kuchanganyikiwa na kufadhaika baina ya watu Siku ya Qiyaamah, na namna watakavyotawanyika wao kwa wao. Allah Ta’ala Akisema: “Siku ambayo watu watakuwa kama nondo waliotawanyika. Kwa maneno mengine, watu watatawanyika wao kwa wao katika hali ya unyonge na dhiki, kama vile nondo wanavyotawanyika kutoka kwa kila mmoja.

وَتَكُونُ الْجِبَالُ كَالْعِهْنِ الْمَنفُوشِ ‎﴿٥﴾

Na milima itakuwa kama sufi zilizo chambuliwa.

Kwa sasa, milima duniani imesimama kwa uthabiti kiasi kwamba hakuna kitu kinachoweza kuisogeza. Lakini, siku hiyo milima itakapovunjwa-vunjwa, itatawanyika kama matete na vipande vya sufu zilizo chambuliwa.

فَاَمَّا مَن ثَقُلَتْ مَوَازِيْنُهُۥ ‎﴿٦﴾‏ فَهُوَ فِى عِيشَةٍ رَّاضِيَةٍ ‎﴿٧﴾

Basi ambaye mizani yake (ya amali) ni nzito, atakuwa katika maisha ya furaha.

Siku ya Qiyaamah, matendo mema na mabaya ya watu yatapimwa kwenye mizani. Kutokana na Aya na Hadithi mbalimbali tunaelewa kwamba mizani ya matendo itafanyika mara mbili katika Siku ya Qiyaamah.

Mizani ya kwanza itafanyika kupima Imaan ya wale walioleta Imaan. Katika mizani hii kutatokea utengano baina ya waumini na makafiri.

Kipimo cha pili kitafanyika ili kupambanua kati ya matendo mema na mabaya ya waumini.

Katika surah hii, mizani iliyotajwa kwa dhahiri inarejelea kwenye mizani ya kwanza ambayo mizani ya kila Muumini itakuwa kizito, bila kujali amali zake nyingine, na mizani ya makafiri itakuwa nyepesi.

Katika Hadith, kuna baadhi ya matendo mema yametajwa ambayo yatasababisha mizani ya matendo kuwa nzito Siku ya Qiyaamah, na hivyo kupata malipo makubwa zaidi. Miongoni mwa vitendo hivi vyema ni vitendo vitano:

1) Kufanya vitendo kwa uaminifu. Sifa ya ikhlaas (unyofu) husababisha kitendo kupanda kwa ubora na thamani. Kadiri kiwango cha ikhlasi kinavyokuwa kikubwa katika matendo yetu, ndivyo kitendo kitakavyokuwa na uzito zaidi katika mizani ya matendo na ndivyo itakavyopata malipo makubwa zaidi Siku ya Qiyaamah.

2) Kufanya vitendo vinavyoafikiana na sunnah. Uzuri na ubora wa kitendo ni kiungo na kipengele kinacholeta uzito juu ya mizani ya matendo na kusababisha thawabu kubwa zaidi kupatikana. Sio wingi wa kitendo kinacholeta uzito. Ikiwa kitendo kitaafikiana na Sunnah ya Mubaraka ya Rasulullah (Sallallaahu ‘alaihi wasallam), kinapata uzuri na ubora.

3) Kukaa kimya na kutozungumza bila ya lazima. Sifa hii, na kukaa kimya katika kumkumbuka Allah Ta‘ala, unazingatiwa miongoni mwa matendo mema ambayo yatathibitika kuwa na uzito kwenye mizani Siku ya Qiyaamah.

4) Kuwa na tabia nzuri. Kuamiliana na watu kwa heshima na kuonyesha tabia njema mbele yao ni miongoni mwa vitendo vikubwa na vizito katika mizani Siku ya Qiyaamah.

5) Kusoma kalimah “Laa ilaaha illallah”. Imepokewa katika Hadith kwamba kisomo cha kalimah kitakuwa na uzito mkubwa siku ya Qiyaamah, kwa sharti isomwe na ikhlasi.

Matendo haya yana thamani kubwa kiasi kwamba kila Muumini anapaswa kuwekeza ndani yake, kwa sababu yataleta kheri katika vitabu vyetu vya matendo na yataipa uzito mizani yetu Siku ya Qiyaamah.

