Dalili Ndogo Kuongezeka Kabla ya Dalili Kubwa
Wakati wa kuzitazama dalili ndogo za Qiyamah zilizoandikwa katika Hadith, mtu hutambua kwamba ni kichocheo cha kuja kwa dalili kubwa. Kwa hivyo, kwa kweli, dalili ndogo zitaongezeka kwa wingi, hadi mwishoni zitafikia kilele kwa kuja kwa dalili kubwa.
Katika hadith fulani, Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) alielezea fitna kuongezeka kwa wingi kwa kuzilinganisha na giza la usiku ambao huongezeka giza jinsi usiku unavyozidi. Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) amesema: “Kimbilieni kwenye matendo mema kabla ya kuanza kwa fitnah ambazo zitakuwa kama sehemu za usiku wa giza. Mtu atakuwa Muumini asubuhi na akawa kafiri jioni, au mtu atakuwa Muumini jioni na akawa kafiri ifikapo asubuhi. Atakuwa tayari kuiuza Dini yake kwa kumiliki kidogo ya ulimwengu.” (Sahih Muslim #118)
Miongoni mwa mambo yatakayochochea ukali wa fitnah ni kupenda mali. Kwa ajili ya mali, watu watakuwa tayari kuondoa maadili yao ya Deeni, staha na aibu. Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) amesema:
Kabla ya Qiyaamah, (utaona) watu wanatoa salaam kwa watu maalum tu, na (utaona) biashara zinaendelea vizuri kiasi kwamba wanawake watatoka majumbani mwao ili kuwasaidia waume zao katika biashara, na (utaona) mahusiano ya familia kukatwa (kwa sababu ya kupenda mali)… (Musnad Ahmed #3870)
Fitnah Tano za Uharibifu Zinazojumuisha Fitnah zote
Wakati fitna zilizoandikwa katika Hadith mbalimbali zinapochunguzwa kiujumla, zinaweza kuingizwa katika fitnah tano zenye uharibifu. Fitnah hizi tano za uharibifu zinajumuisha kiasi kwamba ndio sababu za msingi za kuleta madhara makubwa kwa Dini ya mtu na huvutia maovu mengine baada yake. Fitnah hizi tano zenye uharibifu ni: (1) Kuwaiga Makafiri, Mayahudi na Wakristo (2) Kupoteza hayaa [aibu na staha] (3) Kupoteza heshima ya Dini na haki za watu (4) Kupenda mali na kufuata matamanio (5) Kuwa na fikraa zako mwenyewe na kutotaka kujitiisha na Dini na Maulamaa wachamungu waongofu.