Vile vile Muumini anatakiwa kujiepusha na vitendo ambavyo vitasababisha matendo vyetu vipoteze mng’aro na uzito wake kwenye mizani Siku ya Qiyaamah. Hadith inaeleza kwamba kuna matendo kadhaa ambayo yanasababisha vitendo kupoteza thamani na uzito wake. Miongoni mwa hatua hizo ni zifuatazo:

1) Kuwasababishia watu maumivu au kuwakandamiza kwa njia yoyote ile. Hadith inaeleza kuwa mtu atakuja Siku ya Qiyaamah na milima ya amali njema. Lakini, alikuwa ni mtu wa kuwatukana watu, kuwadhulumu watu, kukashifu watu, kupora mali za watu, n.k.  Kutokana na matendo haya maovu, mema yote aliyoyapata yatatolewa kwa wale aliowadhulumu.

2) Kufanya vitendo bila ikhlaas, kwa maonyesho na kujionyesha. Imepokewa katika Hadith kwamba Siku ya Qiyaamah, watu watatu wa mwanzo watakaoingia Jahannum watakuwa ni Aalim (sheikh) aliyeeneza Dini katika maisha yake yote, tajiri aliyetoa mali nyingi katika sadaka, na mujaahid aliyepigana Jihaad. Watu wote hawa watatupwa kichwakichwa katika moto wa Jahannam kutokana na kutokuwa na ikhlaas na kufanya vitendo vya kujionyesha.

Katika Hadith moja, imetajwa kuwa mwenye kuswali au kufunga kwa nia ya kujionyesha ametenda aina ya shirki (kumshirikisha Allah Ta’ala) katika mambo mema aliyoyafanya, na mtu huyo atopata malipo yoyote kwa wema alioufanya.

Katika Hadith nyingine, Rasulullah (Sallallaahu ‘alaihi wasallam) ametaja kwamba mtu yoyote aliyefanya jambo jema kwa ajili ya kujionyesha, Siku ya Qiyaamah, Allah Ta’ala atamwambia, “Sina mshirika. Kwa hivyo, kwa kuwa mlinishirikisha katika jambo jema, hamtapata malipo yoyote kutoka Kwangu. Unaweza kwenda kutafuta malipo yako kwa wale wote uliowafanyia kitendo hicho.”

3) Kutumia ulevi au kutumia haramu yoyote. Imepokewa katika Hadith kwamba mwenye kula haramu au kujiingiza katika ulevi, du‘aa zake na ibaadah zake hazikubaliwi. Kwa hivyo, Siku ya Qiyaamah, mtu hatapata ujira juu ya mizani kwa matendo mema anayoyafanya, isipokuwa akitubia dhambi na kurekebisha maisha yake.

4) Kuacha Swalaah. Kuacha Swalaah ni sababu ya kupotea kwa amali njema. Kwa hivyo, Siku ya Qiyaamah, kwa sababu ya mtu kuacha Swalaah yake, hatapata thawabu kubwa alizozitarajia kwenye mizani kwa matendo yake mema.

5) Kutotoa zaka. Imepokewa katika Hadith kwamba asiyetoa zaka yake, basi mbali na dhambi anayoipata kwa kutotoa zaka, atanyimwa ujira wa Swalaah anayoifanya. Kwa maneno mengine, japokuwa itahesabiwa kama kaswali faradhi, lakini hatapata malipo ya Swalaah.

Kwa hiyo, nyakati zote, mtu anapaswa kuwa na wasiwasi kuhusu matendo anayofanya. Kila tendo njema au mbaya, hata lionekane dogo kiasi gani – mtu hapaswi kuliona kuwa lisilo na maana. Inawezekana kwamba kitendo ambacho mtu anaweza kukiona kuwa ni kidogo, lakini akakitekeleza kwa ikhlaas na kuafikiana na sunna, kinaweza kuwa ni sababu ya mizani yake kuwa na uzito, na sababu ya kuokoka kwake, kusamehewa na kuingia katika Jannah.

About admin

Check Also

Tafseer Ya Surah Lahab

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ تَبَّتْ يَدَا أَبِي لَهَبٍ وَتَبَّ ‎﴿١﴾‏ مَا أَغْنَىٰ عَنْهُ مَالُهُ وَمَا كَسَبَ ‎﴿٢﴾‏ سَيَصْلَىٰ نَارًا …